Saturday, August 20, 2011

Vijana Maji Moto

Picha kwa Hisani ya mtandao
Hivi karibuni tumeshuhudia harakati kubwa za vijana sehemu mbalimbali duniani. Harakati hizo zimekuwa na dhima na vyanzo tofauti tofauti. Harakati za vijana mashariki ya kati na Afrika kaskazini zilisababishwa na kukosa mahitaji yao muhimu hususani kukosa nafasi za kazi na kutokuwa na uhakika wa mustakabali wa maisha yao. Giza hilo kwa mustakabali wa maisha ya vijana ulisababishwa na ubinafsi wa viongozi wa nchi hizo. Kiongozi wa Tunisia, Ben Ali amekuwa madarakani kwa muda mrefu na amejikusanyia mali nyingi mno na hivyo kuharibu matumaini ya vijana na wananchi wake kwa ujumla. Hali kadhalika, Misri, Libya, Yemen na kwingineko mashariki ya kati.

Vijana wa Uingereza wao nao walisababisha fujo ama varangati (Kiswahili cha kizamani) lakini wao sababu ilikuwa tofauti. Makala ya mwandishi kutoka London Macha, inatoa sababu ambazo zinawapambanua vijana wa Uingereza na wale wa Mashariki ya kati. Wachambuzi wengine husema kuwa vijana wa dola hiyo kuu zamani, wanafundishwa tu/ ama zaidi juu ya haki zao, hawafahamu kuhusu wajibu wao kwa jamii. Hili ni tatizo kubwa. Vijana wanapokua ni vyema tukawajuza haki zao, lakini muhimu kabisa watambue pia namna ya kuwajibika kwa jamii zao. Hili ni jambo la kila mahali Tanzania na nchi nyingine zote duniani, na tena muhimu kwa wananchi na pia serikali kutoa mchango wo kwa maendeleo ya vijana.

Tanzania kuna asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) lukuki zinazojihusisha na masuala ya vijana. AZAKI hizo zimeanzishwa na wananchi kwa malengo lukuki, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia vijana. Hili ni jambo jema kwani vijana ni moja ya makundi yaliyo muhimu kwa maendeleo ya jamii ya wanadamu. Hata hivyo katika siku za nyuma kidogo kulizuka AZAKI nyingi ambazo hazikujali masilahi ya walengwa husika bali waanzilishi kujijaza mapesa.

Serikali yetu Tanzania, imepiga hatua kubwa hasa kwa kuwa na utashi muhimu wa kisiasa na kuazisha shule za sekondari kila kata. Bila ubishi hii ni hatua kubwa sana ya kuelekea maendeleo ya kweli. Elimu mwanzo wa ustaarabu wote duniani; elimu kwa upana wake si tu ile ya darasani. Hata hivyo changamoto kubwa kwa serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa ujumla wao ni kuziboresha shule hizo lukuki za kata. Ni muhimu kufanya hivyo kinyume na hapo tunapata taifa la watu walioelimika nusu nusu. Hii elimu nusu ni hatari sana, pengine afadhali asiyeipata kabisa; mwenye elimu nusu hatokubalika katika kundi la wajinga kabisa kwani ana maarifa kiasi na hivyo kuwa tofauti na wasiosoma kabisa, lakini hawezi changamana pia na walioiva vilivyo kielimu kwake itakuwa ni kujinyanyapaa – “kujichora” (maarufu kwa vijana) mbele ya wasomi. Ni hatari kama nusu wasomi hawa watakuwa wengi; watadai haki kwa njia zisizokubalika kwani elimu yao yawatuma hivyo.

Hivyo AZAKI zilenge kuwasaidia vijana wapate stahili yao. Wananchi wote kwa ujumla na serikali kwa maana ya dola tujipange kuziboresha shule hizi haraka iwezekanavyo kama inavyoelezewa kwenye MKUKUTA II ili kuepukana na nusu wasomi na matatizo mengi toka kwa vijana wetu siku zijazo.

No comments:

Post a Comment