Wednesday, January 11, 2012

MAVAZI YA AIBU YALALAMIKIWA

Picha toka mtandaoni
imepakuliwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=wxBwsU9u6vw
Picha kwa hisani ya google
                                                                                                                                                          
Wafaransa wana msemo wao, "L'habit ne fait pas le moine" unaotafsiriwa kwa kiingereza "Clothes don't make the man" ama kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, "si mavazi yanayofanya mtu kuwa mtu".



Hapo kale tumesoma katika historia ya kuwa wazazi wetu wa kale walijisitiri tu sehemu zao za utupu na kuwa hiyo ilikuwa ni namna yao ya maisha na hakukuwa na shida yoyote. Unaweza pia kuona katika filamu ya "the gods must be crazy " Mavazi ni kwaajili ya binadamu na si vinginevyo.

Hivi karibuni jamii zetu zimekuwa na muingiliano na jamii zingine na zimepiga hatua kubwa katika nyanja anuwai ikiwa ni pamoja na kwenye suala la mavazi. Binadamu ameona ni vyema akajivika mavazi yenye heshima na yenye kumpendeza.






Picha hii kwa hisani ya
blogu la haki za binadamu
Lakini muingiliano huo haukuishia tu kwenye mambo mazuri ya kujifunza kumekuwa na mambo yasiyo ya kupendeza kwa jamii. Kuna aina ya mavazi ambayo humuacha kiumbe akiwa karibu nusu uchi, ni kweli kwamba si mavazi yanayomfanya mtu kuwa mtu, lakini ni vyema kukubaliana na kile jamii inachotaka. Jamii ya leo Tanzania inahitaji mavazi yenye kusitiri vyema maungo, basi natufanye hivyo.

Kutoka Dodoma Mwandishi wa Tanzania Daima anaandika zaidi

BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wamesema kuwa wanakerwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wanaovalia mavazi ambayo yanaonyesha maungo yao na hivyo kuleta aibu kwa jamii.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, walisema kuwa tabia za wasomi hao haziendani na jinsi jamii inavyowachukulia kwani badala ya wao kuwa kioo kwa jamii wamegeuka kuwa chukizo.

Mmoja wa wakazi hao, Twaha Kivale, alisema kuwa kwa sasa mavazi ambayo yanavaliwa na wanavyuo hususan wa kike katika mkoa wa Dodoma ni ya aibu na yanaleta picha mbaya kwa wadogo wao wa elimu ya chini kama vile shule za msingi na sekondari.

“Tunategemea kuwaona wasomi wakiwa na tabia njema lakini cha kushangaza wasomi hao wanavaa nguo mbaya ambazo zinaonyesha maumbile yao ya ndani, hii ni sawa na kutembea uchi bila aibu tena mchana.

Tunashindwa kutofautisha wasomi na makahaba kutokana na mambo ambayo yanafanyika, kama kweli wasomi ambao tunawategemea kuongoza nchi wanavaa hivi kinyume kabisa na maadili yetu kuna maana gani ya kuelimika,” alihoji Kivalle.

Naye, mchungaji Evance Lucas wa Kanisa la EAGT, Siloam Ipagala, akizungumzia suala hilo alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wanafunzi wa kike kuvaa nguo hizo ni mpango kamili wa shetani.

Alisema kuwa kwa sasa shetani anawatumia sana watu ambao wanaonekana kuwa wasomi na wasipoweza kujitambua ni wazi kuwa watajikuta wakishindwa kufikia malengo ambayo wameyakusidia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, katika hilo alisema kuwa hata yeye anakerwa na tabia hiyo ambayo kimsingi inadhalilisha utu wa mwanamke.

Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuwa mji wa Dodoma una vyuo vikuu vingi na kuonekana kama sehemu ya maendeleo lakini kwa sasa hali ni mbaya kwani zimekuwepo tabia ambazo zinatia aibu katika jamii.

Hata hivyo alisema ili kuondokana na tabia hiyo kunatakiwa kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na serikali ili kuhakikisha tabia ya namna hiyo inakomeshwa.

Naye mwanachuo mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye hakutaka kutaja jina lake, alipoulizwa alisema kuwa mavazi ni hiari ya mtu na kuongeza kuwa licha ya wananchi kulalamika bado wataona mambo mengi kwani kila mtu ana uhuru wa kuvaa atakavyo.

Kwa sasa katika mkoa wa Dodoma kuna vyuo vya elimu ya juu vya Udom, St.Johns, Chuo cha Mipango na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).










Tuesday, January 10, 2012

BASATA YAONYA MAPROMOTA WABABAISHAJI

Na Mwandishi wa BASATA
Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA, Vivian Nsao Shalua
   akizungumza na wadau wa Sanaa katika Jukwa la Sanaa linalofanyika
kila wiki makao makuu ya Baraza hilo. Kulia ni Afisa Habari wa
BASATA Aristide Kwizela.


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaonya wakuzaji sanaa nchini kuacha mara moja ubabaishaji wanapokuwa wanaendesha matukio na matamasha mbalimbali ya Sanaa.

Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa Baraza hilo, Vivian Nsao Shalua wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharifu Shamba.

Shalua alisema kuwa, Mapromota wamekuwa wakiwarubuni wasanii kwa kuwafanyisha kazi zisizo na mikataba huku wao wakinufaika na kuwaacha wasanii wakishindwa kujikwamua kimaisha.

“Utaratibu uliopo sasa kila mdau yeyote anapoandaa tamasha au tukio lolote linalohusisha wasanii lazima aje na mikataba na wasanii hao, aoneshe uwezo wake kifedha katika kuendesha tukio lakini pia awe na kamati inayoeleweka ya uendeshaji” alisisitiza Shalua.

Aidha, aliongeza kuwa, kumekuwa na ukiukwaji kanuni na taratibu za uendeshaji matukio hayo ambapo Baraza limekuwa likiwapa onyo na kuwafungia wahusika lakini akasisitiza kuwa, njia pekee ya kuepuka hali hii ni kwa mapromota kufuata taratibu zilizopo.

Akizungumzia kuhusu suala la mikataba, aliwataka Wasanii kuhakikisha hawashiriki tukio au onyesho bila kuwa na mkataba na waandaaji kwani hali hiyo inawafanya wadhulumiwe na kushindwa kudai haki zao kwa mujibu wa makubaliano.

“Ni lazima sasa wasanii wadai mikataba. Sisi tunawabana wakuzaji sanaa (mapromota) kuambatanisha mikataba yao kabla hatujawapa kibali lakini lazima na wasanii waoneshe wajibu wao kwa kudai mikataba na kutoshiriki maonyesho bila makubaliano ya maandishi” alionya Shalua.

Alisisitiza kuwa, Baraza litakuwa makini katika kufuatilia wadau wanaopewa vibali vya kuendesha matamasha na matukio mbalimbali ya Sanaa na mara taratibu na kanuni zitakapokiukwa halitasita kuchukua hatua za makusudi.

Wednesday, January 4, 2012

Masomo Zaidi...?

Elimu haina mwisho ndivyo usemavyo mmoja wa semi za wahenga wetu.
Kujiendeleza kielimu ni muhimu kabisa kwa wale wenye kupenda kufanya hivyo.

Mtandao wa Advance Africa lengo lao kuu ni kufanya hivyo; hebu sasa wale wenye moyo na nia ya kufanya hivyo wasome zaidi hapa. Bonyeza hapa

Mbinu za kazi tofauti malengo yaleyale - safi sana!


    

Sunday, January 1, 2012

MAISHA NI MALENGO

Leo ni mwanzo wa juma jipya, mwezi mpya, mwanzo wa miezi mipya kumi na mbili ama maarufu zaidi mwaka mpya.

Mwanzoni mwa mwaka ni kipindi kizuri kufanya tathmini ya kile tulichokuwa tukikifanya kama hatukufanya hivyo mwishoni mwa mwaka. Ama yaweza kuwa fursa ya kuweka malengo mapya ama kuyapitia yaliyotangulia kwaajili ya muda mpya unaoanza mbele yetu.

Kufanya tathmini ama kujiwekea malengo katika maisha ni suala la msingi mno kama tunataka kuishi katika namna inayoeleweka na yenye tija na mchango katika dunia yetu. Lengo la maisha kwa kila binadamu awe anafahamu ama la ni kuwa na furaha maishani. Aristotle, mwanafalsafa wa kale anasema hivyo pia; ili mtu awe na furaha basi hana budi kujiwekea malengo. Malengo huwekwa na watu wa kila kada.

Mwalimu shuleni hujiwekea malengo yake, mwanafunzi, mwanasiasa, mwanamichezo, mwanasanaa, mwanauchumi, msomi, mwanazuoni, mwanasheria, mkufunzi, mfanyabiashara, mkulima, mchungaji kanisani, shehe msikitini, imamu sinagogini, na kadhalika…watu wote makini wa kada zote hujiwekea malengo maishani. Kutokuwa na malengo maishani ni mithili ya muuza duka bila daftari, ambapo twajua mali bila daftari hupotea bila habari. Maisha bila malengo hupotea bila taarifa.

Kujiwekea malengo ni utamaduni ambao inafaa watu wote tuwe nao. Kwa kusema hivyo nafahamu fika kuwa kuna ndugu wasio na mazoea ya kufanya hivyo; watu hao mara nyingine hufananishwa na bendera fuata upepo hufuata chochote kitakachokuwa mbele yao. Bila ubishi si utaratibu mzuri wa maisha. Kwa wasio na utaratibu huo ni wakati sawia kuuanzisha.

Dini nyingi hutueleza kuwa hapa duniani ni sehemu tu ya mpito - twapita tu na kwamba makao yetu halisi yapo kwa muumba wetu. Hivyo wakati tukiandika malengo yetu ya maisha ni vyema tukamshirikisha huyo muumbaji kwa kuwa sisi hatujui siku wala saa ya kuyahama makazi ya hapa duniani, japokuwa hatutakiwi kuogopa kifo.

Unapoandaa malengo fanya hivi:

Kwa wanandoa, ama watarajiwa, wawashirikishe wenzi wao. Malengo haya si yako peke yako. Kwa hiyo nafsi ya kwanza ni Mwenyezi Mungu na pili ni mwenzi wako wa maisha; mkeo, mumeo ama mchumba wako. Muombe(ni) Mungu ili awaangazie kufanya malengo ya kweli.

Hatua ya pili ni kuwa mkweli na hali yako halisi; weka malengo ambayo yana uhalisia wa maisha yako. Mfano haina maana kwako mwanafunzi wa Tanzania kuwa na lengo la kuwa rais wa Pakstani miaka mitano ijayo. Weka malengo ambayo kwa kiasi fulani una nafasi ya kuyatekeleza. Mfano kusoma kozi ya Kifaransa kwa undani mara baada ya kumaliza masomo yako mwezi wa Juni.

Weka malengo yenye kukujenga na yatakayohitaji juhudi zako kuyatimiza.

Usiogope kuwa na malengo mengi bora tu ni muhimu katika makuzi na utu wako, mwisho wa muda wa kuyatimiza utakapowadia utakuwa na wasaa wa kujitathmini na kujua wapi ulihitaji ama utahitaji juhudi zaidi. Mara nyingine tukiwa na malengo mengi na yenye kudai juhudi zetu zaidi ndipo ambapo huwa na mafanikio zaidi maishani.

Usiwe mtu wa kujihurumia; kuona kuwa malengo haya ni mengi na magumu mno siwezi kuyatimiza. Usishindwe kujaribu, jaribu kutenda na ukishindwa wakati ukitenda ni tofauti kabisa na ukishindwa kujaribu kufanya chochote.

Jiamini na usijilaumu. Fanya utakachoweza kwa juhudi zako na mambo yakienda kombo, bila shaka utapata fursa nyingine ya kutenda tena!



Kila la heri na Mungu akubariki!

Mandalu
01/01/2012

Saturday, December 31, 2011

Masomo kadhaa yalifunzwa!

Moja ya sababu kubwa ya umaskini Afrika kumbe ni rushwa...








































Friday, December 30, 2011

Ubunifu ulionyeshwa vyema

Si mchezo wa karata tatu, hapa ni uwezekano wa mambo katika hisabati

















Unazifahamu baadhi ya ajira za watu duniani?














Unafahamu mtoto wa dada yako wamuita nani, na watoto wa baba mdogo, mama mdogo n.k?

















Wajua vilivyomo udongoni?

Baadhi ya Walimu waliohudumu mwezi huo

Mwalimu wa Jiografia akifanya kazi yake















Mwalimu mwingine wa Jiografia akielimisha juu ya Mazingira













Mwalimu akikazia jambo kwa maandishi


















Mwalimu akiweka msisitizo kwa wanafunzi

Wednesday, December 28, 2011

Walimu Bora Matumaini kwa Taifa


Mwalimu wa somo la jiografia akiwa kazini 2011




























Wahenga walisema, mtoto anapozaliwa ni ishara kuwa Mwenyezi Mungu bado anaipenda dunia. Msemo huu una ukweli pia katika sekta ya elimu. Unapokutana na walimu bora, unakuwa na hisia na pia uhakika na taifa la watu wenye fikra yakinifu, wataalamu wake lenyewe, maendeleo ya kweli na kadhalika.

Maendeleo ya kweli yataletwa kupitia matumizi mazuri na sahihi ya ubongo wa binadamu; njia mojawapo ya kuufanya ubongo huu ufanye kazi yake sawa sawa ni mafunzo. Mafunzo hayo yaweza kuwa nyumbani mtoto angali mdogo kabisa kabla ya kwenda shule tunazozifahamu. Kwa watu wengi mafunzo yanayotambulika rasmi huanzia shuleni, lakini kumbe mtoto huweza kufunzwa hata kabla ya kuanza kuhudhuria shule rasmi. Hapa hata hivyo najadili juu ya shule rasmi tunazozifahamu. 

Mwezi Novemba 2011, STELLA MARIS MTWARA UNIVERSITY COLLEGE (STEMMUCO)(Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT) kiliandaa mitihani maalumu kuwapima wanachuo ambao ni walimu wa baadaye.

Mitihani hiyo ilenge kupima mambo anuai; uwezo wa kujieleza kwa lugha ya kiingereza, uwezo wa kuwasilisha mada, kujiamini kwa mwalimu, uwezo wa kutafsiri somo katika mazingira ya usasa, na kadhalika.

Walimu wengi walitia fora sana katika ufundishaji; walijiamini, waliwasilisha mada vyema kabisa, walitumia vielelezo vya masomo na waliwashirikisha wanafunzi wao vyema. Hata hivyo wengine bado wanahitaji kuboresha zaidi kipengele cha tafsiri ya somo kwenda kwenye maisha halisi ya leo na ya usasa. Mwanafunzi atavutika kujifunza zaidi pale atakapogundua kuwa kwa kusoma mada fulani darasani anaweza akaitumia kucheza na rafikize ama akamweleza bibi yake kijijini akatambua na kuitumia mbinu husika. Mfano kwenye somo la utunzaji wa vyakula. Maeneo mengi ya kanda ya ziwa hulimwa kwa wingi viazi vitamu, huwa vingi na si rahisi kula vyote katika msimu mmoja. Wakulima wa ukanda huo, wamebuni njia ya kuvihifadhi viazi kwa njia mbili.

Njia ya kwanza ni kuvimenya viazi hivyo vingali vibichi na kisha kuvichanja vipande vidogo vidogo na kuvianika juani kwenye uchanja maalumu kwa kazi hiyo ama kwenye paa la nyumba. Vikikauka huwa vyeupe na huitwa michembe.

Njia ya pili; viazi vitamu huchemshwa na kisha humenywa maganda yake na kisha zoezi la kuvichanja kama vile vibichi hufuata. Vikikauka, kwa kuwa vilichemshwa huwa na rangi ya dhahabu, ni vitamu sana na hujulikana kwa jina la matobolwa. Huifadhiwa katika magunia ama ghala na huliwa hasa wakati wa msimu wa kilimo, huliwa kama sehemu ya kifungua kinywa lakini pia hata mlo wa jioni.

Tafsiri ya somo katika maisha ya sasa ama halisi inaleta hamu na maana zaidi ya kujifunza na hiyo itawavutia watoto wetu wajifunze zaidi.

Mbinu hizo zitumike zaidi kwenye masomo yote lakini hasa na muhimu kwenye hisabati, hili ni somo linalosumbua wanafunzi wengi nchini, na masomo mengine ya sayansi, biolojia, fizikia, na kemia.

Kwa kufanya hivyo tutakuwa na matumaini ya maendeleo ya kweli katika nchi yetu vinginezo tutaendelea kushuhudia wengine wakitupita kimaendeleo na sisi tukiendelea kuwa soko la bidhaa zao kila uchao.

Mandalu

Tuesday, December 27, 2011

Ndugu Simbakalia Mtumishi aliyetukuka

Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma
Picha kwa niaba ya blogu la bongo ndiyo home
Mkuu wetu wa mkoa wa Mtwara amepatiwa nishani ya Utumishi uliotukuka kwa kanisa na jamii. Hii ni habari njema kwa mkoa wa mtwar. Mchango wake huo ni ule alioutoa kwa taifa hususan kwa mkoa wa kigoma. Kwa Mtwara ni furaha kubwa kwa kuwa tumepata mkuu ambaye ana sifa za uchapaji kazi. Ndugu mkuu wa mkoa endelea na moyo huo ili utakapokamilisha shughuli zako nasi wanaMtwara tutakupatia nishani nyingine bila shaka. Kwa sasa hongera sana kwa mchango wako.










Nishani hiyo ilikabidhiwa kwa Simbakalia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa karibu miaka sita, na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma, Protas Rugambwa kwa niaba ya Papa katika misa ya Ibada ya Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa la Bikira Maria mshindaji mjini Kigoma.

Simbakalia alitiririkwa na machozi wakati akikabidhiwa nishani hiyo kutokana na kutoamini kile anachokiona hali iliyofanya kanisa kuzizima kwa hali hiyo katika tuzo hiyo ambayo ni ya kwanza kutolewa kwa muumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma tangu kuanzishwa kwake.

Sunday, December 25, 2011

YOSEFU NA VIJANA WA LEO


Yosefu ama Yusufu alikuwa baba mlishi wa mtoto Yesu. Ndugu huyu alikuwa na mchumba aliyejulikana kwa jina la Maria ama Mariamu; wote wawili walikuwa Wayahudi. Kabla ya kuishi pamoja kama mume na mke, Mariamu alionekana kuwa mjamzito. Kwa taratibu za kiyahudi, husasani za wakati ule, Yosefu alitakiwa kutoa taarifa kwa wahusika na binti huyo angeuwawa kwa kupigwa mawe. Yosefu lakini aliadhimia kumuacha kimya kimya yule binti. Maandiko yanatuambia kuwa Mwenyezi aliingilia kati na hatimaye Yosefu akamchukua mchumba wake.

Vijana wa kiume hapa Tanzania na duniani kote wanaweza kujifunza tabia hiyo ya Yosefu. Vijana wetu wa kiume wakijifunza tabia hiyo basi matatizo mengi yanayoisibu jamii yetu yanaweza kupungua ama kuisha kabisa.

Vijana hawawezi kukataa mimba wanazowapa mabinti na kisha kuwakana. Hii itasaidia kupunguza watoto wa mitaani. Miji yetu mingi mikubwa ina watoto wengi wa mitaani; watoto hawa kwa kiasi fulani ni matokeo ya kina kaka na kina baba kuwatelekeza wake na ama wachumba wao, wao pekee na watoto. Basi sherehe hizi za Krismasi tunaweza kuzitumia kuwakumbuka watoto wa mitaani na sisi kubadilisha tabia zetu kwa mfano wa Yosefu.

Wednesday, December 21, 2011

Mvua kubwa zaleta madhara Dsm

Picha hii kwahisani ya blogu la mjengwa inaonyesha wanachi
wakijaribu kuokoa mali zao toka kwenye nyumba zilizojaa maji.
Kwa siku ya tatu mfululizo mvua zimeendelea kunyesha jijini Dar es Salaam na kusababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na maisha kupotea.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania wamesema kuwa mvua hizi zimezidi vipimo vyote vilivyorekodiwa toka mwaka 1954. Utaona kuwa ni mvua kubwa hasa.






Hii ni shida kubwa kwa jiji la Dar es Salaam ambalo sehemu kubwa halijapangiliwa vizuri kuwa makao ya kuishi binadamu. Kwa kuwa tumekumbwa na baa hili, tunawapa pole sana ndugu zetu wanaopitia hali hii nguvu ambayo haijawahi kutokea ndani ya Tanganyika na kisha Tanzania huru. Pole sana kwa msiba huu mkubwa; kwa hakika ni janga la taifa.

Pengine tatizo hili litupatie funzo wananchi tunaojenga maeneo ambayo si rasmi. Maeneo ya mabondeni siku zote wananchi tumekuwa tukiambiwa tusijenge lakini hatujali maelekezo rasmi na ya kitaalamu. Tatizo kama hili likitokea basi tunalazimika kuwasaidia ndugu hawa kwa kuwa ni binadamu wenzetu na hatuwezi kuwaacha katika matatizo. Hata hivyo sasa ni lazima kufuata taratibu rasmi ili kuweka mambo katika mstari mnyofu.

Mafuriko ya mara hii yamegusa hata maeneo rasmi, hii inaonyesha shida kubwa ya miundo mbinu mibovu ya jiji kuu hilo la kibiasahara hapa Tanzania. Ni lazima sasa kwa wadau wa miundo mbinu, mipango miji na wengine wote wanaohusika kwa karibu kuhakikisha kuwa mifumo muhimu na ya msingi kama vile maji taka, iwekwe vyema zaidi; tusisubiri tena kutokea kwa maafa kama haya tena.

WANACHUO WAPEWA MBINU ZA KUFAULU...


Wanafunzi wanahudhuria vipindi na kuandika kumbukumbu zao
wenyewe wana nafasi kubwa ya kufanya vyema zaidi katika
mitihani yao kuliko wale wenyekuandika nukuu za rafiki zao



 Wanachuo wakifuatilia mhadhara maalumu chuoni kwao. Kumbe mafanikio katika majaribio na mitihani huanza toka mwanzoni kabisa. Jinsi ambavyo mwanafunzi anasoma na kuandika kile anachofundishwa na kujisomea ni muhimu kwa kuwa hiyo humsaidia pia katika utunzaji wa kumbukumbu akili. Hivyo wale waliozoea kuchukua maandishi ya wenzao wapunguze tabia hiyo na badala yake wahudhuria vipindi wawo wenyewe. Kwa habari zaidi soma hapa.

1. Start Studying in School

Studying for tests and quizzes actually starts way before you even know you'll have a test.Good study techniques begin in the classroom as you take notes. Note-taking is a way of remembering what you were taught or what you've read about.
Where's your favorite place to study?
Some keys to note-taking are to write down facts that a teacher mentions or writes on the board during class.If you miss something, ask your teacher to go over the facts with you after class.
Keep your notes organized by subject and making sure they're easy to read and review. This may mean that you need to recopy some notes at home or during a free period while the class is still fresh in your mind.
Unfortunately, most schools don't have classes that teach you how to take notes. When it comes to taking good notes, it can take some experimenting to figure out what works, so don't give up.
Original link:

Saturday, December 17, 2011

Unamfahamu mwanaAfrika huyu?



Thomas Sankara( Desemba 21, 1949 – Oktoba 15, 1987), Che Guevara wa Burkina Faso
Mwana Afrika halisi, mtu mnyofu, mwadilifu, mkweli na mzalendo wa kweli!
Mwanamapinzuzi na rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Isidore Sankara ( 1949 -1987) wiki moja kabla ya kifo chake alisema: “ Wakati wanamapinduzi kama watu binafsi wanaweza kuuwawa, kamwe huwezi kuziua fikra zao za kimapinduzi.”

Thomas Sankara ndiye mtu aliyebadilisha jina la nchi yake; hapo kabla ilijulikana kwa jina la Upper Volta; yeye alibadilisha na kuiita nchi yake Burkina Faso yaani NCHI YA WATU WAADILIFU – Pays des hommes integre” ama land of the upright people” hujulikana pia kama Che Guevara wa Burkina Faso


Kaburi la kawaida kabisa la MwanaAfrika huyo
likiwa limezungukwa na makaburi ya walinzi wake












 Thomas Noel Isidore Sankara alizaliwa Desemba 21, 1949. Alikuwa rais Agost 4, 1983 na huyu ndio hasa kiongozi wa kwanza aliyetambulika kwa kuwa na upendo dhahiri wa nchi yake na ambaye alihimiza kuindeleza nchi yake, kukuza na kuzitambulisha tunu za nchi hiyo na kufanya zifahamike kwa wananchi na kwa mataifa ya nje.

Sankara alipitia mafunzo mbalimbali ya kijeshi. Mwaka 1970 alikwenda Madagaska, 1978 alikwenda Moroko. Alishiriki katika vita ya Mali na Burkina Faso mwaka 1974.


Katika siasa alikuwa na mafanikio; 1981 alikuwa waziri wa habari, waziri mkuu mwaka 1982. Na kati ya 1981 na 82 alifungwa kwa tuhuma za rushwa. Na mwisho katika wigo wa kisiasa aliongoza Chama Kidemokrasia na cha Kimapinduzi hadi alipofanya mapinduzi maarufu ya Agosti 4

Kitu muhimu sana ambacho Sankara alipenda kufanya baada ya kuwa rais ni kuwataka watu wote wawe waadilifu. Alitaka serikali yake ifanye hivyo ili kutoa mfano mzuri kwa vijana na vizazi. Rushwa ilipigwa vita kwa nguvu zote. Mpango huo ulianza rasmi pale alipobadalisha jina la nchi yake. Zaidi alibadilisha pia motto, nembo ya taifa na kuwa " Nchi yetu ama kifo, Tutashinda" wananchi walihimizwa kuwa wazalendo kwa kuungana, kuilinda na kuipenda nchi yao. 
Sankara alikuwa karibu na wananchi alipiga gitaa, alicheza mpira, aliendesha baisikeli na kufanya mambo mengi ambayo yalimuweka karibu na wananchi. Kuhusu uchumi aliwapatia wananchi ardhi wapate maeneo ya kulima, aliondoa mambo kadhaa ya kuwapendelea viongozi; alifanya viongozi wawe kweli watumishi wa wananchi.
















Alifanya mambo mengi sana mazuri; hata hivyo kama wasemavyo waswahili, kizuri hakidumu. Thomas Sankara aliuwawa miaka minne baadaye. Ndani ya miaka minne aliweza kuleta mabadiliko makubwa kuliko ya miongo kadhaa. Vijana wengi barani Afrika walilia hadharani kwa kuwa waliona kuwa ile ndoto ya kuwa na mabadiliko barani Afrika iliondolewa. Wazo muhimu hapa ni je, wewe kijana unachangia nini kuleta maendeleo ya kweli kwa familia yako, jamii yako na kwa upana zaidi kwa nchi yako? Unaweza kusoma zaidi hapa











Sunday, December 11, 2011

Elimu ya kweli ni vitendo!



Elimu ikitafsiriwa kwenye matendo ndo haswa Elimu!























Chuo kikuu cha Makerere, kikishirikiana na vyuo vikuu vingine kimeshiriki katika mradi wa kutengeneza gari linalotumia nguvu ya umeme. Magari ya aina hii yatasaidia katika utunzaji wa mazingira kwani hayatoi moshi na hivyo kutunza mazingira. Changamoto ni kwa vyuo vikuu vingine hususani vile vikongwe, Afrika Mashariki vinafanya nini?

Kupata maelezo vizuri juu ya mradi huu soma hapa



Sehemu tofauti za gari hilo!


Siku za Usoni Chuo Kikuu cha Makerere kikishirikiana na vyuo vikuu vingine kitatengeneza gari la aina hii. Je, huu ni ukombozi wa kweli kwa bara letu la Afrika? 

Saturday, December 10, 2011

Sala / Swala kabla na baada ya kazi


File:Flag of Tanzania.svgTanzania ni nchi isiyo na dini ila watanzania wana imani na dini zao. Tanzania, ni nchi na si binadamu, mtanzania ni binadamu na wala si nchi. Hivyo watanzania hawa kwa kuwa wanamwamini Mungu basi katika mambo muhimu na rasmi yanayohusu nchi, watanzania hawa huyaanza kwa kumuomba na kumshukuru Mungu. Huu ni wito tosha kwetu sote pamoja na viongozi wetu kusali kabla na baada ya shughuli zetu.Changamoto mpya kwa maendeleo ya nchi yetu - Hofu ya Mungu na upendo kwa Jirani ni muhimu hasa!




WIMBO WA TAIFA WA TANZANIA


Mungu ibariki Afrika                                                   God bless Africa


Wabariki Viongozi wake                                             Bless its leaders
Hekima Umoja na Amani                                            Wisdom, unity and peace
Hizi ni ngao zetu                                                         These are our shields

Afrika na watu wake.                                                  Africa and its people

Kiitikio:                                                              Chorus

Ibariki Afrika, Ibariki Afrika                                   Bless Africa, Bless Africa

Tubariki watoto wa Afrika.                                    Bless us, the children of Africa


Mungu ibariki Tanzania                                           God bless Tanzania
Dumisha uhuru na Umoja                                        Grant eternal freedom and unity
Wake kwa Waume na Watoto                                To its women, men and children
Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.                     God bless Tanzania and its people


Kiitikio:                                                               Chorus:
Ibariki Tanzania, Ibariki Tanzania                              Bless Tanzania, Bless Tanzania
Tubariki watoto wa Tanzania.                                   Bless us, the children of Tanzania












Friday, December 9, 2011

Uhuru wa Tanzania Bara na Maoni


Sehemu ya wadau kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru

















Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ama ya iliyokuwa Jamuhuri ya Tanganyika, mkoani Mtwara yalifanyika kwa mdahalo wa kitaaluma Katika Chuo Kikuu cha STEMMUCO.

Kulikuwa na mada kedekede zenye kuangalia hali halisi ya nchi hii toka ijipatie uhuru wake toka mikononi mwa walezi wa kiingereza miaka hamsini kamili hivi leo. Asilimia kubwa ya washiriki ni wale waliozaliwa kisha uhuru. Baadhi yao ni watu waliopata fursa za kuzunguka sehemu mbalimbali duniani. Wengine walikuwa ni watu wenye taaluma kubwa kwa maana ya ujuzi na vyeti. Hata hivyo walikuwepo pia washiriki wachache waliokuwa hai wakati Tanganyika ikijipatia uhuru wake.

Matokeo ya mjadala, hususani ya wasomi wengi, yalidhihirisha kuwa toka uhuru, ukitilia maanani rasilimali nyingi tulizonazo, nchi hii haijapiga hatua kabisa. Mengi yaliyofanyika ni hovyo mno na kwamba juhudi kubwa na za haraka zinahitajika sana ili tupate nafuu. Hivyo kauli mbiu ya “Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” haina ukweli kabisa labda kama ni kuthubutu kuihujumu nchi. Ilhali wazee wachache walioshiriki mjadala huo na kuongea, japo kwa muda mfupi, walisema bila kificho kuwa nchi imepiga hatua kubwa ingawa bado kuna haja ya kutenda zaidi.

Binafsi naungana sana na wazee na wengine wenye mtazamo huo kuwa; nchi yetu imefanya mambo mengi mazuri na kuna juhudi zinaendelezwa ili tufanye vyema mara dufu. Hata hivyo kutokana na utajiri wa kiasili ulio katika maliasili ya nchi yetu, basi kweli, utaona kwamba tunatakiwa kuwa mbali sana kimaendeleo. Shida yetu kubwa kila mmoja wetu ni ubinafsi; kila mmoja anataka kunufaika yeye na familia yake kwanza, na kisha hapo ndo aangalie uwezekano wa kuwakumbuka wengine, uwezekano. Tuache ubinafsi na tujifunze toka kwa waasisi wa nchi yetu kujitoa muhanga kwa maendeleo ya watu na taifa letu. Sina hakika kama Mwalimu Nyerere, Mzee Kawawa, Shujaa Moringe Sokoine waliacha pesa kwenye akaunti nje ya nchi.

Utawala bora uimarishwe; wenye makosa washitakiwe na sheria ifanye kazi yake kwa uwazi na uhuru. Tuliambiwa ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Mambo haya yote na tuyazingatiwe na hatimaye tutaweza kufika tunakopaswa kuwa kulingana na rasilimali tulizonazo.

Watu wetu tuwapate elimu ya maana zaidi; shule za kata tuziboreshe tuongeze walimu katika shule hizo na hivyo tutakuwa na watu walio tayari kuijenga nchi.Kupitia ELIMU ukombozi wa kweli utapatikana. Wanafunzi wetu tuwafunze kujitegemea kwa maana ya kujenga udadisi wao, kuimarisha ubunifu wao na kuwawekea misingi ya kuwa na fikra zao binafsi. Ili Tanzania na Afrika kwa ujumla tuweze kuendelea tunahitaji FIKRA ZETU WENYEWE fikra tunazotumia ni za kuazima; haziwezi kutufikisha mbali. Tutapata fikra zetu wenyewe tutakapowaweka wanafunzi wetu kwenye mazingira ya kufikiri, kutafakari, kupenda hesabu na masomo ya sayansi. Kwa kuanzia tufundishe masomo ya FALSAFA kwa shule zote za sekondari.

Ardhi tunayo tena ya kutosha; tuilinde na kuwapatia wananchi kwa usawa hatutaki kuingia kwenye migogoro ya Zimbabwe, Kenya, na sehemu zingine duniani.


 
Siasa zetu: Siasa ni muhimu mno. Kwa maoni yangu hii nd’o hutoa mwongozo ama dira kwa nchi, ukiwa na siasa mbaya basi huendi popote. Tanzania kwa sasa hatuna siasa nzuri; hili ni dhahiri, sisi si wajamaa wala si mabepari na mfumo tulionao haufahamiki, walu siufahamu. Kama hatujui kinachotuongoza basi hatuwezi kwenda popote. Siasa ndo hasa itatoa mwongozo kwenye uchumi wa nchi na hatimaye kwenye mambo ya kijamii.


Uongozi bora. Uongozi bora ni rahisi sana. Ili uongozi uitwe bora una kazi moja tu; kutafsiri katika vitendo sera zake yenyewe, sera ambazo zinakubaliwa na wananchi walio wengi. Kuwe na utawala wa sheria ambao ni huru na wenye uwezo wa kusimamia mambo yake bila kuingiliwa. Kwa kufanya hivyo tutapiga hatua kubwa na kufanya wananchi wetu waishi maisha yanayomfaa binadamu huru kama inavyotakikana.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

Thursday, December 8, 2011

UHURU NIGHT


















Wanachuo wa STELLA MARIS MTWARA UNIVERSITY COLLEGE wameendesha mjadala juu ya uhuru wa Tanzania bara. Ni jambo jema mno kusikiliza mawazo na malubano ya kihoja ya wanataaluma / wanazuoni.

Hapa chini kuna sehemu kidogo tu ya yaliyojiri katika mazungumzo hayo. Mijadala ndo hasa fursa za vijana kujifunza kujenga hoja na kuwa na mawazo yetu binafsi jambo hili ni muhimu sana.

Independence and Freedom of TanzaniaJe, Tanzania ipo huru?

Wanachuo wa STELLA MARIS MTWARA UNIVERSITY COLLEGE jioni ya leo wameandaa mdahalo kuadhimisha Jubilei ya dhahabu ya Uhuru wa Tanzania bara, kipindi hicho ikiitwa Tanganyika.

Tanganyika, sasa Tanzania bara, ilipata uhuru wake toka kwa waangalizi wa kiingereza. Waingereza walipatiwa mamlaka ya kuilinda Tanganyika ili itakapokuwa tayari waipatie uhuru wake… maelezo zaidi ni historia ya uhuru wa Tanzania…

Wanachuo wamejadiliana juu ya masuala mengi ya msingi kwa taifa la Tanzania. Wameangalia muda uliopita, uliopo na ujao. Wameangalia mafanikio, changamoto, kufeli kwa viongozi na taifa kwa jumla. Lakini wanachuo wameangalia nafasi na mchango wao pia katika maendeleo ya Tanzania.

Wanachuo waliuchambua uhuru kupitia nyanja kuu tatu:


ii. Kijamii na

iii. Kiuchumi

Watanzania wana uhuru mkubwa kuliko wananchi wa nchi nyingi jirani barani. Hata hivyo changamoto ya uhuru huu ni kwamba uhuru huo unahitaji kwenda sambamba na haki; kuwe na haki kwa wananchi.

Imeelezwa kwamba, wasomi wetu wenyewe ndo hasa wanaididimiza nchi. Wasomi hao wanasaini mikataba mibovu inayoleta kipato duni kwa nchi na wananchi wengi.

Mwalimu JKNyerere aliwaambia wananchi waende vyuoni ili waisaidie nchi na wananchi lakini leo wasomi hao nd’o wasaliti wa taifa. Hawainufaishi nchi katu; wanatumia kalamu zao kuwaibia watanzania wa kawaida.

Wakati Tanganyika ikipata uhuru kulikuwa na lengo kuu la kuwashinda maadui wakuu watatu:

i. Ujinga,

ii. Maradhi na

iii. Umasikini

Wanachuo wamejiuliza tumepiga hatua kiasi gani kushinda vita ya adui hawa watatu?

Leo, twaambiwa watanzania ni wajinga zaidi kuliko wakati tulipopata uhuru; - wasomi wanasaini mikataba mibovu inayoiweka nchi katika hali ngumu kiuchumi ilihali mharibifu husika aendelea kutembea huru tu; hivyo watanzania bado tu wajinga.

Leo hii watanzania bado tu wagonjwa; tunakimbilia kwa waganga wa kienyeji kupunga mapepo na kunyweshwa dawa ya kikombe, kijiko, kibuyu… n.k

Wananchi wengi vijijini wanaendelea kuishi katika umaskini. Hawa masoko ya uhakika wala uhuru wa kuuza mazao yao ili kujipatia mahitaji yao. Wengine wanazalisha kiashi cha kutosheleza kwa miezi kadhaa tu.

Sunday, December 4, 2011

TUMETHUBUTU, TUMEWEZA NA TUNASONGA MBELE!

Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika - Tanzania Bara












































Miaka 50 ya Uhuru. Siku ya Uhuru Mwalimu Julius Kambarage alibeba bango lililoandikwa
"Tanganyika 1961 Complete Independence." Leo miaka hamsini baadaye watanzania wajiuliza je, ni kweli kuwa tu huru?

Nchi imefanikiwa katika mengi, lakini pia kuna changamoto za kutosha ambazo bado zi mbele yetu watanzania...

Heri ya Siku ya Uhuru Watanzania wote...
Tuangalie mazuri tuliyofanikiwa na yatutie nguvu kusonga mbele zaidi...

Makosa tuliyofanya yawe kweli vyanzo vizuri vya kupiga hatua mbele zaidi


Siku ya Uhuru wa Ghana rais Kwame Nkrumah wa nchi hiyo alisema " Ghana you are free for ever" Haya ndo maneno ambayo napenda tuyaseme kwa taifa letu tukufu la Tanzania.  "TANZANIA YOU ARE FREE FOR EVER!"

               TANZANIA HAPPY GOLDEN JUBILEE - GOD BLESS YOU MY DEAR  TANZANIA

Miundo Mbinu wakati wa Mvua Dar!

Maeneo ya Mbagala wakati wa mvua