Wednesday, September 14, 2011

Uzembe ukipungua ajali pia zitapungua !

Google Image
                                          Inapakiwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=MpzE7flW9_A
Wakati tukiendelea na tafakari juu ya ajali ya meli kule Nungwi ni wasaa mwafaka kwa watanzania na wanadamu wote kwa ujumla na hasa wenye kutumia vyombo mbalimbali kusafirisha binadamu wennzao, iwe ni vya ardhini, majini ama angani, kuwa waangalifu zaidi. Ajali ya meli ya abiria LCT Spice Islanders, iliyokuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba, imesababisha vifo vya ndugu zetu wengi. Ni msiba mkubwa kuona watu wengi wenye afya njema na ambao ni  nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa Taifa, wakiaga dunia.Tunamwomba Mwenyezi Mungu kwa huruma yake awapokee ndugu hawa kwenye makazi ya kudumu, na wafiwa na wajeruhi wote wapate faraja na kupona haraka! Kutokana na tukio hili serikali na wananchi wote kwa ujumla wetu tunapenda kuona wamiliki vyombo vya kusafirishia abiria, mamlaka za kudhibiti vyombo vya usafiri na wasafiri wenyewe wakiongeza umakini...

Wamiliki wa vyombo vya kusafirishia abiria waongeze juhudi zaidi kuvikagua vyombo vyao. Wamiliki hao waende kwa wataalamu wa vyombo mara kwa mara kuvifanyia ukarabati wa lazima. Kufanya hivyo kutapunguza ajali nyingi zinazosababishwa na uzembe wa kutofanya marekebisho husika ya mara kwa mara.

Mamlaka zenye kusimamia taratibu na sheria za uendeshaji wa vyombo vya usafirishaji, mfano Sumatra, wawe wabunifu zaidi katika kudhibiti ajali ambazo zina nafasi ya kuepukika. Mathalani, wanaweza kubuni njia na kuhakikisha kuwa abiria wengi iwezekanavyo wanakuwa na nambari za maofisa udhibiti toka mamlaka kama hiyo zenye jukumu la kikatiba kulinda maisha ya wananchi.

Abiria kwa nafasi yetu tuna jukumu muhimu kupunguza ajali mbalimbali. Tujifunze kuuona ukweli kwa jinsi ulivyo; abiria wakijaa kwenye vyombo vya usafiri tukemee kitendo hicho kwa kauli moja. Mwendesha chombo cha usafiri akizidisha mwendo, pale inapowezekana, tukemee badala ya kumpongeza. Askari akikagua chombo, gari, tumjulishe kama kuna shida; tupunguze na tuache uzembe na uvivu wa akili- lazima tupige picha ya mbali zaidi. Sisi kama raia na wananchi tunawajibu mkubwa kwa taifa letu. Hivyo tukishindwa kuzuia ajali ama uovu ambao tunaweza kuuzuia tunafanya makosa. Mosi hatuutendei haki ubinadamu kwa binadamu ni kiumbe mwenye uwezo wa kufikiri na kuchanganua na kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali. Pili kama ambavyo tumesema tayari; tunaikosea nchi yetu ambayo tunawajibu wa kuiendeleza...

1 comment:

  1. Ni ukweli usiopinga kuwa asilimia kubwa ya ajali hutokea kwa sababu ya uzembe wa abiria, waendesha vyombo ama wasimamizi wa sheria za vyombo hivyo. kwa mfano utapanda gari linasimamishwa na wasimamizi wa sheria hizo lakini litasimama zaidi ya mita 5 mbele kisha kondakta anashuka na kuwasalimia jamaa kisha safari inaedelea; wala hakuna ukaguzi wowote unaofanywa ndani ya gari ili kuona abiria wamezidi kwa kiasi gani, nk. Niungane nawe kwamba kama kila mmoja atatimiza majukumu yake hatutapoteza nguvu kazi kubwa kama inavyofanyika sasa. Tanzania bila ajali inawezekana.

    ReplyDelete