Monday, August 6, 2012

Wabunge ‘wala’ rushwa marufuku kuingia China

Bunge la Tanzania Mjini Dodoma















Tumeambiwa na tunafahamu siku zote kuwa rushwa ni adui wa haki, na ni ya wananchi, ya binadamu, ama ya viumbe vilivyo hai walau kulingana  na miongozo na makubaliano yetu. Moja ya makubaliano hayo, kwa Tanzania ni kuwa rushwa ni adui wa haki, na kwenye kanuni/ ahadi za mwanaTANU (chama kilichopigania uhuru wa Tanganyika) kulikuwa na ahadi ya kutotoa na kutopokea rushwa kwani hupinga ama huzuia watu wengine kupata haki zao.

Katika nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwa mojawapo, kuna utaratibu wa kuwa na chombo cha kutolea mawazo, kuihoji serikali iliyo madarakani, kutunga sheria n.k. Chombo hicho kinafanya kazi kwa uwakilishi; si rahisi kwa mwananchi mmoja mmoja kuingia katika chombo hiko kutetea, kudai haki yake ama/ na kufanya shughuli zingine za chombo hicho ambazo kwetu kinajulikana kwa jina la BUNGE. Kwa kuwa si rahisi wote kuingia basi tumelazimika kuwa na wawakilishi wachache ili wawe SAUTI zetu na waseme na kutenda kwa niaba yetu. Hivi karibuni tumesikia habari ya kushangaza juu ya hawa wawakilishi wetu. Tumesoma na kusikia vyombo vya habari vikielezea juu ya baadhi ya wawakilishi wetu hawa wakifanya kile tulichofundishwa kuwa ni adui wa haki, sio lengo la makala hii kuongelea suala hilo bali tu kuiwasilisha makala iliyo katika gazeti la MTANZANIA inayoeleza juu ya kicha habari.   

Mwalimu JKNyerere aliwahi kusema IKULU ni patakatifu nadhani BUGENI halikadhalika ni vivyo hivyo. Je, kama kweli kuna wabunge wameenda kinyume na utakatifu inafaa kweli waendelee kuwepo patakatifu?

Na Arodia Peter .

TUHUMA za rushwa zinazoendelea kuwaandama wabunge, zimechukua sura mpya, baada ya Serikali ya China kujiandaa kupiga marufuku wabunge wote wanaotuhumiwa kujihusisha na rushwa kuingia nchini humo.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata kutoka ubalozi wa China hapa nchini, zinasema umepokea taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wakuu wa China, wafuatilie kwa karibu wabunge wote wanaotuhumiwa kwa rushwa, kisha watume taarifa ili wakibainika wasiingie kwenye nchi hiyo.
“Tumeletewa taarifa na viongozi wetu wa ngazi za juu, kuwa tufuatilie kwa kina wabunge wote ambao wanatuhumiwa na wakibainika majina yao yatumwe China, ili wazuiliwe kuingia kule,

…unajua taifa letu ni taifa ambao halina mchezo na mtu anayepokea rushwa ovyo ovyo na ni kosa la jina. kwa kiongozi kama hawa wabunge kujihusisha na siasa,

“Kwa kipindi chote hiki, kama wabunge hawa wangekuwa China leo hii, tungekuwa tunazungumza mambo mengine, wangekuwa wamechukuliwa hatua kali,

“Tunashangaa kuona kwa nini hapa kwenu, bado wanaendelea kuruhusiwa kuingia bungeni… au wanasubiri majibu ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizi,” kilihoji chanzo chetu.

Chanzo hicho, kilisema ubalozi wa China hapa nchini, umetuma maofisa wake mjini Dodoma kwa ajili ya kupata mwenendo wa wabunge wote wanatuhumiwa.

“Hivi sasa hapa Dodoma kuna maofisa wa ubalozi wa China, wanaendesha uchunguzi kuhusu tuhuma hizi, ikibainika ni za kweli baada ya majina ya wabunge ‘wala rushwa’ kutajwa, watachukua picha zao kwa ajili ya kuzituma China, ambako hawataruhusiwa kukanyaga kwa sababu kwao rushwa ni kosa la jinai,” kilisema chanzo chetu.

Naye Mratibu wa maombi yanayoendeshwa na Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania, mjini Dodoma Mchungaji William Mwamalanga alisema kwa kauli moja viongozi wa dini, wamesikitishwa na tuhuma hizo.

Alisema viongozi wa dini ambao wamepiga kambi mkoani Dodoma, kwa ajili ya kuliombea taifa, wamewataka wabunge wote waliotajwa wajiuzulu mara moja.

“Viongozi wa madhehebu mbalimbali tupo hapa Dodoma, kwa ajili ya kuliombea taifa, lakini moja ya jambo kubwa ambalo tumekubaliana kupita katika majimbo yao, kueleza waumini wetu matatizo haya ya rushwa… tunataka wajiuzulu kwa ajili ya kulinda heshima zao,  
…viongozi wa dini wamekerwa na tabia ya wabunge kuhusishwa na rushwa, wao wana neno moja tu, wanataka Bunge livunjwe kwa sababu nje ya nchi tunachekwa mno.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na MTANZANIA jana, Mchungaji alisema, viongozi wote waliotajwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na kusababisha nchi kuingia katika mgao wa umeme bandia, wanapaswa kujiuzulu, ili kulinda heshima zao, na kamwe wasisubiri kuwajibishwa na kamati iliyoundwa ya Spika wa Bunge Anne Makinda.

Alisema si jambo jema kwa wabunge kusubiri kuchunguzwa na Kamati ndogo inayoongozwa na Brigedia Jenerali, Hassan Ngwilizi iwaumbue.

“Dawa ya wala rushwa si kuunda kamati kuwachunguza, vitendo hivi vinafanywa kwa siri kubwa, wabunge wetu wafike mahali wabadilike, kiongozi akituhumiwa, lazima jambo hilo lipo, kama halipo basi linakuja.”

“Vitendo vya rushwa ni kama vile mtu kukamatwa ugoni na mke au mume wa mtu, ukikuta vinafanywa mchana kweupe hicho ni kiwango cha ukichaa, rushwa katika nchi yetu imefikia kiwango cha ukichaa.”

“Wanaotuhumiwa wasingoje kamati ya Spika, tutawaona ni wakweli wakijiuzulu, hata kama hawajatenda, wanapaswa kuwa mfano maana hizo ni tuhuma nzito kwao.”

“Wakumbuke aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alipoamua kujiuzulu si kwamba alikuwa na makosa ya moja kwa moja, bali alitaka kulinda heshima ya chama chake na taifa lake,

“Wito wetu kwa hao waliotuhumiwa watambue taifa letu lipo katika wakati mgumu sana, rushwa ilikofikia inaweza kuangusha nchi wakati wowote kwa kiwango kisichotarajiwa, hivyo wataonekana waungwana na hekima ya hali ya juu kama wakijiuzulu nafasi zao na kuwapisha wengine” alisema Mchungaji Mwamalanga.

Alisema hivi sasa, Watanzania wamefika mahali hawamwamini mtu yeyote, si kamati za Bunge wala vyama vya upinzani, kwa sababu baadhi yao wametajwa katika kashfa za aina hiyo.

Mchungaji huyo alikwenda mbali zaidi na kuonya kuwa, kama watagoma kujiuzulu, basi kwa kutumia umoja wao wa dini watakwenda katika majimbo yao na kuwataka wananchi wasiwape tena nafasi katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

“Sisi kwa umoja wetu, tumekubaliana kuombea taifa kwa miezi mitatu mfululizo, kiongozi mwenye kujihusisha na rushwa tutamtaja hadharani na katika jimbo lake la uchaguzi,

“Tunao ushahidi wa kutosha, mgao wa umeme kwa miaka yote hii, ilikuwa hujuma kwa umma, viongozi wote waliohusika wamelidhalilisha taifa kwa ukimya wao, wabunge wa upinzani hawakupaswa kuwemo katika kashfa hii …wao ndiyo walikuwa tumaini la Watanzania.”

“Mathalani tamko la aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo William Ngeleja kwamba, mgao wa umeme nchini ungekuwa historia, ilikuwa ni ghiliba tu, kwani Watanzania waliendelea na mgao huo bila kuwepo na dalili ya kuisha, kibaya zaidi watendaji waliendelea kumdanganya Rais kwamba, mambo yako safi, haya hayavumiliki” alisema Mchungaji Mwamalanga.

Kuhusu uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alisema ni kiongozi mzuri, isipokuwa watu wanatumia upole wake kujinufaisha binafsi na kuliacha taifa.

“Rais Kikwete ni mpole na muungwana sana, tatizo watumishi badala ya kutumia mwanya huo kujenga nchi, wanautumia vibaya kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

“Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye hekima na busara, alijua si kila ovu linaweza kuundiwa na kujadiliwa katika vikao, alikuwa na ujasiri wa kukemea hadharani bila woga na viongozi wenzake walimtii kwa hilo.”

“Ni bahati mbaya watumishi na watendaji wa Serikali hawana huo woga tena, wanafanya watakavyo kwa kisingizio kwamba hadi mahakama iwatie hatiani,” alisema.



No comments:

Post a Comment