Friday, October 5, 2018

WHO WILL CRY WHEN YOU DIE - NANI ATAKULILIA SIKU UKIFA?


Tafakuri ya uchambuzi wa kitabu kiitwacho: WHO WILL CRY WHEN YOU DIE (Nani atakulilia siku ukifa?),Na Robin Sharma.

Habari mpenzi msomaji makala hizi,ninatumai u mzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku,leo nimekuja na uchambuzi wa kitabu cha mwandishi Robin Sharma(WHO WILL CRY WHEN YOU DIE)  nakukaribisha nawe usome uchambuzi huu naamini kuna mengi utaenda kujifunza.

Kwanza kabisa katika maisha haya tunayoishi lazima tukumbe kuwa ipo siku yana ukomo wake,hakuna ambaye ataishi milele.Sasa je ulishawahi kujiuliza nani atakulilia siku ukifa?,mwandishi Robin Sharma anaeleza mambo 101 katika kitabu hiki lakini embu twende kuona haya machache na siku baada ya siku tutazidi kujifunza mengine.Karibu,

1.Chunguza na ujue wito wako ni upi? yaani uliletwa duniani ili uje kufanya nini? ukikaa na kupata jawabu,anza kuishi kwa lile kusudi uliloitiwa kuja kulifanya duniani ili uache alama yenye kukumbukwa na kila mtu hata siku ukiwa haupo tena duniani.

2.Jifunze kuwa na shukrani kwa watu,jijengee tabia ya kushukuru hata kama ulichopewa ni kidogo ila ukiweza kuthamini kilicho kidogo basi utaweza kuthamini hata kilicho kikubwa pia.

3.Simamia mitazamo yako,ili utimize lile kusudi ulilolipanga kulitekeleza.

4.Jifunze kuwa na nidhamu binafsi(self discipline),hii itakusaidia kuwa na nidhamu katika utendaji wa mambo yako bila ya kuyumbishwa tena utayatimiza kwa wakati muafaka.

5.Weka kumbukumbu ya yale uyafanyayo kila siku,andika katika notibuku yako ili uweke kumbukumbu na upate tathimini ni wapi pa kujirekebisha.

6.Jijengee tabia ya kuwa muaminifu.Unapotoa ahadi na ukashindwa kuitekeleza jua kwamba uaminifu wako unapotea kwa watu na mwisho wa siku utajikuta ukiangukia katika mahusiano mabaya na watu.Kaa chini kisha jitafakari ni mambo mangapi uliyoahidi ndani ya wiki na hujayatekeleza? ukipata jibu tafuta njia ya kujiboresha ili usirudie makosa.

7.Anza siku yako vizuri.Asubuhi ukiamka tenga japo dakika 30 za kujipanga kwa siku yako ujue kuwa itakwendaje na angalia tathimini ya siku yako iliyopita ila leo ufanye mambo kwa uzuri zaidi.

8.Jifunze kusema hapana.Hapa ipo shida kwa wengi,watu wanashindwa kujizuia kufanya mambo hata ambayo hayana faida yoyote kwao,embu jijengee tabia ya kusema hapana sio kila kitu ukiambiwa utende basi unakuwa mwepesi kutenda,ukifanya hivi itakusaidia kuokoa muda wako na kufanya mambo kwa uzuri zaidi.

9.Tenga siku yako ya mapumziko,jiwekee muda wako hata kama si siku nzima ila tenga masaa utakayopumzika na kupumzisha akili,ikiwa ni pamoja na kukaa na familia ama ndugu kisha ujipange kwa mwanzo mpya wa juma linalofuata.

Machache haya yanaweza kukusaidia endapo utachukua hatua ya utendaji,nami nikutakie kila heri katika hatua unayoenda kuchukua ya kufanya maamuzi ya kutenda.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha,mshairi na mchambuzi wa vitabu;
Marko Kinyafu
+255 714 129 520
Kinyafumarcos@gmail.com.

AMKA HAPO ULIPOKAA KUNA MAVUMBI,SIMAMA UJIFUTE NA UANZE KUSONGA MBELE.

No comments:

Post a Comment