Picha hii kwahisani ya blogu la mjengwa inaonyesha wanachi wakijaribu kuokoa mali zao toka kwenye nyumba zilizojaa maji. |
Kwa siku ya tatu mfululizo mvua zimeendelea kunyesha jijini Dar es Salaam na kusababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na maisha kupotea.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania wamesema kuwa mvua hizi zimezidi vipimo vyote vilivyorekodiwa toka mwaka 1954. Utaona kuwa ni mvua kubwa hasa.
Hii ni shida kubwa kwa jiji la Dar es Salaam ambalo sehemu kubwa halijapangiliwa vizuri kuwa makao ya kuishi binadamu. Kwa kuwa tumekumbwa na baa hili, tunawapa pole sana ndugu zetu wanaopitia hali hii nguvu ambayo haijawahi kutokea ndani ya Tanganyika na kisha Tanzania huru. Pole sana kwa msiba huu mkubwa; kwa hakika ni janga la taifa.
Pengine tatizo hili litupatie funzo wananchi tunaojenga maeneo ambayo si rasmi. Maeneo ya mabondeni siku zote wananchi tumekuwa tukiambiwa tusijenge lakini hatujali maelekezo rasmi na ya kitaalamu. Tatizo kama hili likitokea basi tunalazimika kuwasaidia ndugu hawa kwa kuwa ni binadamu wenzetu na hatuwezi kuwaacha katika matatizo. Hata hivyo sasa ni lazima kufuata taratibu rasmi ili kuweka mambo katika mstari mnyofu.
Mafuriko ya mara hii yamegusa hata maeneo rasmi, hii inaonyesha shida kubwa ya miundo mbinu mibovu ya jiji kuu hilo la kibiasahara hapa Tanzania. Ni lazima sasa kwa wadau wa miundo mbinu, mipango miji na wengine wote wanaohusika kwa karibu kuhakikisha kuwa mifumo muhimu na ya msingi kama vile maji taka, iwekwe vyema zaidi; tusisubiri tena kutokea kwa maafa kama haya tena.