Saruji ya Rhino/ Kifaru - Picha na wadau |
Saruji ya Simba- Picha wadau husika |
Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoendelea, uchumi wake kwa mujibu wa taarifa rasmi, japokuwa bado haujatafsiriwi kwenye maisha ya mwananchi wa kawaida, unaendelea kukua kwa kasi ya zaidi ya asilimia 6. Kasi ya asilimia sita, hii maana yake nini kwa mkulima wa Sangamwalugesha, Chibe, Kinyanambo n.k. Pamoja na uchumi wa Tanzania kukua kwa kiasi kilichoelezwa bado nchi hii haizalishi bidhaa nyingi zinazotumiwa na wananchi wake. Kumbe mawazo yale yale ambayo Mwalimu Julius Nyerere, Mzalendo Thomas Sankara na kanuni za kimaendeleo zinayapinga, waTanzania na waAfrika wengi hutumia bidhaa na huduma wasizozalisha wenyewe. Mfano magari mengi yenye kuleta foleni ndefu katika miji yetu hususani majiji, simu za mkononi ambazo kulingana na tafiti za hivi karibuni zimeleta mapinduzi makubwa na chanya ya mawasiliano hapa nchini na sehemu nyingi barani Afrika; pamoja na umuhimu wa bidhaa na huduma hizi hakuna ambazo tunazalisha wenyewe; karibu kila kitu kinatoka nje ya mipaka yetu. Sisi tunaendelea kuwa mabingwa katika matumizi ya bidhaa hizo toka nje na tena hushiriki kupata matoleo mapya zaidi, bila kuumia rohoni na akilini kuwa tunatumia tu walivyozalisha wengine na kwamba sisi pia tuna jukumu la kuzalisha.
Coca Coala - Picha wadau husika |
Hapa nchini na nchi nyingi Afrika, tuna bidhaa nyingi zinazotoka nje ya bara letu, zipo pia zinazotengenezwa katika nchi zetu. Kuna bidhaa anuwai katika maduka ya bidhaa; baadhi ya mahitaji hayo yapo toka viwanda, nchi, tamaduni na ustaarabu tofauti na wa nchi mbalimbali. Chukua mfano wa dawa ya meno. Madukani zipo za kila aina; Whitedent, Colgate, Rungu, nini dent na kadhalika.., Sabuni za kipande; Jogoo, Mbuni, Magwanji, Dobi...Sabuni za kuogea; Malaika, Ayu, Geisha, Protex, Familia...Sigara; Nyota, Baridi, SM, Aspen, Portsman n.k. Baadhi ya bidhaa nilizozitaja huwa na maelezo ya matumizi na faida kwa mlaji / mtumiaji. Hata hivyo tuna bidhaa nyingine nyingi ambazo hazitoi maelezo yoyote ya matumizi, faida na hata hasara kwa mtumiaji lakini bidhaa hizo zipo madukani na sehemu nyingine za kujipatia mahitaji. Ni jambo muhimu na lazima kwa bidhaa kuwa na maelezo kwa mtumiaji. Vyombo husika nchini vina jukumu la kufanya hivyo ili kunusuru afya za wananchi na kuwawezesha kufika inapotakiwa.
Nchini kuna mafanikio yaliyofikiwa; watengeneza sigara walitakiwa kuweka alama ama tangazo linaloonyesha madhara ya bidhaa hiyo na kwamba atakayeamua kuitumia afanye hivyo kwa hiari yake mwenyewe na si kwa kukosa elimu. Nadhani halikuwa jambo jepesi, pamoja na kwamba maandishi yale ni madogo, lakini walau jambo hilo limefanyika. Hata hivyo kuna bidhaa nyingine nyingi zinahitaji kuelezewa ili kufanya mambo yaende sawa sawa. Natumia mifano miwili tu hapa. Mmoja ni mfano wa bidhaa inayoingia mwilini mwa binadamu na mwingine ni wa bidhaa tunayoitumia kujenga nyumba zetu; vinywaji baridi na saruji.
Kinywaji Pepsi - Picha wadau husika |
Vinywaji baridi al maarufu zaidi SODA; havionyeshi vilivyotumika kutayarisha bidhaa hiyo. Faida wala hasara yake mwilini haijulikani kwa watu wengi. Binafsi naamini kuwa bidhaa hizi zina faida na hasara mwilini kama ilivyo kwa bidhaa nyingi, sasa kama ni hivyo kwanini mimi mtumiaji sipatiwi hiyo elimu? Je nini lengo la kutotoa elimu hiyo kwa mtumiaji? Je, tunaangalia faida za kiuchumi tu kuliko afya ya mlaji? Ni muhimu kwa vyombo husika kuwasimamia waandaa bidhaa hiyo ili watoe hayo maelezo muhimu. Na serikali kwa ujumla wake inalazimika kusimamia hilo, ni vyema kufanya hivyo bila kuogopa tu kupungua kwa kodi toka makampuni husika pindi wananchi watakapofahamu kilichomo ndani ya vinywaji hivyo na kusitisha ama kupunguza matumizi yake. Najua yamekuwa ni mapokeo kwa baadhi ya bidhaa, toka nchi fulani zenye nguvu kiuchumi, kutotaja vilivyomo kuepuka mbinu zao za biashara kuibwa na washindani wao, lakini sisi tunasema afya za watu wetu walio wengi ni muhimu zaidi kuliko faida za wachache wanaonufaika kupitia ujinga wetu juu ya bidhaa zao.
Saruji Twiga - Picha na wadau husika |
Saruji Tembo - Picha na wadau husika |
Hitimisho la jumla ni kwamba wazalishaji wote nchini na barani Afrika wazalishe bidhaa zenye ubora, maelekezo ya matumizi kwa walaji / watumiaji ili kujenga afya njema kwa wananchi na kusaidia kusukuma mbele zaidi hatua za kimaendeleo kwa wananchi mmoja mmoja, Tanzania na bara Afrika zima kwa ujumla wake.