Sehemu ya umati uliofika kumuaga mwanachuo aliyeaga dunia |
Kama ilivyo kwa mawiyo na macheyo ya jua, ndivyo ilivyo kwa kuzaliwa na kifo. Msemo mmoja wa kiafrika wasema: "Kamwe ardhi haichoki kutupokea" ama kama inavyojidhihiri katika vitabu vitakatifu; kuna muda wa kila jambo: kupanda na kuvuna, kuzaliwa na kufa... ama tena binadamu u mavumbi na mavumbini utarudi. Na zaidi na pengine muhimu kupindukia; mbegu isipoanguka ardhini na kufa hubaki kama ilivyo, lakini ikianguka na kufa huzaa zaidi na zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla. Mbegu ya mmea wowote inaweza kufananishwa na maisha ya binadamu.
Inafaa kukumbushana kuwa mara tu binadamu anapotungwa kwenye tumbo la mamaye, tayari anakuwa na sifa za kuaga dunia, kufa. Hii inadhihirisha kwa maisha ya vichanga ambavyo hata kabla ya kuzaliwa, hufariki dunia. Vijana wengi hudhani ya kuwa kifo ni kwaajili ya wazee; watu walioishi kwa miongo kadhaa hapa duniani. Ni vyema tuambiane kuwa hii si kweli, kila binadamu yupo tayari, ameiva, amepevuka kwaajili ya kifo. Kama isemwavyo hivi leo kila mtu ni marehemu mtarajiwa. Kwa mantiki hiyo basi hatuna haja ya kuogopa. Kinyume chake inafaa tujiandae kwa tukio hilo la uhakika kama ilivyo kwa kuchomoza jua bila juhudi zetu kila asubuhi, kwa uzoefu tu twafahamu kuwa jua litachomoza. Pamoja na kujua ukweli huo bado hatuzoei suala hili.
Jeneza likiwa ndani ya ndege tayari kwa safari |
Kamwe hatuzoei kifo kwa sababu kila kinapotokea, kinatokea kwa mtu ambaye hajawahi kufa. Najua hili si jambo geni lakini huo ndo ukweli wenyewe, je ni kwanini? Jambo hili li hivyo? Bila shaka ni kwa sababu kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kiimani twaelewa kuwa binadamu ameumbwa na Mungu na kuwa binadamu nd'o kazi nzuri kuliko kazi nyingine zote za Mungu na ni kwa sababu hiyo kila anapofariki dunia mwenzetu basi sisi hupatwa na simanzi lisiloelezeka, hata wale wenye mioyo migumu huguswa pia na kifo cha mpendwa ama mwanadamu ambaye walimfahamu, kuishi naye na kadhalika. Kifo ni sehemu ya ukamilifu wa binadamu.
Katika vitabu vitakatifu twaambiwa ya kuwa Mwenyezi alitufahamu hata kabla ya kuiumba dunia hii, kama nilivyoeleza hapo awali, binadamu kwa hakika ni kazi bora kabisa ya Mwenyezi Mungu. Twajua pia kuwa binadamu huanza kibaiolojia pale yai la mwanamke linaporutubishwa na mbegu ya mwanamume: kuanzia hapo safari ya binadamu fulani kibaiolojia huanza, na maisha yake huanza hapa duniani kwa kuzaliwa. Binadamu anazaliwa anaishi na hatimaye lazima afariki dunia. Kupitia kifo mzunguko wa binadamu unakamilika. Hivyo tukichukulie kifo kama ukamilifu wa ubinadamu wetu. Hata hivyo jambo la msingi hapa ni je, maisha hayo tunayaishi vipi hapa duniani?
Hivi leo wengi tunadhani kazi yetu katika sayari hii ya dunia ni kukusanya na kujilimbikizia mali nyingi iwezekanavyo. Tunajisahau, ukweli na wito wa binadamu ni kutoa mchango wa kuiboresha zaidi dunia kwaajili ya utukufu wa Mungu kama asemavyo Inyasi wa Loyola (1491-1556) . Tunaweza kuiboresha dunia kila mmoja kwa nafasi yake; mwalimu afanye kzi yake ya ualimu vyema, mwanasiasa afanye kazi yake vizuri, mwandishi, mkulima, mwanasayansi, mwanafalsafa, mwanafunzi na kila mmoja wetu afanye vyema kabisa kazi yake. Kushidwa kufanya vyema ama kutimiza wajibu wetu ni sawa na kushindwa kuitikia wito wa maisha yetu na tukishindwa kufanya hivyo basi maisha yetu yanakosa maana!
Tafakari hii imenijia baada ya kuona nyuso nyingi za huzuni wakati wa kumsindikiza mwanachuo wa stemmuco hivi karibuni baada ya kukamilisha safari yake hapa duniani.