Saturday, March 17, 2012

Mkanganyiko wa Maisha: Misitu ama Maisha?


Baiskeli hii TZ MKAA ikiwa imeengesha bidhaa kusubiri wahitaji mjini Mtwara
Kuishi kwenye jumuiya ya wasomi ni faida kubwa. Msomi, kwa tafsiri yangu ni mtu yeyote mwenye elimu kuanzia darasa la saba, ama kwa upana zaidi anayejua kusoma na kuandika, lakini mwenye moyo wa utafiti, kujisomea na kuwashirikisha wengine taarifa ya anachosoma ama anachotafiti.

Mwanachuo wa Stella Maris Mtwara University College (STEMMUCO), ambao kwa maelezo yangu ni wasomi, wapo katika harakati za kuandika taarifa, ripoti ya tafiti walizofanya sehemu mbalimbali hapa nchini. Kuna mada nyingi karibu kadri ya idadi ya watafiti hao. Kuna ripoti juu ya hali ya uchumi nchini, hali ya hisabati shuleni, nafasi ya sayansi katika elimu ya tanzania, hali ya elimu nchini, ushiriki wa wasichana katika elimu, jando na maendeleo, kwa ufupi nyanja zote muhimu zimeguswa, kuanzia siasa, uchumi, sayansi, na jamii. Zaidi tasnifu hizo za wasomi zimeangazia makundi mbalimbali katika jamii; wazee, wanawake, walemavu, vijana na kadhalika.

kwa ufupi, makala hii inagusia mkanganyiko unaowakuba vijana wanaofikia kundi la kujitegemea maishani. Hili ni kundi muhimu mno; hii ndio nguvu kazi hitajika ya ujenzi wa taifa letu. Tafiti zinaonyesha kuwa kundi kubwa la vijana karibu ya vijana milioni mbili na laki tatu (2.3), takwimu rasmi za serikali ya Tanzania 2005, hawana ajira zinazoeleweka. Kumbuka hii ni idadi ya makadirio tu, kuna idadi kubwa sana ambayo mara nyingi haijumuishwi kwenye taarifa rasmi, kwa hivi basi, vijana wengi hawana kazi. na wanakumbana na mkanganyiko wa maisha.

Baadhi ya sera zinakataza ama zinapiga vita shughuli ambazo vijana huzitegemea kuendesha maisha yao. Bishara ya mkaa ni moja ya biashara zinazopigwa vita kwa vile watayarishaji mkaa wengi huvuna miti kwaajili ya kuni bila mpangilio maalumu. Ni kweli zao la mkaa linaharibu mazingira na kuhatarisha dhana ya maendeleo endelevu. Wakati zao hili linapigwa vita, mahitaji na matumizi yake ndo kwanza yanazidi kuongezeka kila uchao. Na hii ni dhahiri kuwa mkaa ni bidhaa ambayo itaendelea kutumika kwa miaka mingi ijayo; kama wasemavyo vijana wa Bongo Flava; mkaa bado tutakuwa nao kwa muda mrefu sana. kumbe tufanye nini sasa.

1. Mosi, maafisa misitu, ama wataalamu wa maliasili waweke utaratibu wa kupanda miti kuwe na maeneo maalumu ya kupanda miti na vijana wavuna miti kwaajili ya mkaa wapewe maeneo ya kupanda miti na kuitunza ili hali waonyeshwe eneo maalumu la kuvuna miti ya kazi yao hiyo.

2. Pili, mamlaka husika zenye kujihusisha na gesi ya kupikia majumbani waangalie uwezekano wa kupunguza kwa kiasi kikubwa kodi za chanzo hicho mahususi cha nishati hitajika ili wananchi wengi ikiwa ni pamoja na mashambani waweze kuitumia pia.

3. Tatu, tafiti zifanyike kuangalia upunguzaji wa bei ya umeme ili walio na fursa ya kutumia nishati toka shirika la taifa la umeme watumie pia kwa kupikia; kwa sasa bei yake ni kubwa mno kwa mwananchi mwenye kipato cha wastani kumudu gharama hizo.

Mpanda baiskeli akitafuta wahitaji wa biadhaa yake manispaa ya Mtwara-Mikindani
Nchini Tanzania hali halisi ndivyo ilivyo vijana wengi wamejiajiri kuuza mazao ya miti

Tukifanya haya kuna uwezekano wa kufikia ndoto tuliyonayo ya kuwa na Watanzania wa daraja la kati ifikapo 2025 kama inavyoelezwa kwenye mpango wa maendeleo wa taifa. Kinyume na hivyo vijana wetu wataendelea kuwa kwenye mkanganyiko mkubwa wa misitu ama maisha ya leo; je nikate miti ili nichome mkaa ama nisikate na kufa njaa? 

No comments:

Post a Comment