Tuesday, January 10, 2012

BASATA YAONYA MAPROMOTA WABABAISHAJI

Na Mwandishi wa BASATA
Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA, Vivian Nsao Shalua
   akizungumza na wadau wa Sanaa katika Jukwa la Sanaa linalofanyika
kila wiki makao makuu ya Baraza hilo. Kulia ni Afisa Habari wa
BASATA Aristide Kwizela.


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaonya wakuzaji sanaa nchini kuacha mara moja ubabaishaji wanapokuwa wanaendesha matukio na matamasha mbalimbali ya Sanaa.

Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa Baraza hilo, Vivian Nsao Shalua wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharifu Shamba.

Shalua alisema kuwa, Mapromota wamekuwa wakiwarubuni wasanii kwa kuwafanyisha kazi zisizo na mikataba huku wao wakinufaika na kuwaacha wasanii wakishindwa kujikwamua kimaisha.

“Utaratibu uliopo sasa kila mdau yeyote anapoandaa tamasha au tukio lolote linalohusisha wasanii lazima aje na mikataba na wasanii hao, aoneshe uwezo wake kifedha katika kuendesha tukio lakini pia awe na kamati inayoeleweka ya uendeshaji” alisisitiza Shalua.

Aidha, aliongeza kuwa, kumekuwa na ukiukwaji kanuni na taratibu za uendeshaji matukio hayo ambapo Baraza limekuwa likiwapa onyo na kuwafungia wahusika lakini akasisitiza kuwa, njia pekee ya kuepuka hali hii ni kwa mapromota kufuata taratibu zilizopo.

Akizungumzia kuhusu suala la mikataba, aliwataka Wasanii kuhakikisha hawashiriki tukio au onyesho bila kuwa na mkataba na waandaaji kwani hali hiyo inawafanya wadhulumiwe na kushindwa kudai haki zao kwa mujibu wa makubaliano.

“Ni lazima sasa wasanii wadai mikataba. Sisi tunawabana wakuzaji sanaa (mapromota) kuambatanisha mikataba yao kabla hatujawapa kibali lakini lazima na wasanii waoneshe wajibu wao kwa kudai mikataba na kutoshiriki maonyesho bila makubaliano ya maandishi” alionya Shalua.

Alisisitiza kuwa, Baraza litakuwa makini katika kufuatilia wadau wanaopewa vibali vya kuendesha matamasha na matukio mbalimbali ya Sanaa na mara taratibu na kanuni zitakapokiukwa halitasita kuchukua hatua za makusudi.

No comments:

Post a Comment