Sunday, October 7, 2018

WHO WILL CRY WHEN YOU DIE? - NANI ATALIA UTAKAPOKUFA?



Tafakuri ya leo; Uchambuzi wa kitabu kiitwacho WHO WILL CRY WHEN YOU DIE Na Robin Sharma.

Habari mpendwa msomaji wa makala hizi naamini unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku,basi leo nimetamani tupate muendelezo na tuendelee kujifunza katika mambo mazuri ambayo mwandishi Robin Sharma ametushirikisha katika kitabu chake cha Who will cry when you die.Kwenye makala iliyopita tulipata kuona mambo tisa kati ya 101 basi leo tuendelee kujifunza mambo mengine machache ambayo tukiyatenda hakika itakuwa ni faida kwetu na kwa vizazi vijavyo.

Jambo la kwanza ni kuishi kinyenyekevu(be humble),mtu yeyote aishiye maisha ya unyenyekevu kwanza kabisa huwa tayari kujifunza kwa wengine lakini pia hujijengea mahusiano bora na watu wanaomzunguka na jamii kwa ujumla,hivyo unyenyekevu ni silaha kubwa sana ya kuishi nayo,jamii itakuwa ikijifunza kwako na itamani kuendelea kuwa na wewe na hata siku ukifa itakukumbuka na kukulilia sana.

Jitoe kubeba hatari kubwa(risks).Siku zote mtu aliyeradhi kubeba hatari kubwa huwa ndiye anayepata matokeo makubwa,hivyo basi usiwe muoga kubeba hatari kubwa katika maisha yako binafsi,jamii na hata kwa taifa kwa ujumla.

Acha kuwa na hofu na vitu ambavyo huna uwezo wa kuvibadilisha.Hii pia ni moja ya changamoto kubwa sana watu wanayokutana nayo katika maisha yao ya kila siku,unakuta mtu anawaza mambo makubwa na ya hatari ambayo hayawezi kutokea ama hana uwezo nao wa kuyabadilisha,ndugu yangu acha kuwaza vitu vilivyo nje ya uwezo wako,maana hatari yake ni kuwa utajikuta ukipoteza nishati nyingi huku ukipata matokeo kidogo na hii ni hasara.

Penda kazi yako.Kuna msemo unasema "kazi mbaya ukiwa nayo",hii huonyesha ni jinsi gani watu hudharau kazi zao pindi pale wanapokuwa wakizifanya na kujiona kama wao ni watu duni tofauti na wengine,lakini dhana hii ni potofu,unachotakiwa ni kuipenda kazi yako hata kama ni ndogo kiasi gani au wewe unaiona ni dunia kiasi gani utakapoipenda kazi yako utaifanya kwa ufanisi na hata wale uwapao huduma yako watavutiwa sana na watakukumbuka sana hata siku ukiwa haupo tena duniani.

Pia tuwapo katika shughuli zetu za kazi baada ya kumaliza wakati mwingine hujikuta tukiwa tumechoka na wenye mawazo mengi sana,lakini unachotakiwa kufanya ni kutafuta namna ya kuondoa hayo mawazo ya kazi kabla haujafika kwenye mlango wa nyumbani,kumbuka kwamba na familia nayo inatamani uwepo wako hivyo unapofika huku ukiwa na mawazo hutakuwa na uwezo wa kushirikiana vyema na familia yako na hii hupelekea kupunguza mahusiano mazuri na familia yako.Unaweza sikiliza miziki tulivu hii itakusaidia kukuweka sawa kiakili kabla hujafika nyumbani.

Kusanya nukuu(Quotes) zote uzipendazo.Nukuu za watu wakubwa ama wabobezi wa jambo fulani ni moja kati ya vitu muhimu sana vinavyozidisha hamasa(inspiration) kwa mtu mwingine kutenda jambo kama hilo.Kusanya nukuu uzipendazo zitakusaidia kukupa msukumo wa kufanya mambo makubwa.

Andika tena historia ya maisha yako.Uandishi wa historia za maisha yetu ni jambo muhimu sana japo si wengi wenye utamaduni wa kufanya hivyo,wengi huupuuzia tu na kuona kuwa hamna haja ya kufanya hivyo,lakini wakiwa hawajui kuwa wanapoteza kitu kikubwa sana.Unapoandika historia ya maisha yako husaidia kujitathimini kwa siku za mbeleni kuwa wapi ulipotoka na wapi ulipo sasa,lakini pia kuacha historia yako siku ukifa ni alama pia.

Piga picha nyingi kadiri uwezavyo.Katika jambo jingine muhimu sana japo laonekana kama ni la kawaida kawaida ni hili la upigaji wa picha.Picha zina faida nyingi kwanza ni kumbukumbuku,lakini pia hukuonyesha taswira halisi ya maisha yako wapi ulipokuwa na wapi ulipo sasa,siku ukifa watu watazitazama picha zako na kuendelea kukukumbuka daima,anza leo kupiga picha na uziweke kwenye kumbukumbu nzuri ikiwa ni kwenye nakala tete(soft copy) au hata kwenye nakala ngumu(hard kopi).

Wenye hekima wakubwa walioishi miaka ya zamani walisema; ukitaka kuishi maisha ya kikamilifu fanya vitu vitatu kabla hujafikwa na umauti,vitu hivyo ni,ZAA MTOTO,PANDA MTI na ANDIKA KITABU,hivi vitu vitatu si lazima uvifanye vyote japo ukiweza kuvitenda vyote ni heri.Ukifanikiwa kuwa navyo vitu hivi huwa ni urithi mkubwa utakaokuja kuuacha duniani,hata siku ukifa lakini hazina hii itaishi kwa miaka mingi sana.

Mwisho kabisa Ishi maisha ya kikamilifu ili uje kufa ukiwa mtu mwenye furaha.Hapa lipo somo kubwa sana watu wamekuwa wakiishi mambo ambayo sio kusudio lao waliloitiwa duniani,unakuta mtu anasoma uhasibu kwa sababu familia yao nzima ni wahasibu lakini yeye fani hiyo haikiwa wito wake, na hii hupelekea watu kuishi maisha yenye huzuni na mateso makubwa,inachotakiwa ni mtu uishi kikamilifu katika lile kusudio lako uliloitiwa hii itakufanya uishi kwa amani na hata siku ukifa utakufa ukiwa na furaha.

Haya ni machache niliyotamani nikushirikishe mpenzi msomaji,utakapopata wasaa wa kukisoma kitabu hiki hakika utajifunza mengi zaidi.Ruhusa kuwashirikisha na wengine tunaoona wana kiu ya kupata maarifa na kama utakuwa unahitaji kitabu hiki utanipata kwa barua pepe na namba za simu nitakazo kuachia.Nikutakie heri sana wewe unaenda kuchukua hatua ya kufanyia kazi.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha, mchambuzi wa vitabu na mshairi;

Marko Kinyafu
+255 714 129 520
Dar es salaam,Tanzania.

HAIJALISHI UMESHAPOTEZA MUDA KWA KIASI GANI,NAFASI YA KUFIKA KULE UNAPOTAKA KUFIKA BADO IPO KAMA UKIAMUA LEO.


No comments:

Post a Comment