Mwalimu wa somo la jiografia akiwa kazini 2011 |
Wahenga walisema, mtoto anapozaliwa ni ishara kuwa Mwenyezi Mungu bado anaipenda dunia. Msemo huu una ukweli pia katika sekta ya elimu. Unapokutana na walimu bora, unakuwa na hisia na pia uhakika na taifa la watu wenye fikra yakinifu, wataalamu wake lenyewe, maendeleo ya kweli na kadhalika.
Maendeleo ya kweli yataletwa kupitia matumizi mazuri na sahihi ya ubongo wa binadamu; njia mojawapo ya kuufanya ubongo huu ufanye kazi yake sawa sawa ni mafunzo. Mafunzo hayo yaweza kuwa nyumbani mtoto angali mdogo kabisa kabla ya kwenda shule tunazozifahamu. Kwa watu wengi mafunzo yanayotambulika rasmi huanzia shuleni, lakini kumbe mtoto huweza kufunzwa hata kabla ya kuanza kuhudhuria shule rasmi. Hapa hata hivyo najadili juu ya shule rasmi tunazozifahamu.
Mwezi Novemba 2011, STELLA MARIS MTWARA UNIVERSITY COLLEGE (STEMMUCO)(Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT) kiliandaa mitihani maalumu kuwapima wanachuo ambao ni walimu wa baadaye.
Mitihani hiyo ilenge kupima mambo anuai; uwezo wa kujieleza kwa lugha ya kiingereza, uwezo wa kuwasilisha mada, kujiamini kwa mwalimu, uwezo wa kutafsiri somo katika mazingira ya usasa, na kadhalika.
Walimu wengi walitia fora sana katika ufundishaji; walijiamini, waliwasilisha mada vyema kabisa, walitumia vielelezo vya masomo na waliwashirikisha wanafunzi wao vyema. Hata hivyo wengine bado wanahitaji kuboresha zaidi kipengele cha tafsiri ya somo kwenda kwenye maisha halisi ya leo na ya usasa. Mwanafunzi atavutika kujifunza zaidi pale atakapogundua kuwa kwa kusoma mada fulani darasani anaweza akaitumia kucheza na rafikize ama akamweleza bibi yake kijijini akatambua na kuitumia mbinu husika. Mfano kwenye somo la utunzaji wa vyakula. Maeneo mengi ya kanda ya ziwa hulimwa kwa wingi viazi vitamu, huwa vingi na si rahisi kula vyote katika msimu mmoja. Wakulima wa ukanda huo, wamebuni njia ya kuvihifadhi viazi kwa njia mbili.
Njia ya kwanza ni kuvimenya viazi hivyo vingali vibichi na kisha kuvichanja vipande vidogo vidogo na kuvianika juani kwenye uchanja maalumu kwa kazi hiyo ama kwenye paa la nyumba. Vikikauka huwa vyeupe na huitwa michembe.
Njia ya pili; viazi vitamu huchemshwa na kisha humenywa maganda yake na kisha zoezi la kuvichanja kama vile vibichi hufuata. Vikikauka, kwa kuwa vilichemshwa huwa na rangi ya dhahabu, ni vitamu sana na hujulikana kwa jina la matobolwa. Huifadhiwa katika magunia ama ghala na huliwa hasa wakati wa msimu wa kilimo, huliwa kama sehemu ya kifungua kinywa lakini pia hata mlo wa jioni.
Tafsiri ya somo katika maisha ya sasa ama halisi inaleta hamu na maana zaidi ya kujifunza na hiyo itawavutia watoto wetu wajifunze zaidi.
Mbinu hizo zitumike zaidi kwenye masomo yote lakini hasa na muhimu kwenye hisabati, hili ni somo linalosumbua wanafunzi wengi nchini, na masomo mengine ya sayansi, biolojia, fizikia, na kemia.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa na matumaini ya maendeleo ya kweli katika nchi yetu vinginezo tutaendelea kushuhudia wengine wakitupita kimaendeleo na sisi tukiendelea kuwa soko la bidhaa zao kila uchao.
Mandalu