Thursday, September 29, 2011

MWANAFUNZI BORA


                                          Imepakuliwa hapa :https://www.youtube.com/watch?v=Y1JhL9FTA8Y                
Hapo juu wanafunzi wa moja ya shule za msingi hapa Tanzania. Mwanzo kabisa wa safari ndefu ya miaka kadhaa... wana mahitaji mengi kufanikisha ndoto zao.

Mwanzoni mwa mwaka huu shirika binafsi la HakiElimu lilitoa shindano la kuandika sifa za mwanafunzi bora. Shindano lilimtaka mshiriki aandike insha ama achore picha juu ya mada hiyo. Hatimaye hivi leo mshindi amepatika; unaweza kusoma mada hiyo kwenye Habari Leo Hapa  chini ni moja ya insha zilizoshiriki shindano hilo:

Mada hii ni muhimu kwa kuwa ni mwanzo wa maendeleo ya nchi yoyote duniani. Mwanafunzi mwenye sifa bora hufanya vyema katika masomo yake na kupata ujuzi wa aina fulani wenye manufaa kwa nchi. Mwanafunzi mwenye sifa bora hufaulu vyema masomo yake na kufaulu kwake ni lulu kwa nchi kwani kupitia ujuzi na weledi wake katifa fani aliyonayo huchangia katika maendeleo ya taifa lake.

Mwanafunzi ni mtu anayetafuta elimu ama maarifa fulani . Kwa kawaida mtu huanza kupata elimu toka utotoni. Ni vyema ikawa hivyo kwa kuwa mtoto anapokuwa mdogo ana uwezo mkubwa kwa maana ya wepesi wa kujifunza na kuelewa mambo mengi mapya kwa urahisi zaidi. Wakati wa umri mdogo mtoto anahitaji uangalizi wa karibu kabisa wa mzazi/ mlezi wake. Uangalizi huo ni vyema ukaangalia pia suala kujifunza kwa mtoto. Hivyo kujifunza kwa mwanafunzi wakati angali na umri mdogo ina maana kuwa huwahusisha pamoja naye mwenyewe, mwalimu, mzazi/mlezi, na familia yote kwa ujumla wake. Pamoja na hayo yote kuna vigezo na mazingira ambayo ni muhimu kwa mwanafunzi kuweza kutafuta maarifa kwa usahihi zaidi.

Ili mwanafunzi aweze kufanya vyema katika masomo yake na hivyo kuweza kuchangia katika maendeleo ya taifa lake na ya jamii yote ya wanadamu kwa ujumla wake, mara baada ya kupata ujuzi, ni lazima awe na sifa kadhaa. Sifa za mwanafunzi bora ndio hasa mada ya insha hii. Mwanafunzi bora anatakiwa awe na aina mbili ya sifa. Awe na sifa za ndani na za nje; nitazielezea kwa unagaubaga hapa chini.

Sifa za ndani ni za kimaumbile, hizi ni zile ambazo binadamu anazaliwa nazo. Hafanyi chochote kuzipata ni zawadi ya uumbaji na ni sifa za lazima kabisa; nazo ni akili na utashi. Akili ni ule uwezo wa kupokea, kuzisoma na kuzitafsiri taarifa zote toka nje ya mwili wa binadamu. Utashi ni ule uwezo wa binadamu kuamua kufanya jambo moja ama jingine baada ya utashi huo kupewa na akili taarifa zote zihusianazo na jambo fulani kabla ya kulifanyia maamuzi. Akili inampatia mwanafunzi uwezo wa kujifunza mambo mapya na kuyatunza kama ujuzi; hivyo ni jukumu la mwanafunzi, kupitia utashi, kuamua kujifunza. Sifa hiyo inatufikisha kwenye utashi; kazi ya utashi ni kuamua kufanya hili ama lile kisha kupewa taarifa zote muhimu. Hivyo basi, kwa sifa hii, mwanafunzi ana hiari ya ama kujifunza ama kutojifunza.

Sifa za nje za mwanafunzi bora ni usikivu, udadisi, heshima na matumizi sahihi ya ujuzi alioupata. Kijana wa kike ama wa kiume ili aweze kujifunza vyema hana budi kuwa msikivu. Asikilize kwa makini maagizo ya mzazi/mlezi nyumbani, mafunzo ya mwalimu shuleni na ni vyema pia milango yake yote ya fahamu ikawa na usikivu ili maarifa mapya yapatikane. Picha ya mtu mwenye masikio makubwa inaweza kuwakilisha twasira ya mwanafunzi mwenye usikivu.

Udadisi; hali ya kutafuta jambo kwa kuulizauliza . Kwa hakika hii ni sifa muhimu kwa mwanafunzi bora. Pamoja na kufundishwa na mzazi/mlezi nyumbani na mwalimu darasani, mwanafunzi mwenyewe inamlazimu ajifunze kutafuta elimu, mambo mbalimbali juu ya mafunzo yake bila ya kuwa tegemezi kwa mwalimu tu. Mwanafunzi mdadisi anaweza kuomba na kujiunga uanachama katika maktaba mahalia kwa lengo la kusaka mambo mbalimbali kwa kina zaidi.

Heshima, thamani ya utu, adabu ; hii ni sifa nyingine muhimu kwa mwanafunzi bora. Sifa hii humfanya mwanafunzi awe mwenye mahusiano mazuri na wazazi /walezi na walimu wake. Mahusiano mazuri ni kigezo na kichocheo cha muhimu cha udadisi na kujifunza. Mwanafunzi mwenye mahusiano mema na mwalimu wake hana hofu kuuuliza ama kutoa maoni yake juu ya mada fulani darasani.

Matumizi sahihi ya ujuzi alioupata. Mwanafunzi bora, si yule mwenyekukariri kila afundishwacho na kwa kurudia aliyoweka kichwani hupata alama nzuri katika mitihani, bali ni yule mwenye uwezo wa kutafsiri nadharia na masomo yake kwenda kwenye vitendo halisi. Mfano, kwenye somo la Sayansi kimu, mwanafunzi anajifunza juu ya utunzaji wa vyakula; swala hilo anaweza kulifanya kuwa kitendo halisi kwa kuwashirikisha wazazi wake kama simulizi inayoweza kufanyiwa kazi na hivyo kuipatia familia mbinu ya kuhifadhi chakula.

Kuhitimisha insha hii; wazazi/walezi na walimu wao pia wana majukumu makubwa juu ya wanafunzi wao. Kubwa na muhimu zaidi ni kuwajengea mazingira ya kujifunza na kuwatia shime ili wawe na hamu ya kuzitumikisha sifa zote za ndani na za nje. Akili, utashi wa kujifunza, usikivu, udadisi, heshima na matumizi sahihi ya ujuzi mpya ni sifa za mwanafunzi bora. Sifa hizi huleta matokeo mazuri mno pale zinapopatiwa mazingira na fursa sahihi na hiyo huweza kudhihirisha uwezo wa mwanafunzi bora.

No comments:

Post a Comment