Sunday, March 11, 2012

Mashindano ya PRO-LIFE - MTWARA

Picha kwa hisani ya google
Mashindano ya Pro life, ambayo yanaanza kujenga mizizi mjini Mtwara, kwa mwaka huu 2012 yamefunguliwa rasmi hapo jana. Mashindano hayo yanajumuisha taasisi kadhaa za elimu mjini Mtwara.

Moja ya malengo la mashindano haya ni kujenga uhusiano baina ya wanavyuo katika manispaa ya mji huu wa kusini mashariki mwa Tanzania. Yanatumika pia kama sehemu ya matumizi sahihi ya nguvu za vijana; kundi la watu wenye nguvu kubwa za mwili. Mashindano ni sehemu ya mazoezi muhimu yanayohitajika kwaajili ya kujenga na kuulinda mwili.

 Pamoja na malengo mengine mahususi na mazuri mno yaliyotajwa; Jina la mashindano haya lengo lake hasa ni kutetea na kulinda uhai kama jinsi ilivyo kwa malengo halisi ya "Pro-life". Pro life ni vuguvugu lenye lengo mahususi la kutetea na  kulinda uhai wa binadamu. Binadamu huanzia kwenye muungano wa yai la mama na mbegu ya baba, na hapo safari ya mwanadamu mpya huanza. Kwa hiyo binadamu anaanzia tumboni mwa mama hata kabla ya kuzaliwa. Kutokana na maelezo hayo basi utaona kuwa Prolife hutetea uhai wa mtoto anayekuwa tumboni mwa mama na kwa hivi hupinga utoaji mimba kwa lengo la kutetea na kulinda uhai.

Kwa hiyo basi vijana wa kike na wa kiume wanaalikwa kuheshimu uhai wa mwanadamu kwa kujizuia kabisa kushiriki katika utoaji mimba. Kunaweza kuwa na sababu lukuki za kuhalalisha utoaji mimba lakini ukweli ni ule ule kwamba utoaji mimba ni uuaji ni uharibifu wa maisha. Vijana hivi leo wanashindwa kujizuia kushawishiwa kutoa mimba; njia rahisi ya kuepuka kujiingiza kwenye kosa hilo ni kuwa na mahusiano yenye heshima. Mvulana na msichana wawe marafiki ili kusaidiana kukua kikamilifu katika ubinadamu (mwanaume hujifunza toka kwa mwanamke na kinyume chake pia) mahusiano ya kimwili yasubiri vijana watakapofunga ndoa na kutambulika mbele ya jamii na mwenyezi kuwa wao ni bwana na bibi fulani. Kufanya hivyo kutasaidia kuondoa utoaji mimba-uuaji!

Katika tafsiri ya leo ya kutetea na kulinda uhai vijana tunaalikwa kuacha mambo yote ambayo yanapunguza maana ya maisha yetu. Vijana tupunguze ama kuacha kabisa unywaji wa pombe, tuache uvutaji wa sigara kwa kuwa hasara na matatizo yanayosababishwa na uvutaji ni makubwa kuliko furaha ya uvutaji. Kwa wale tunaotumia dawa za kulevya tuache na tuwashawishi rafiki zetu waache ushiriki na utumiaji wa vitu hivi vinavyopingana na maisha. Tukifanikiwa katika hayo amani, upendo na mafanikio vitatamalaki kote duniani, lakini vianzie kwa kila mmoja wetu.

Kwa hivi basi mashindano ya "STEMMUCO Pro-life 2012" yanalenga kutetea na kulinda uhai wa binadamu. Vijana wote walio mashindanoni wanapaswa kufahamu hilo na kwamba wao tayari wanakuwa ni mabalozi wa uhai-ni watetezi na walinzi wa uhai. Mashindano mema!!!

No comments:

Post a Comment