Picha toka mtandaoni |
Picha kwa hisani ya google Wafaransa wana msemo wao, "L'habit ne fait pas le moine" unaotafsiriwa kwa kiingereza "Clothes don't make the man" ama kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, "si mavazi yanayofanya mtu kuwa mtu". |
Hapo kale tumesoma katika historia ya kuwa wazazi wetu wa kale walijisitiri tu sehemu zao za utupu na kuwa hiyo ilikuwa ni namna yao ya maisha na hakukuwa na shida yoyote. Unaweza pia kuona katika filamu ya "the gods must be crazy " Mavazi ni kwaajili ya binadamu na si vinginevyo.
Hivi karibuni jamii zetu zimekuwa na muingiliano na jamii zingine na zimepiga hatua kubwa katika nyanja anuwai ikiwa ni pamoja na kwenye suala la mavazi. Binadamu ameona ni vyema akajivika mavazi yenye heshima na yenye kumpendeza.
Picha hii kwa hisani ya blogu la haki za binadamu |
Lakini muingiliano huo haukuishia tu kwenye mambo mazuri ya kujifunza kumekuwa na mambo yasiyo ya kupendeza kwa jamii. Kuna aina ya mavazi ambayo humuacha kiumbe akiwa karibu nusu uchi, ni kweli kwamba si mavazi yanayomfanya mtu kuwa mtu, lakini ni vyema kukubaliana na kile jamii inachotaka. Jamii ya leo Tanzania inahitaji mavazi yenye kusitiri vyema maungo, basi natufanye hivyo.
Kutoka Dodoma Mwandishi wa Tanzania Daima anaandika zaidi
BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wamesema kuwa wanakerwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wanaovalia mavazi ambayo yanaonyesha maungo yao na hivyo kuleta aibu kwa jamii.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, walisema kuwa tabia za wasomi hao haziendani na jinsi jamii inavyowachukulia kwani badala ya wao kuwa kioo kwa jamii wamegeuka kuwa chukizo.
Mmoja wa wakazi hao, Twaha Kivale, alisema kuwa kwa sasa mavazi ambayo yanavaliwa na wanavyuo hususan wa kike katika mkoa wa Dodoma ni ya aibu na yanaleta picha mbaya kwa wadogo wao wa elimu ya chini kama vile shule za msingi na sekondari.
“Tunategemea kuwaona wasomi wakiwa na tabia njema lakini cha kushangaza wasomi hao wanavaa nguo mbaya ambazo zinaonyesha maumbile yao ya ndani, hii ni sawa na kutembea uchi bila aibu tena mchana.
Tunashindwa kutofautisha wasomi na makahaba kutokana na mambo ambayo yanafanyika, kama kweli wasomi ambao tunawategemea kuongoza nchi wanavaa hivi kinyume kabisa na maadili yetu kuna maana gani ya kuelimika,” alihoji Kivalle.
Naye, mchungaji Evance Lucas wa Kanisa la EAGT, Siloam Ipagala, akizungumzia suala hilo alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wanafunzi wa kike kuvaa nguo hizo ni mpango kamili wa shetani.
Alisema kuwa kwa sasa shetani anawatumia sana watu ambao wanaonekana kuwa wasomi na wasipoweza kujitambua ni wazi kuwa watajikuta wakishindwa kufikia malengo ambayo wameyakusidia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, katika hilo alisema kuwa hata yeye anakerwa na tabia hiyo ambayo kimsingi inadhalilisha utu wa mwanamke.
Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuwa mji wa Dodoma una vyuo vikuu vingi na kuonekana kama sehemu ya maendeleo lakini kwa sasa hali ni mbaya kwani zimekuwepo tabia ambazo zinatia aibu katika jamii.
Hata hivyo alisema ili kuondokana na tabia hiyo kunatakiwa kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na serikali ili kuhakikisha tabia ya namna hiyo inakomeshwa.
Naye mwanachuo mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye hakutaka kutaja jina lake, alipoulizwa alisema kuwa mavazi ni hiari ya mtu na kuongeza kuwa licha ya wananchi kulalamika bado wataona mambo mengi kwani kila mtu ana uhuru wa kuvaa atakavyo.
Kwa sasa katika mkoa wa Dodoma kuna vyuo vya elimu ya juu vya Udom, St.Johns, Chuo cha Mipango na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).