Tuesday, December 11, 2012

SACCOS suluhisho la Mitaji kwa Wasanii


Picha kwa hisani ya mtandao Mkurugenzi wa Basata ndugu Ghonche Materegho na Mbunifu mahiri wa sanaa ya mitindo ya mavazi nchini Tanzania ndugu Mustafa Hassanal  
Picha kwa hisani ya Tanzaniatoday 
Na Mwandishi wa BASATA

Wasanii nchini wametakiwa kutumia vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) ili kujiwekea akiba itakayowawezesha kukopa ili kuendeleza kazi zao za Sanaa.

Akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa SAA Saccos ambayo inamilikiwa na washereheshaji (Mc’s) na wachezeshaji muziki (Dj’s), Emmanuel Urembo, amesema saccos ni suluhisho la mitaji kwa kazi za wasanii ambao wengi wao wameshindwa kukamilisha kazi zao kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.

Saccos zinaweza kuwasaidia kupata mitaji na kujikwamua kiuchumi kwa kupata mikopo yenye riba nafuu ili kuendeleza ubunifu walionao, kwa kuwa wasanii wamekuwa hawana sifa za kukopesheka na benki mbalimbali kutokana na kutokuwa na fedha na dhamana za zinazowezesha mkopaji kupewa mikopo, lakini kwa kupitia saccos zao wenyewe wanaweza kujikopesha na kujiendeleza zaidi.

Aidha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini, Ghonche Materegho, aliwasisitiza wasanii kuanza kujizoesha kujiwekea akiba. Aliwahimiza wasanii kujifunza kwa SAA ambao wameshaanza katika mfumo huu wenye kuleta maendeleo na tija katika sekta ya sanaa, “kuendelea kulia juu ya ukosefu wa mitaji ya kufanyia kazi zetu na miradi ya sanaa hakutusaidii kusonga mbele, bali tunapaswa kujikwamua wenyewe kwa kuanzisha vyama hivi vya kuweka na kukopa kwa maendeleo yetu wenyewe” alitilia mkazo zaidi.



No comments:

Post a Comment