Thursday, November 3, 2011

KUMBE KWELI SISI SHAMBA LA BIBI...

Picha kwa hisani ya google
Moja ya makala za HabariLeo katika chapisho lake la leo, imetoa habari inayotufanya nchi yetu kuonekana kama shamba la bibi lisilo na mmiliki...

Bibi ni mama mzazi wa baba ama mama; ni mtu muhimu kwani, huyu pamoja na mumewe ama mwanaume flani ambaye tutamuita babu, ameshiriki moja kwa moja kuwaleta duniani wazazi wetu. Mtu huyu ki-umri amekula chumvi nyingi, na kitamaduni sehemu nyingi barani ni mahiri katika mambo mengi. Ujuzi na busara ya mambo ipo katika uzoefu wa siku nyingi.

Bibi ndiye aliyewalea baba na mama (kila mmoja na mzazi wake - wote waitwa bibi ); hivi basi kwa jinsi wazazi wetu walivyo na nidhamu na utaratibu wa maisha, sehemu flani wamevipata toka kwa bibi. Ni yeye hasa ndio aliyewalea na kupata watoto wenye maadili mema na staha kama tuwajuavyo wazazi wetu. Ni kweli kuwa hupata ujuzi mwingine kwenye mazingira waliokulia, mafunzo sehemu mbalimbali lakini nafasi ya bibi kwa maana ya mzazi na mlezi ni kubwa hasa. Hata hivyo kuna jambo jingine ambalo hushangaza sana toka kwa bibi.

Kina bibi wengi wanaelezewa kama watu wenye kuwadekeza kupindukia watoto wa watoto wao; wajukuu. Kiasi cha kuwadekeza huko, huwashangaza watoto wao yaani baba na mama zetu, ambao mara nyingine hulazimika hutoa simulizi za namna ambavyo bibi alivyokuwa mkali enzi za malezi yake kwao. Kuna sababu kadhaa zinazoeleza kwanini bibi anakuwa mpole na rafiki mno kwa wajukuu zake. Moja ya sababu hizo ni uzee, uchovu na upweke wa utu uzima. Bibi anawahitaji watoto wa watoto wake ambao kwake ni marafiki; ili kuwapata mara nyingi huweza kutumia rasilimali alizonazo kuwaweka kwenye himaya yake. Ni kupitia mwanya huo basi mali za bibi huweza kutumika vibaya; kuharibiwa, kuhujumiwa, kila mmoja akachukua anachotaka na tena kwa nafasi yake. Katika hili bibi hajali mali yake inaharibiwa kiasi gani, muhimu kwake ni kujenga mahusiano na wajukuu wake wakiharibu ama wasiharibu hilo si muhimu kwake muhimu ni kwamba uhusiano wa kirafiki na wajukuu unakuwa bora zaidi na zaidi. Ni kutokana na masuala hayo ndo analojia ya shamba la bibi ikazuka.

Habari Leo hivi leo wametoa taarifa yenye kufanana na analojia ya shamba la bibi. Hapa nchini, katikati ya kitovu cha uchumi wa nchi, Dar es Salaam kumekuwa na shule ikiendeshwa kinyume na sheria kwa miaka kumi na miwili. Hii inaweza kuwa kipande cha pande kubwa la “jabari” la barafu baharini. Si ajabu kuna mengi ambayo hayajagunduliwa na tena yenye madhara makubwa kwa taifa.  Nchi ina mali asili nyingi tena za kila namna; je ni namna gani rasilimali hizo zinaendeshwa katika namna inayowanufaisha wananchi walio wengi na taifa kwa ujumla wake.

Tanzania ina mbuga lukuki za wanyama pori, je shughuli za kiuchumi za wanyama pori zinafanyika kwa jinsi inayotakikana? Je, taifa linapata pato stahiki? Tanzania ina bahari, maziwa, mito na mabonde yenye uwezo wa kunufaisha taifa kwa namna anuwai; je watu waliokabidhiwa madaraka kuendesha vyanzo hivyo vya mapato wanaitendea haki jamii na taifa kwa ujumla? Je, shughuli hizo zinaendeshwa katika namna endelevu? Ili kwamba wajukukuu wa wajukuu wetu wakute mali hizo ama faida zake na wao pia wamudu kuendesha maisha yao kwa furaha? Tunaweza kuorodhesha utajiri na zawadi nyingi zilizopo nchini  hata hivyo si nia yangu kufanya hivyo lengo ni kukumbushana juu ya taifa letu na mustakabali wake.

Kuhitimisha tunasema kuwa kila mmoja wetu awajibike kizalendo ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa letu la Tanzania, na kuboresha maisha ya jamii ya wanadamu wanaoishi sasa na wale watakao kuja baadaye kwa taratibu na sheria zinazokubalika.

No comments:

Post a Comment