Picha kwa hisani ya mtandao |
Ukosefu wa ajira za kutosha kwa vijana ndo hasa tatizo kuu linaloipasua kichwa serikali ya Tanzania. Hakuna ajira za kutosha kuwapatia fursa vijana wote wanaomaliza vyuo hapa nchini. Hivi karibuni tumesikia idadi ya wahitimu toka vyuo mbalimbali; kati yao wapo walio na ajira na wasio na ajira; kundi la pili likiwa kubwa zaidi. Wahitimu hao kwa baadhi ya vyuo ilikuwa kama ifuatavyo: Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, SUA, walihitimu zaidi ya 1000, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Mwanza, zaidi ya wahitimu 2000, Chuo Kikuu cha Dodoma wahitimu lukuki, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wahitimu lukuki pia. na kadhalika. Utaona ya kwamba kila uchao Vyuo vingi zaidi vinazidi kuongeza idadi ya wahitimu na hili ni jambo jema.
Kwa upande mmoja hili ni suala jema sana kwa nchi yetu, kwamba tunapata wasomi wengi zaidi. Lakini jambo hili halifariji sana pale unapoona kwamba wasomi wote ama wengi kati yao wanasubiri tu kuajiriwa. Hapa ndipo penye changamoto kubwa kwa mitaala ya elimu tunayoitumia toka shule zetu za msingi hadi sekondari. Wengi wa vijana wetu kulingana na mitaala tunayotumia ni tegemezi mno kiuchumi, kimsingi elimu wanayoipata haiwakwamui kiuchumi; pamoja na kumaliza kidato cha sita kijana wa kitanzania bado anaomba pesa kwa wazazi ama walezi kwaajili ya matumizi yake ya kawaida kama kununua nguo n.k; hii ni aibu. Mfumo wa elimu inafaa uweze kumfunza kijana kujitegemea, kuweza kuzalisha mali kwa kiwango fulani hata kama ni dhaifu lakini mtaala huo umsaidie kuwa na uthubutu; kijana awe na moyo wa kujaribu kufanya shughuli fulani halali kwa lengo la kuzalisha mali hata kama ni kidogo tu.
STEMMUCO/SAUT MTWARA |
Vijana wengi wa kitanzania wanafanya shughuli za umachinga; naambiwa machinga moja ya tafsiri zake ni ile ya “marching guys” jamaa watembeao (tafsiri si rasmi). Kwa mtazamo wangu hiki ni kitu muhimu kabisa vijana na ndugu wengine wanaofanya shughuli hizo ni kielelezo tosha kabisa cha ulazima wa kuwa na mitaala ya kufunza ujasiriamali (ujasiri wa kutafuta mali kihalali – tafsiri yangu mwenyewe). Ujuzi wa ujasiriamali na hamu ya kufanya majaribio katika masomo uguse aina zote za masomo yaani ya sayansi, sanaa na kadhalika. Kwa kufanya hivyo utaona kwamba hata machinga wetu watafanya mambo kizalendo tofauti na ilivyo hivi sasa.
Bidhaa za Wajasiriamali - twahitaji kuongeza tu ubora katika bidhaa zetu na mambo yatakuwa safi. Picha kwa hisani ya blogu la marchingguys |
Wengi wa machinga wa Tanzania kwa hakika ni vibarua wa nchi ya Uchina na nchi nyingi zilizoendelea. Wafanyabiashara wengi wanafanya biashara ya bidhaa zinazotoka nje ya Tanzania. Mfumo wetu wa uchumi, kwa kujua ama kwa kutokujua, umetufanya kuwa soko zuri sana la bidhaa za watu wengine. Fikiri kuhusu vitu ulivyonunua juma hili, bidhaa kumi; pengine sita hadi saba zimetoka nje ya Tanzania, japokuwa zinauzwa na wamachinga wetu ambao kimsingi ni vibarua wa uchina, Afrika Kusini n.k. Serikali ina nia njema sana ya kuwasaidia vijana, ndio maana ikaamua kujenga Machinga Complex pale Ilala. Nimesikia kuna mpango wa kujenga Machinga Complex kadhaa katika mikoa mingine kwa lengo lilelile la kuwakwamua vijana na kina mama. Ukiachia mbali kuhusu ufanisi wa jengo hilo, angalia bidhaa zinazouzwa ndani ya jengo hilo, asilimia kubwa zinatoka Jamhuri ya watu wa Uchina, mita chache toka pale Machinga Complex unakutana na iliyogeuzwa kuwa Dubai ya Tanzania Kariakoo, chunguza bidhaa zinazotoka, Dar es Salaam, Tanga, Iringa, Mwanza, Mbeya, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Mtwara n.k; ni chache mno. Hii ni changamoto kubwa kwa nchi yetu; hizi “Machinga Complexes” zinazowalenga vijana wetu inatakiwa ziuze bidhaa zitokazo Kigoma, Iringa, Ruvuma, Manyara, Mwanza, Shinyanga, Rukwa, Njombe n.k - bidhaa za Tanzania. Tazama hata sekta zingine; usafirishaji: foleni za motokaa kwenye majiji hapa nchini; Dar es Salaam, Mwanza na kwingineko pamoja na magari mengi vile, sina hakika kama kuna moja lililotengenezwa pale Kibaha. Tazama baadhi ya miji yetu ilivyojaa na kuwa jaa la pikipiki, bajaji, baiskeli, hakuna zinazotoka Tanzania, lakini wamachinga na wajasiriamali ni wengi kupindukia, huoni kuwa sisi ni wamachinga wa wachina tu!
No comments:
Post a Comment