Monday, September 12, 2011

Alaa kumbe ni NEWALA !














Hapa nikijiandaa kuanza safari asubuhi na mapema- mjini Newala! Picha na Eric Wamalwa

Nipo wilayani Newala. Hii ndo wilaya ya kwanza kuandikishwa hapa Tanzania, ni moja ya wilaya tano za mkoa wa Mtwara. Wilaya hii, kama jinsi ilivyo kwa maeneo mengine, ina mahitaji ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kuna makundi yote ya lazima katika jamii; watu wazima, vijana, na watoto.

Kijamii; maji ni shida (jamii imejenga utamaduni wa kuvuna maji ya mvua: karibu kila familia ina mikingio maji kwaajili hiyo – huu ni utamaduni wa kuigwa hasa na sehemu zenye mvua za kutosha. Maji hayo ya akiba yaweza kuwa na matumizi kedekede. Mfano kumwagilia bustani za mboga mboga, kuanzisha mabwawa ya samaki n.k )

Elimu: wilaya ina shule kadha wa kadha; karibu kila kata ina shule yake. Hili ni moja ya mambo mazuri ya serikali iliyopo madarakani. Ni vyema kuwa na shule za kuweza kuandikisha wanafunzi wengi iwezekanavyo. Vijana wengi wakiandikishwa shule za sekondari ndo hasa mwanzo mzuri na wa uhakika wa kupiga vita umasikini kwa vitendo. Hata hivyo mtaala wa elimu uzingatie mfumo wenye vitendo zaidi kuliko nadharia kama ilivyo hivi sasa. Vijana wetu wengi wakimalima masomo yao, kwa mfumo tulio nao hivi sasa, hulazimika kusubiri ajira. Mfumo unaofaa ni ule wa kumuandaa kijana ili aweze kujiajiri; hilo hasa ndo liwe lengo la elimu yetu. Tukirejea mada yetu; shule nyingi huko Newala zina watenda kazi wachache sana.

Shule kadhaa zina walimu wawili, watano, sita, nyingi zina idadi isiyozidi walimu kumi. Hii ni changamoto kuu na kubwa mno katika sekta ya elimu. Wanafunzi wanapokuwa na walimu wa kutosha ndo inawarahisishia kujifunza kwa ufanisi zaidi. Kwa walimu wakiwa na wanafunzi kiasi, kwao inakuwa ni vyema zaidi katika utendaji kazi wao.

Ukosefu nyumba za walimu; shule nyingi za kata zipo vijijini hasa, ni sawa kwani huko ndiko wanapoishi wananchi na watanzania wengi zaidi. na vijiji vyetu vingi havina huduma kwa wageni hususani nyumba za kulala wageni. Ukosefu nyumba za kulala wageni vijijini unakwamisha hata wakaguzi na wataalamu wa kada zingine kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. Shule nyingi hizi za kata ama hazina nyumba za kutosha kwa walimu ama hazina kabisa nyumba hizo. Ni kweli walimu waliopo katika shule hizo ni wachache pengine inajieleza sawa pia kutokuwa na nyumba kwa walimu. Kuwa na nyumba za ziada kwa walimu inaweza kuwa ni fursa ya kuwavutia walimu wageni, ambao wengi wafikapo kujitambulisha na kuona mazingira ya shule hugoma kurejea shuleni huko.

Kisiasa: Newala ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hivyo huko pia kuna mfumo wa vyama vingi vya kisiasa lakini wakazi wa huko wanaishi kwa amani na undugu. Hata hivyo hii ni tathmini yangu ya juma moja tu.

Kiuchumi: zao la korosho ni uti wa mgogo wa uchumi wa wilaya hiyo; wakazi wengi hujihusisha na kilimo cha zao hilo la msimu na lenye kuhitaji matunzo ya karibu hasa. Kwa wananchi wanaoweza kufuata vyema maelekezo ya wataalamu wa kilimo hujipatia mavuno na pesa nzuri kutokana na kilimo cha zao hilo. Hata hivyo mkulima siku zote huchukua tu bei inayopangwa sokoni na watu wengine; yeye hufanya kazi ngumu ya kutunza shamba na kufuatilia ukuazi wa korosho hadi kuwa tayari na kisha hapo watu wengine wenye “utu” zaidi ya mkulima hukaa meza na kupanga bei ya zao hilo kama ilivyo kwa mazao mengine ya wakulima wetu maskini hapa Tanzania na sehemu nyingi nyingine barani Afrika. Siku moja tufikie hatua ya kupanga bei ya mazao yetu wenye kwenye hilo soko la dunia; hii ni mantiki zaidi kwa kuwa wakulima wetu ndio wanafahamu haswa gharama za kilimo.

Ajira za vijana: Vijana kundi lenye nguvu na msukumo mkubwa wa maendeleo ya wakati uliopo na ujao katika jamii. Nikiongea na vijana kadhaa wa mjini Newala niligundua kuwa kuna idadi kubwa ya vijana wa kitanzania wanofanya shughuli za kiuchumi, hususan biashara nchini Msumbiji. Newala ni wilaya ya mpakani kabisa na Msumbiji. Upande wa kaskazini ya Msumbiji haujapiga hatua kubwa kimaendeleo na hivyo kutoa fursa nyingi kwa watafuta mali: hivyo vijana wetu hupitia huko na kufanya biashara za bidhaa anuwai. Vijana niliongea nao, wanijuza kuwa vijana hao wa kitanzania huko, hususani wale wenye bidii ya shughuli zao, ni wenye mafanikio makubwa.

Nyumba za kulala wageni chache: wilaya hii ina nyumba chache za kulala wageni. Upungufu huo hivyo unatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi kujiimarisha kiuchumi na hivyo kujiongezea pato na pia kuongeza pato la taifa kwa ujumla.Kuna changamoto lakini pia fursa anuwi za kujiimarisha kiuchumi, kujiondoa kwenye umasikini na kuchangia kwa pato jumla la taifa.



No comments:

Post a Comment