Huko Tanzania, Oktoba 14 ya kila mwaka imetangazwa kuwa siku mahususi ya kumkumbuka na kumuenzi Julius Kambarage Nyerere, maarufu zaidi, Mwalimu Nyerere, ni siku aliyofariki huko Uingereza mwaka 1999. Rais wa kwanza wa nchi hiyo, MwanaAfrika na mjengadunia halisi; mpigania uhuru wa nchi nyingi barani humo, mwanafalsafa, mwandishi, mzalendo, mcha Mungu na binadamu mwadilifu.
Mwalimu ni mmoja kati ya viongozi wachache wa kiafrika aliyekuwa kwenye mamlaka kwa muda mrefu. Alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika mara tu baada ya kupata uhuru 1961 (1962 -1985) bila kujilimbikizia mali kama wafanyavyo viongozi wengi barani humo, mwalimu hakuwa mbinafsi. Alijitahidi kuishi vyema na kufuata misingi ya fikra za ujamaa na kujitegemea alizoziasisi.
Mwalimu pamoja na wenzake aliasisi Azimio la Arusha ambalo lilitoa maelekezo ya kuliongoza taifa ikiwa ni pamoja na maadili ya viongozi. Hii ilisaidia kuongoza nchi kwa uadilifu na ubadhilifu ulidhibitiwa kwa umakini, “Awamu ya kwanza rushwa ilikuwepo, lakini mtoa na mpokea rushwa wote walitiwa msukosuko mkubwa,… aliyebainika kupokea rushwa alicharazwa viboko 24, kumi na viwili kabla ya kwenda gerezani na kumi na viwili akimaliza kifungo chake ili akamwonyeshe mke wake…”
Julius Nyerere alikuwa na fikra binafsi ambazo aliziasisi, moja ya fikra hizo ni ile ya Ujamaa na kujitegemea. Katika nadharia hii Mwalimu alilenga kujenga taifa lenye uwezo wa kujipatia mahitaji yake lenyewe bila kutegemea sana mataifa ya ng’ambo. Mwalimu alijaribu kusimamia nadharia hiyo kwa mfano hata kama haikufanikiwa kama ambavyo angependa.
Zaidi Mwalimu aliwaunganisha watanzania wenye makabila zaidi ya miamoja na ishirini; wakati Tanganyika ikipata uhuru, kulikuwa na vijitaifa vingi, hivyo kazi aliyoifanya Mwalimu na viongozi wenzake ilikuwa ni kuunganisha mataifa hayo madogo madogo kuwa taifa moja kubwa. Kazi hiyo nzuri ilisaidia kuliepusha taifa hili la Tanganyika, na kisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26. 04. 1964, Tanzania, toka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambazo zimesambaa kote barani Afrika.
J.K Nyerere aliasisi mbio za Mwenge kwa tukio lenye hisia, kumbukumbu, na ujumbe mzuri hasa. Mwenge huo wa uhuru ulisimikwa kileleni mwa mlima mrefu kuliko yote barani Afrika; Kilimanjaro. Ni kapteni Alex Nyirenda wa jeshi la wananchi wa Tanganyika ndiye aliyefanya kazi hiyo nzuri. Akihutubia mjumuiko wa Umoja wa mataifa Mwalimu Nyerere alisema sisi tumeamua kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale walipokata tama, heshima palipojaa dharau (si maneno halisi)…………Ni dhahiri kuwa makala hii ni fupi mno kumuelezea mmoja wa waasisi wa taifa tukufu la Tanzania. Hata hivyo jambo la msingi ni je, tunamuenzi kwa kiasi gani Mwalimu Julius Nyerere?
Miaka kadhaa baada ya kifo cha Mwalimu, Tanzania inaendelea kumuenzi mzee huyu aliyefanya mambo mengi makubwa kwa taifa hili la Afrika Mashariki, lenye utajiri mkubwa japokuwa utajiri wake hauwafikii wote kwa usawa. Taifa linaendelea kumuenzi sana Mwalimu kwa sifa na sherehe zenye mbwembwe nyingi kote nchini. Lakini hatumuenzi Mwalimu kwa mambo ambayo yeye mwenyewe aliyataja kama muhimu kufikia maendeleo ya kweli ya watu. Kwani lengo kuu la kuongoza nchi ni kuleta maendeleo kwa wananchi; mwalimu alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne;
1. Watu,
2. Ardhi,
3. Siasa safi na
4. Uongozi bora
Ili nchi zetu ziweze kuendelea tunawahitaji watu wenye elimu nzuri, afya njema, chakula cha kutosha na mahitaji yao muhimu ya kila siku ili kushiriki katika ujenzi wa taifa lao, jamii ya wanadamu na dunia kwa ujumla wake. Lakini hivi leo watu wengi wa nchi hiyo bado hawana huduma za lazima kufikia wanapotaka kufika.
Ardhi, ni chanzo cha vyakula vingi anavyotumia binadamu na ni sehemu ambapo shughuli za kijamii na kimaendeleo za binadamu hufanyikia. Hii leo hiyo yenye utajiri, rutuba na mengine muhimu wanapatiwa wananchi wachache wenye pesa nyingi na wageni wenye mapesa na ushawishi mkubwa.
Siasa safi na uongozi bora ni tunu muhimu na za lazima kwa maendeleo ya watu…tunu hizo zimepiga hatua kubwa kwa malengo nia ile ile ya kuleta maendeleo kwa watanzania. Hata hivyo bado kuna mapungufu katika nyanja hiyo ya siasa safi na uongozi bora; kwa hivi kuna haja ya kuendelea kufanya marekebisho kwenye suala hili la uongozi. Hivi leo huko Tanzania, siasa inaonekana kama ni ajira yenye kuleta kipato kikubwa kwa haraka, matokeo yake watu wengi wenye kutaka utajiri wa haraka haraka, ikiwa ni wasomi, wafanyabiashara, wakulima hukimbilia siasa hata kama hawana wito huo. Viongozi wengi hivi leo hawana maadili sahihi ya uongozi, wameingia siasa kwa malengo mbalimbali; wengine wameingia kulinda biashara zao, wengine kujiongezea heshima tu na kulinda malengo yao binafsi. Azimio la Arusha lilitoa mwongozo namna gani kiongozi aongoze watu wake. Siasa safi na uongozi bora ni muhimu mno kwa maendeleo ya kweli ya WATANZANIA WOTE! Hivyo lazima kuwe na namna flani ya Azimio la Kujenga maadili ya viongozi nchini!
Picha kwa hisani ya tovuti ya nyerere.info
Picha kwa hisani ya tovuti ya nyerere.info