Sehemu ya wadau kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru |
Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ama ya iliyokuwa Jamuhuri ya Tanganyika, mkoani Mtwara yalifanyika kwa mdahalo wa kitaaluma Katika Chuo Kikuu cha STEMMUCO.
Kulikuwa na mada kedekede zenye kuangalia hali halisi ya nchi hii toka ijipatie uhuru wake toka mikononi mwa walezi wa kiingereza miaka hamsini kamili hivi leo. Asilimia kubwa ya washiriki ni wale waliozaliwa kisha uhuru. Baadhi yao ni watu waliopata fursa za kuzunguka sehemu mbalimbali duniani. Wengine walikuwa ni watu wenye taaluma kubwa kwa maana ya ujuzi na vyeti. Hata hivyo walikuwepo pia washiriki wachache waliokuwa hai wakati Tanganyika ikijipatia uhuru wake.
Matokeo ya mjadala, hususani ya wasomi wengi, yalidhihirisha kuwa toka uhuru, ukitilia maanani rasilimali nyingi tulizonazo, nchi hii haijapiga hatua kabisa. Mengi yaliyofanyika ni hovyo mno na kwamba juhudi kubwa na za haraka zinahitajika sana ili tupate nafuu. Hivyo kauli mbiu ya “Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” haina ukweli kabisa labda kama ni kuthubutu kuihujumu nchi. Ilhali wazee wachache walioshiriki mjadala huo na kuongea, japo kwa muda mfupi, walisema bila kificho kuwa nchi imepiga hatua kubwa ingawa bado kuna haja ya kutenda zaidi.
Binafsi naungana sana na wazee na wengine wenye mtazamo huo kuwa; nchi yetu imefanya mambo mengi mazuri na kuna juhudi zinaendelezwa ili tufanye vyema mara dufu. Hata hivyo kutokana na utajiri wa kiasili ulio katika maliasili ya nchi yetu, basi kweli, utaona kwamba tunatakiwa kuwa mbali sana kimaendeleo. Shida yetu kubwa kila mmoja wetu ni ubinafsi; kila mmoja anataka kunufaika yeye na familia yake kwanza, na kisha hapo ndo aangalie uwezekano wa kuwakumbuka wengine, uwezekano. Tuache ubinafsi na tujifunze toka kwa waasisi wa nchi yetu kujitoa muhanga kwa maendeleo ya watu na taifa letu. Sina hakika kama Mwalimu Nyerere, Mzee Kawawa, Shujaa Moringe Sokoine waliacha pesa kwenye akaunti nje ya nchi.
Utawala bora uimarishwe; wenye makosa washitakiwe na sheria ifanye kazi yake kwa uwazi na uhuru. Tuliambiwa ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Mambo haya yote na tuyazingatiwe na hatimaye tutaweza kufika tunakopaswa kuwa kulingana na rasilimali tulizonazo.
Watu wetu tuwapate elimu ya maana zaidi; shule za kata tuziboreshe tuongeze walimu katika shule hizo na hivyo tutakuwa na watu walio tayari kuijenga nchi.Kupitia ELIMU ukombozi wa kweli utapatikana. Wanafunzi wetu tuwafunze kujitegemea kwa maana ya kujenga udadisi wao, kuimarisha ubunifu wao na kuwawekea misingi ya kuwa na fikra zao binafsi. Ili Tanzania na Afrika kwa ujumla tuweze kuendelea tunahitaji FIKRA ZETU WENYEWE fikra tunazotumia ni za kuazima; haziwezi kutufikisha mbali. Tutapata fikra zetu wenyewe tutakapowaweka wanafunzi wetu kwenye mazingira ya kufikiri, kutafakari, kupenda hesabu na masomo ya sayansi. Kwa kuanzia tufundishe masomo ya FALSAFA kwa shule zote za sekondari.
Ardhi tunayo tena ya kutosha; tuilinde na kuwapatia wananchi kwa usawa hatutaki kuingia kwenye migogoro ya Zimbabwe, Kenya, na sehemu zingine duniani.
Siasa zetu: Siasa ni muhimu mno. Kwa maoni yangu hii nd’o hutoa mwongozo ama dira kwa nchi, ukiwa na siasa mbaya basi huendi popote. Tanzania kwa sasa hatuna siasa nzuri; hili ni dhahiri, sisi si wajamaa wala si mabepari na mfumo tulionao haufahamiki, walu siufahamu. Kama hatujui kinachotuongoza basi hatuwezi kwenda popote. Siasa ndo hasa itatoa mwongozo kwenye uchumi wa nchi na hatimaye kwenye mambo ya kijamii.
Uongozi bora. Uongozi bora ni rahisi sana. Ili uongozi uitwe bora una kazi moja tu; kutafsiri katika vitendo sera zake yenyewe, sera ambazo zinakubaliwa na wananchi walio wengi. Kuwe na utawala wa sheria ambao ni huru na wenye uwezo wa kusimamia mambo yake bila kuingiliwa. Kwa kufanya hivyo tutapiga hatua kubwa na kufanya wananchi wetu waishi maisha yanayomfaa binadamu huru kama inavyotakikana.