Image by google |
Hivi karibuni nimesikia kutoka radio Maria Tanzania kuwa wana mpango wa kuanzisha kipindi kipya juu ya maisha. Nimesikia wanauliza maisha ni nini? Swali hilo limenivutia kufanya tafakari. Kisha tafakari hiyo nikaona vyema kuwashirikisha watakaopata fursa ya kutembelea ukurasa huu.
Maisha ni nini? Ni swali linalohitaji kufikiria ili kulijibu na hakika mtu hawezi kutoa jibu la maana kama atafanya hivyo bila tafakari. Swali hili lahitaji maelezo ya utangulizi kabla ya kueleza maana ya maisha. Maisha yanahusu viumbe hai, swali letu linamlega hasa binadamu nami nitamuelezea binadamu bila kwenda kwenye falsafa ya ndani ya binadamu - philosophical anthropology, nitamuelezea binadamu kwa lugha nyepesi kabisa ili kila msomaji aelewe. Hivyo basi kwa kuanza na kiumbe huyu, binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi zaidi kuliko viumbe wengine.
Kiumbe huyu huanza safari ya maisha baada ya mtu mume na mtu mke kushiriki tendo la ndoa na kutungwa mimba. Kisha kutungwa mimba kiumbe kipya kinaanza kuishi ndani ya mji wa uzazi wa mwanamke. Kuishi kwa kiumbe ndani ya mwanamke kunatupatia fursa ya kurudi kwenye swali letu la msingi la maisha, yaani maisha ni nini hasa?
Maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu toka kutungwa mimba hadi pale moyo (kiungo chenye kazi ya kusukuma damu mwilini sehemu zote za mwili na hivyo kuurutubisha mwili kwani damu ndiyo njia kuu ya usafirishaji mwilini) utakapokoma kufanya kazi yake.
Katika maisha ya kila binadamu kuna shughuli zinazofanana kwa viumbe wote na kuna shughuli zinazotofautiana toka binadamu mmoja hadi mwingine. Kwa kawaidaa shughuli zote za kimaumbile za binadamu hufanana. Shughuli hizo ni pamoja na zile zifanyikazo ndani ya mwili wa binadamu; ndani ya mwili wa binadamu kuna mifumo zaidi ya kumi inayoshirikiana kati yao na pia ikipata ushirikiano na idara kadhaa mwilini. Baadhi ya mifumo iliyo mwilini kwa binadamu ni pamoja na mfumo wa usafirishaji ambapo moyo na mishipa mwilini husafirisha damu na vyakula sehemu zote za mwili. Upumuaji ni mfumo unaotumia idara za pua, mapafu na kadhalika kuwezesha upumuaji wa mwili. Utoaji taka mwilini huhusisha idara kadhaa na hata mifumo mingine kufanya kazi hiyo...
Pamoja na shughuli zinazofanana kwa binadamu wote kuna mahitaji ya lazima ambayo ni muhimu kwa viumbe wote hao bila kuzingatia nafasi zao kijamii, kiuchumi na kadhalika. Chakula, hewa safi, na hifadhi ya namna fulani ni kati ya mahitaji ya lazima kwa binadamu wote.
Ili aweze kuishi vyema na mwili wake ufanye kazi, binadamu analazimika kula; lazima apate chakula katika kipindi fulani ili mwili wake uendelee kupata mahitaji na virutubisho vinavyouwezesha mwili kuendelea kuishi, hali kadhalika kwa hewa safi. Ili mwili uendelee na kazi zake lazima upate hewa safi ili kubadilishana kwa hewa safi (Okisijeni O2) na hewa chafu (Kaboni diokisaidi CO2) kuendelee kufanyika. Binadamu wote huhitaji hifadhi ya namna fulani; toka kwenye mavazi hadi nyumba ya kujihifadhi, ni ubora tu ndiyo hutofautiana toka mmoja hadi mwingine.
Tunapojiuliza maisha ni nini kuna jambo la lazima kuligusa pia. Nini lengo la maisha? LENGO KUU LA MAISHA NI KUTAFUTA FURAHA. Kwenye dini tunaambiwa lengo kuu la maisha ni kumtumikia Mungu kupitia huduma kwa binadamu wenzetu na mwisho turudi kwa Mungu. Kwahiyo, kwa mara nyingine, kwa binadamu wote lengo kuu la maisha ni kutafuta furaha. Binadamu wote shughuli zetu zote, ama kwa kujua ama kwa kutokufahamu, ni harakati za kutafuta furaha na hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote binadamu anazozifanya katika harakati za kusaka furaha.
Binadamu wote bila kasoro, lengo la maisha yetu ni kusaka furaha. Tuliona mwanzoni kuwa binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi mkubwa kuliko viumbe wengine wote. Utashi na akili nyingi aliyonayo binadamu humpatia fursa ya kuitafuta furaha kwa namna ya kipekee kwa jinsi ya maumbile na muundo wake unaotokana na mpangilio wa 'genes' zake, ushawishi wa mazingira aliyolelewa na pia aina na ubora wa chakula alacho hasa toka utotoni. Ndiyo maana kuna wenye hutafuta furaha kwa kufanya kazi halali kwa bidii, wengine kwa kufanya kazi haramu kwa bidii (kazi haramu huleta furaha ya muda tu kwa kuwa huwadhuru binadamu wengine), wengine kwa namna yao kulingana na vipaji vyao na wengine kwa namna zao kwa namna namna.
Hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu katika harakati za kusaka furaha katika kipindi chote ambapo moyo unafanya kazi ya kusukuma damu mwilini!
Martin Mandalu
Alice, Eastern Cape
15/11/2014
Martin Mandalu
Alice, Eastern Cape
15/11/2014