Sunday, December 25, 2011

YOSEFU NA VIJANA WA LEO


Yosefu ama Yusufu alikuwa baba mlishi wa mtoto Yesu. Ndugu huyu alikuwa na mchumba aliyejulikana kwa jina la Maria ama Mariamu; wote wawili walikuwa Wayahudi. Kabla ya kuishi pamoja kama mume na mke, Mariamu alionekana kuwa mjamzito. Kwa taratibu za kiyahudi, husasani za wakati ule, Yosefu alitakiwa kutoa taarifa kwa wahusika na binti huyo angeuwawa kwa kupigwa mawe. Yosefu lakini aliadhimia kumuacha kimya kimya yule binti. Maandiko yanatuambia kuwa Mwenyezi aliingilia kati na hatimaye Yosefu akamchukua mchumba wake.

Vijana wa kiume hapa Tanzania na duniani kote wanaweza kujifunza tabia hiyo ya Yosefu. Vijana wetu wa kiume wakijifunza tabia hiyo basi matatizo mengi yanayoisibu jamii yetu yanaweza kupungua ama kuisha kabisa.

Vijana hawawezi kukataa mimba wanazowapa mabinti na kisha kuwakana. Hii itasaidia kupunguza watoto wa mitaani. Miji yetu mingi mikubwa ina watoto wengi wa mitaani; watoto hawa kwa kiasi fulani ni matokeo ya kina kaka na kina baba kuwatelekeza wake na ama wachumba wao, wao pekee na watoto. Basi sherehe hizi za Krismasi tunaweza kuzitumia kuwakumbuka watoto wa mitaani na sisi kubadilisha tabia zetu kwa mfano wa Yosefu.

No comments:

Post a Comment