Tuesday, February 28, 2012

Kumbe wabunge wetu ni maskini vile !

Jengo la kisasa la Bunge la Tanzania huko Dodoma
Mbunge ni mwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi wengine kwenye chombo rasmi cha kuwasilishia mawazo na maoni ya wakaazi wa nchi wenzake. Kwa hivi ni mtu muhimu katika jamii, japokuwa anabaki kuwa mtumishi wa wananchi, kwani wao ndio hasa wanaompatia ridhaa ya kuwaongoza.

Sasa ili mtu huyu aweze kufanya kazi yake vizuri ni vyema kwa hakika kuwa na mazingira stahiki ya kufanya kazi zake kwa weledi na hasa kwa uzalendo unaojidhihirisha kabisa.

Ili kuwa mbuge kwa Tanzania, tunahitaji mtu mwenye kuwa na sura na mfano wa watu anaowawakilisha ndio maana enzi zile wakaitwa 'ndugu' hivi leo ni waheshimiwa. Pamoja na kufanana na waajiri wake kwa maana ya kuyafahamu vyema mazingira yao na inafaa zaidi akiishi huko huko na wala si mjini tu, inafaa awe na nafasi kiasi ya kiuchumi kiasi ili mambo mengine yanayohusu kazi yake aweze kuyamudu kwa pesa zake mwenyewe. Si saw kila kazi ihitaji kodi za watanzania, hapo ndio has inafaa ajiulize anaifanyia nini Tanzania?

Makala hii imechochewa na taarifa niliyoiona kwene televisheni hivi karibuni na hatimaye kuingia kwenye mtandao wa youtube ikielezea japo kwa kifupi tu hali ngumu kiuchumi ya ndugu zetu wabunge. Hayo yamedhihirishwa na kiongozi wa bunge hilo la Tanzania alipoongea na wananchi wa jimbo lake huko Njombe. Kwa habari zaidi tazama hapa

Kwa hakika jambo hili nimeniacha na maswali mengi kuliko majibu. Kwanini watangaza nia hutumia nguvu na wakati wao mwingi vile kujinadi mbele ya wapiga kura ili wapate nafasi hii yenye umasikini wa kutupa?

Je, wengi wao huenda bungeni bila kujua kuwa kuna umasikini wa kiwango hicho?

Uwezekano mwingine wa suala hili ni kuwa watangaza nia na hatimaye wabunge wetu ni watanzania wenye uzalendo sana na  hakika maslahi ya taifa letu yamo mioyoni mwao kiasi kwamba pamoja na umasikini ulio bungeni, ambao nadhani watakuwa wakiufahamu kwani kwa hali ya kawaida mtu hufanya kwanza utafiti wa kile anachokitatuta, bado huamua kwenda bungeni kwenye umasikini wa kutupa.

Wabunge ni wawakilishi wa moja kwa moja wa watanzania. Na hivi wanabeba sura ya nchi yetu; bunge pale Dodoma likiwa kazini inamaanisha kuwa Tanzania yote kupitia majimbo ipo pale katikati ya nchi hii tukufu, na hivyo wawakilishi hawa lazima kuwajali vilivyo. Sasa kwa kuwa kiongozi wa moja ya nguzo kuu za uongozi wa taifa letu amesema kuwa kuna umasikini katika chombo hicho, itakuwa vigumu kwa hawa watumishi wetu kufanya kazi vizuri. Inafaa tutatue tatizo hili kwa kuwawekea wazalendo na watanzania wenzetu hawa mazingira mazuri ya kufanya kazi. Kwa kuwa tuna uzoefu wa kutatua matatizo yetu wenyewe basi natulitatue njia mojawapo ni kuunda tume kwaajili ya kuchunguza ukata unaowakabili waheshimiwa wetu.

Kupitia uchunguzi huo tupate mwongozo wa nini cha kufanya...
Picha zote kwa hisani ya google!

No comments:

Post a Comment