Thursday, March 8, 2012

Siku ya Wanawake duniani katika matukio Mtwara

Vazi rasmi siku hiyo ilikuwa kitenge - Naam kina mama wanapendeza
na kuongeza staha sana kwa mwanamke pale wanapovalia mavazi ya heshima




























Hii ni siku mahususi kwa wanawake duniani. Hutumika kuwakumbusha wanawake wenyewe, watunga sera, na jamii yote kwa ujumla juu ya haki na nafasi ya mwanamke katika nyanja zote za maisha.































Tafiti nyingi hapa Tanzania zinaonyesha kuwa mwanamke hususani yule wa kijijini anafanya kazi nyingi kuliko mwananchi mwingine yeyote. Pamoja na mchango huo mkubwa wa wanawake, mara nyingi juhudi zao hazitambuliki vya kutosha na wala hawathaminiwi na jamii kwa kiasi stahiki. Hivyo kwa siku ya leo ni fursa kuikumbusha jamii na wanawake wenyewe hasa wale wa mashambani. Ni dhahiri kuwa wanawake wengi vijijini wanafanya kazi nyingi kwa kuwa tamaduni nyingi, zenye mfumo dume, zinawalazimu kufanya hivyo.





























Tunawaomba na kuwapa changamoto wanawake wa mijini, kulihamasisha kundi hili lenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu. Mwaka huu, kwa kutambua nafasi ya elimu kuleta mabadiliko kwa jamii, wito umeelekezwa kwa ushiriki wa mtoto wa kike katika elimu kama kichocheo kikubwa kuleta maendeleo ya jamii.

Saturday, March 3, 2012

Duh angurumapo simba mcheza nani?


Hii toka kwa kaka michuzi
Hakuna ubishi kuwa watu wengi tunapenda mchezo wa soka hapa Tanzania.

kupitia huu upenzi wa mpira kwanini tusibuni njia ya kuhamasishana kwenye elimu kupita soka ili kiwango na ubora wa elimu yetu vikue pamoja na soka hasa la kina mama; soka la kina mama Tanzania ni bora zaidi kuliko la kina baba, kwa kigezo cha matokeo. Taifa Stars imewahi kuifunga timu nyingine mabao matano?


Hii ni keki tuliyokula siku ya ufunguzi wa Simba TV. Hata hivyo TV hiyo inayorusha vipindi vyake kupitia clouds tv inaishia tu mikocheni, haifiki walipo watazamaji wa mdenga, Mtwara, Lindi, Mazoo, Shytown, Ta etc fikisheni mapema basi! 

Harakati za Ubunifu wa vazi la Taifa?




Picha zote kwa hisani ya blogu la UDADISI

Thursday, March 1, 2012

Mtazamo Chanya Humjenga Binadamu!

Maneno haya ya kiingereza juu ya rais huyu wa Marekani ni fundisho la aina yake
tujifunze kupenda tunachofanya na tukifanye kwa moyo wote matokeo yake ni furaha na amani
Ujumbe huu nimeupata toka kwenye e-mail niliyotumiwa na Edward Ezekiel, kwa hakika ni ujumbe mzuri na wa maana mno.

Huu unawafaa vijana wote ambao ni wepesi wa kukatishwa tamaa na watu wengine. Kumbuka hakuna mtu mwenye mamlaka ya kukufanya ukose furaha, ili ukose furaha, ukasirike ama uwe kwenye aina yote ya hisia ni lazima wewe mwenyewe uamue; Lincoln ni mfano mzuri mno. Maneno ya watu wengine si yenye kutubomoa.

Fundisho la pili ni kufanya kazi zetu kwa uadilifu, ubunifu, umakini na zaidi ya yote upendo. Mambo hayo husaidia kuvumbua mbinu mpya za kurahisisha maisha na kuleta maendeleo kwa watu haraka. Ndugu huyu japo si Mwafrika na atukumbushe kutenda mema!

Je Afrika imejididimiza yenyewe?

Ndugu zangu salam,
Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere kinawakaribisha wote kwenye , Malumbano ya Hoja baina ya Wanafunzi wa Sekondari na Chuo Kikuu, mada ni " Handira hii inaamini kwamba Afrika imejididimiza yenyewe" ikifuatiwa na filamu ya "The Last Days of Walter Rodney" hapa UDSM-katika ukumbi wa Nkrumah, tarehe 03.03.2012 siku ya Jumamosi kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka 8:15 mchana. Malumbano haya ya hoja yatakuwa katika lugha ya Kiswahili. Nawaombeni tusambaze tangazo hili kwenye mitandao yetu ya jamii. Karibuni sana.
Nimeambatanisha ratiba na bango bonyeza hapa.

Walter Rodney Luanda
Mwalimu Nyerere Chair-Senior Administrative Officer

Tuesday, February 28, 2012

Kumbe wabunge wetu ni maskini vile !

Jengo la kisasa la Bunge la Tanzania huko Dodoma
Mbunge ni mwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi wengine kwenye chombo rasmi cha kuwasilishia mawazo na maoni ya wakaazi wa nchi wenzake. Kwa hivi ni mtu muhimu katika jamii, japokuwa anabaki kuwa mtumishi wa wananchi, kwani wao ndio hasa wanaompatia ridhaa ya kuwaongoza.

Sasa ili mtu huyu aweze kufanya kazi yake vizuri ni vyema kwa hakika kuwa na mazingira stahiki ya kufanya kazi zake kwa weledi na hasa kwa uzalendo unaojidhihirisha kabisa.

Ili kuwa mbuge kwa Tanzania, tunahitaji mtu mwenye kuwa na sura na mfano wa watu anaowawakilisha ndio maana enzi zile wakaitwa 'ndugu' hivi leo ni waheshimiwa. Pamoja na kufanana na waajiri wake kwa maana ya kuyafahamu vyema mazingira yao na inafaa zaidi akiishi huko huko na wala si mjini tu, inafaa awe na nafasi kiasi ya kiuchumi kiasi ili mambo mengine yanayohusu kazi yake aweze kuyamudu kwa pesa zake mwenyewe. Si saw kila kazi ihitaji kodi za watanzania, hapo ndio has inafaa ajiulize anaifanyia nini Tanzania?

Makala hii imechochewa na taarifa niliyoiona kwene televisheni hivi karibuni na hatimaye kuingia kwenye mtandao wa youtube ikielezea japo kwa kifupi tu hali ngumu kiuchumi ya ndugu zetu wabunge. Hayo yamedhihirishwa na kiongozi wa bunge hilo la Tanzania alipoongea na wananchi wa jimbo lake huko Njombe. Kwa habari zaidi tazama hapa

Kwa hakika jambo hili nimeniacha na maswali mengi kuliko majibu. Kwanini watangaza nia hutumia nguvu na wakati wao mwingi vile kujinadi mbele ya wapiga kura ili wapate nafasi hii yenye umasikini wa kutupa?

Je, wengi wao huenda bungeni bila kujua kuwa kuna umasikini wa kiwango hicho?

Uwezekano mwingine wa suala hili ni kuwa watangaza nia na hatimaye wabunge wetu ni watanzania wenye uzalendo sana na  hakika maslahi ya taifa letu yamo mioyoni mwao kiasi kwamba pamoja na umasikini ulio bungeni, ambao nadhani watakuwa wakiufahamu kwani kwa hali ya kawaida mtu hufanya kwanza utafiti wa kile anachokitatuta, bado huamua kwenda bungeni kwenye umasikini wa kutupa.

Wabunge ni wawakilishi wa moja kwa moja wa watanzania. Na hivi wanabeba sura ya nchi yetu; bunge pale Dodoma likiwa kazini inamaanisha kuwa Tanzania yote kupitia majimbo ipo pale katikati ya nchi hii tukufu, na hivyo wawakilishi hawa lazima kuwajali vilivyo. Sasa kwa kuwa kiongozi wa moja ya nguzo kuu za uongozi wa taifa letu amesema kuwa kuna umasikini katika chombo hicho, itakuwa vigumu kwa hawa watumishi wetu kufanya kazi vizuri. Inafaa tutatue tatizo hili kwa kuwawekea wazalendo na watanzania wenzetu hawa mazingira mazuri ya kufanya kazi. Kwa kuwa tuna uzoefu wa kutatua matatizo yetu wenyewe basi natulitatue njia mojawapo ni kuunda tume kwaajili ya kuchunguza ukata unaowakabili waheshimiwa wetu.

Kupitia uchunguzi huo tupate mwongozo wa nini cha kufanya...
Picha zote kwa hisani ya google!

Wednesday, February 22, 2012

Uelewa kwa vitendo!

Wanachuo wakionyesha uelewa kwa vitendo chuoni STEMMUCO
Hapa kaka akifanya kweli
Wanachuo wakionyesha uelewa kwa vitendo chuoni STEMMUCO
Dada hakubaki nyuma katu!

Monday, February 20, 2012

Elimu ya Majanga - Zima Moto!

Ndugu Ibrahim Badiri - Mtaalamu wa kikosi
Cha zima moto Manispaa Mtwara-Mikindani
akitoa mafunzo juu ya majanga hususani moto
Baadhi ya wanachuo wa Stella Maris Mtwara University College (STEMMUCO) walipata mafunzo juu ya majanga na hasa juu ya moto.

Katika mhadhara huo uliofanyika chuoni hapo, ndugu Badiri alisema watanzania wengi hawana elimu ya kujiokoa toka kwenye majanga na hivyo basi tatizo kama la moto linapotokea inakuwa vigumu kujiokoa.

Mtaalamu huyo alichanganua aina za moto: moto utokanao na mada za kioganiki, moto utokanao na hitilafu ya umeme, moto utokanao na gesi na moto utokanao na madini na vyuma mbalimbali. Kupambana na moto alisema kila aina ya moto huzimwa kwa kizima moto mahususi.

Moto wa vifaa vya kioganiki huweza kuzimwa kwa maji, poda / unga mkavu maalumu, mchanga
Moto wa umeme huzimwa kwa poda/unga mkavu maalum,
Moto wa gesi, kama ule wa kituo cha mafuta huzimwa kwa mchanga, poda / unga mkavu maalum
Moto wa madini huzimwa kwa poda/ unga mkavu maalumu.

Baadhi ya wana STEMMUCO wakifuatilia mafunzo hayo
Hata hivyo mtaalamu huyo alisema njia hizi hufanyika zaidi kama huduma ya kwanza na pia kwa moto ambao bado haujawa mkubwa, hulenga zaidi moto ambao ndo kwanza unaanza.

Sunday, February 19, 2012

Binadamu hujiumba

A man, as a general rule, owes very little to what he is born with - a man is what he makes of himself.










































Kanuni ya maisha ni kwamba, binadamu hutegemea kwa kiasi kidogo mno kile anachozaliwa nacho, kimsingi binadamu anaamua yeye mwenyewe kuwa anavyotaka yeye mwenyewe.

Alexander Graham Bell.

Mwenyezi Mungu anatuumba mara moja na kutupatia pumzi ya uhai. Pumzi hiyo ya uhai nd'o has maisha yenyewe; hiyo ndo hasa sayansi bado haiwezi kuelezea ni nini hasa. Tunapozaliwa tunakuwa tumekamilika idara zote za miili yetu. Hata hivyo maamuzi ya binadamu awe nani ni suala na maamuzi binafsi lakini muhimu hasa kama tunapenda maisha yetu yawe na maana na kuleta furaha na maana kwa maisha ya watu wengine.
 
Kuvumbua, kuibua, kuja na wazo jipya na kadhalika ndo hasa mambo amabayo tunatakiwa tuyafanye ili kweli maisha yetu yawe na maana kabisa. Kutafuta na kukusanya mali kwa bidii zote (hili ndilo jambo ambalo wengi wetu hulifanya) ni muhimu na vyema kabisa ili kuupiga vita umaskini na uhohehahe lakini pesa isiwe ndio lengo letu kuu; pesa itumike tu kuboresha maisha ya jamii ya wanadamu kote duniani.
 
Hivi leo vijana wengi hapa Tanzania hatufahamu hasa nini maana ya maisha yetu tunadhani lengo la maisha ni kusaka pesa tu "mkwanja" hasa tukikutana na maneno na ushawishi wa vijana wa Marekani ama bara Ulaya, "Jitahidi kupata mali maishani ama kufani". Kamwe hili si lengo la maisha, jambo muhimu tukumbuke kila mwanadamu ana nafasi ya kujiumba na kuwa anavyotaka awe! 

Friday, February 3, 2012

Maneno ya kujenga na kuimarisha zaidi

Maneno ya kujenga na kutia moyo kwa vijana na wengine wote wenye nia ya kujiendeleza yanapatikana katika mtandao wa Advance Africa ambao hutoa taarifa ya nafasi nyingi za masomo ya juu zaidi. Kwa wanaopenda kujifunza juu ya nafasi hizo wasome hapa


If you think you are beaten, you are.
If you think you dare not, you don't.
If you like to win but think you can't,
It's almost a cinch you won't.

If you think you'll lose, you're lost.
For out in the world we find

Success begins with a fellow's will.
It's all in the state of mind.

If you think you are out classed, you are.
You've got to think high to rise.
You've got to be sure of your-self before
You can ever win the prize.

Life's battles don't always go
To the stronger or faster man.

But sooner or later, the man who wins
Is the man who thinks he can.

C. W. Longenecker.


        "When one door closes another door opens; but we so often look so long and so regretfully upon the
                                      closed door, that we do not see the ones which open for us."

 Alexander Graham Bell.






Tuesday, January 31, 2012

Mgomo wa madaktari Tanzania

Baadhi ya matabibu na wauguzi wa hospitali ya
Muhimbili wakijadiliana mambo kadhaa picha kwa
hisani ya rfi Kiswahili

















Tunawapa pole wote wanaoathiriwa na mgomo huu!

Binadamu, kulingana na biolojia tunayoifahamu sisi wanadamu hivi leo, ndio mnyama mwenye ubongo mkubwa na wenye kufanya kazi vyema zaidi kuliko wanyama wengine. Bila shaka ukweli huu upo kwa lengo mahususi na si kwa bahati mbaya.

Binadamu mara tu anapozaliwa ana jukumu muhimu kwa dunia hii, hiyo ni moja kati ya sababu nyeti za uwepo wake hapa duniani - la raison d'être. Hali hiyo ni lazima kwa kila kilicho!

Hivyo basi, lazima tujiulize hivi nini hasa sababu ya uwepo na wajibu wa serikali kwa wananchi wake, ikiwa ni pamoja na madaktari? Nini sababu ya uwepo na wajibu wa madaktari hapa duniani?

Bila shaka kwa kutumia ubongo wenye uwezo mkubwa wa kupambanua magumu, tunaweza kupata suluhu ya tatizo hili...  

Sunday, January 29, 2012

KUSOMA VITABU KWAJENGA SANA


Hatimaye nimemaliza kusoma  "The Innocent Man"  cha John Grisham

Kitabu hiki kinajadili mambo mengi ya msingi mno kwa maisha ya binadamu. Mawili kati ya hayo ni; mosi jinsi ambavyo mfumo wa sheria, niruhusu kusema duniani, unavyoweza kuwa na mapungufu ya kutoa haki kwa binadamu, pili jinsi ambavyo watoa huduma wengine walivyo makini kuona haki inadhihirika na binadamu anatendewa haki katika mfumo wa sheria. Jambo la pili limenifurahisha sana!

Ni kitabu kizuri mno ambacho kinaweza kuamsha na kujenga moyo na usawasha wa kutenda mema katika jamii. Moyo wa kuona ukweli ukipatikana unaweza kuwa katika nyanja anuwai ama zote za maisha ya binadamu. Asante ndugu Grisham kwa kutushirikisha mawazo mazuri kabisa, huu ndo uzuri wa ubinadamu! 

Tuesday, January 17, 2012

DAWA BANDIA ZA MALARIA NI KIFO KWA AFRIKA...

Tabibu akitoa huduma kwa Mtoto mgonjwa wa malaria













Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la bidhaa nyingi bandia... karibu kila kitu unachonunua ni kama kuna mbadala wake ambao ni bandia. Hali hii imeonekana kuwa ni kitu cha kawaida na hali inayokubalika kimaisha. Hali hii la hasha haijakubalika kisheria, ambapo kuna nyaraka rasmi kwamba kuanzia sasa tuwe na bidhaa bandia, lakini kulingana na jinsi mambo yanavyokwenda basi tunaweza kusema ni hali iliyokubalika. Bidhaa bandia nyingi zinasemekana kutoka nchi za mashariki zinazoendelea kiuchumi.

Inasemekana kuwa katika nchi hizo za mashariki hususani Uchina; unaweza kutengenezewa bidhaa ya aina yoyote kulingana na uwezo wako wa kifedha. Tatizo hili linasababishwa na wafanyabiashara wenye uchu wa kujitajirisha haraka... utajiri si jambo baya ila utajiri kwa njia isiyo sahihi ni makosa. Lazima mambo haya ya bidhaa BANDIA TUYAKEMEE, na katika afya ni hatari zaidi.

Dawa bandia kwa hakika ni kifo kwa bara la Afrika, takwimu za shirika la afya duniani WHO linaonyesha kuwa Malaria ndo ugonjwa unaoongoza vifo vya watu wengi zaidi barani humo, bara linawekwa kwenye orodha za umasikini duniani. Kuzuka kwa wimbi la dawa bandia za ugonjwa huo unaoongoza kwa vifo barani ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa waafrika hususani wale wenye kipato duni; sehemu kubwa ya Waafrika. Jambo la kusikitisha hapa ni kuwa hukumu hii inatolewa na ndugu zetu wa barani humu.

Wanaoingiza nchi dawa bandia za Malaria ni ndugu zetu waafrika, kwa hili tusimame pamoja tuwaambie acheni kuua ndugu zetu- wafanyabiashara wanaoingiza, wanaoagiza dawa bandia hawana utu na ni wauaji - waache kufanya hivyo!

Taarifa hizi zinapatikana pia kwenye wavuti wa Bbc Kiswahili

MZEE JANGALA AONGELEA SANAA

  Na Mwandishi wa BASATA
 Msanii Nguli wa sanaa za maonesho, Bakari Kassim
Mbelemba (Mzee Jangala) aikizungumza na
wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa


Msanii nguli wa Sanaa za Maonesho, Bakari Kassim Mbelemba (Mzee Jangala) amesema kuwa programu ya Jukwaa la Sanaa inayoendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni chuo tosha kwa wasanii katika kuwapa elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali ya sekta ya Sanaa.

Akizungumza wiki hii, kwenye programu hiyo katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharif Shamba, Jangala alisema kuwa, Jukwaa la Sanaa ni jambo la kujivunia na ni chachu ya kukua kwa Sanaa.

“Jukwaa la Sanaa ni programu inayonifanya nithubutu kusema, sasa Sanaa ni kazi, maana kazi yoyote ili ifanywe kwa ufanisi inahitaji elimu, uratibu na mwongozo, hivyo wasanii tuitumie fursa hii adimu” Jangala alisema.

Aliongeza kuwa, programu hii imekuwa ikiwaleta wataalam na wadau mbalimbali wenye uzoefu katika sekta ya Sanaa hivyo, kwa wasanii ambao wamekuwa wakihudhuria toka mwanzo wamepata mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Alisisitiza kuwa, Sanaa inabadilika na kumezwa na teknolojia mpya zinazokuwa zinajitokeza hivyo, ni lazima wasanii wajenge utamaduni wa kutafuta maarifa mapya na kuwa wabunifu huku wakizingatia maadili ya kitanzania.

Kuhusu wasanii kulewa umaarufu na sifa, alishauri kuwa ni vema wakabadilika na kufanya kazi zao kwa bidii na ubunifu zaidi kwani, sifa ya msanii inakuja yenyewe kutokana na kazi anazozalisha na kupeleka kwa jamii inayomzunguka.

“Sifa ya mpishi hutolewa na mlaji, kwa hiyo wasanii wanapotengeneza kazi zao wasijisifu wenyewe bali wasubili kusifiwa na msikilizaji au mtazamaji” alishauri Mzee Jangala.

Alizungumzia pia suala la wasanii kutegemea vipaji tu pasipo kuingia darasani na kusema kuwa hilo haliwezi kukuza sekta ya sanaa na badala yake tutakuwa na kazi zinazoandaliwa kwa msukumo wa soko na si taaluma ya Sanaa

“Wasanii ni lazima watambue kuwa, mbolea ya kipaji chochote kile ni elimu. Ni vigumu sana kutegemea kipaji tu pasipo kukipalilia kwa taaluma ya sanaa husika”

Kwa upande wake, kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa, Vivian Nsao Shalua alishauri wasanii kulitumia Jukwaa la Sanaa ili kuzijua sheria, taratibu na mbinu mbalimbali zitakazo waongoza katika shughuli zao za Sanaa.

Wednesday, January 11, 2012

MAVAZI YA AIBU YALALAMIKIWA

Picha toka mtandaoni
imepakuliwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=wxBwsU9u6vw
Picha kwa hisani ya google
                                                                                                                                                          
Wafaransa wana msemo wao, "L'habit ne fait pas le moine" unaotafsiriwa kwa kiingereza "Clothes don't make the man" ama kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, "si mavazi yanayofanya mtu kuwa mtu".



Hapo kale tumesoma katika historia ya kuwa wazazi wetu wa kale walijisitiri tu sehemu zao za utupu na kuwa hiyo ilikuwa ni namna yao ya maisha na hakukuwa na shida yoyote. Unaweza pia kuona katika filamu ya "the gods must be crazy " Mavazi ni kwaajili ya binadamu na si vinginevyo.

Hivi karibuni jamii zetu zimekuwa na muingiliano na jamii zingine na zimepiga hatua kubwa katika nyanja anuwai ikiwa ni pamoja na kwenye suala la mavazi. Binadamu ameona ni vyema akajivika mavazi yenye heshima na yenye kumpendeza.






Picha hii kwa hisani ya
blogu la haki za binadamu
Lakini muingiliano huo haukuishia tu kwenye mambo mazuri ya kujifunza kumekuwa na mambo yasiyo ya kupendeza kwa jamii. Kuna aina ya mavazi ambayo humuacha kiumbe akiwa karibu nusu uchi, ni kweli kwamba si mavazi yanayomfanya mtu kuwa mtu, lakini ni vyema kukubaliana na kile jamii inachotaka. Jamii ya leo Tanzania inahitaji mavazi yenye kusitiri vyema maungo, basi natufanye hivyo.

Kutoka Dodoma Mwandishi wa Tanzania Daima anaandika zaidi

BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wamesema kuwa wanakerwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wanaovalia mavazi ambayo yanaonyesha maungo yao na hivyo kuleta aibu kwa jamii.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, walisema kuwa tabia za wasomi hao haziendani na jinsi jamii inavyowachukulia kwani badala ya wao kuwa kioo kwa jamii wamegeuka kuwa chukizo.

Mmoja wa wakazi hao, Twaha Kivale, alisema kuwa kwa sasa mavazi ambayo yanavaliwa na wanavyuo hususan wa kike katika mkoa wa Dodoma ni ya aibu na yanaleta picha mbaya kwa wadogo wao wa elimu ya chini kama vile shule za msingi na sekondari.

“Tunategemea kuwaona wasomi wakiwa na tabia njema lakini cha kushangaza wasomi hao wanavaa nguo mbaya ambazo zinaonyesha maumbile yao ya ndani, hii ni sawa na kutembea uchi bila aibu tena mchana.

Tunashindwa kutofautisha wasomi na makahaba kutokana na mambo ambayo yanafanyika, kama kweli wasomi ambao tunawategemea kuongoza nchi wanavaa hivi kinyume kabisa na maadili yetu kuna maana gani ya kuelimika,” alihoji Kivalle.

Naye, mchungaji Evance Lucas wa Kanisa la EAGT, Siloam Ipagala, akizungumzia suala hilo alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wanafunzi wa kike kuvaa nguo hizo ni mpango kamili wa shetani.

Alisema kuwa kwa sasa shetani anawatumia sana watu ambao wanaonekana kuwa wasomi na wasipoweza kujitambua ni wazi kuwa watajikuta wakishindwa kufikia malengo ambayo wameyakusidia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, katika hilo alisema kuwa hata yeye anakerwa na tabia hiyo ambayo kimsingi inadhalilisha utu wa mwanamke.

Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuwa mji wa Dodoma una vyuo vikuu vingi na kuonekana kama sehemu ya maendeleo lakini kwa sasa hali ni mbaya kwani zimekuwepo tabia ambazo zinatia aibu katika jamii.

Hata hivyo alisema ili kuondokana na tabia hiyo kunatakiwa kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na serikali ili kuhakikisha tabia ya namna hiyo inakomeshwa.

Naye mwanachuo mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye hakutaka kutaja jina lake, alipoulizwa alisema kuwa mavazi ni hiari ya mtu na kuongeza kuwa licha ya wananchi kulalamika bado wataona mambo mengi kwani kila mtu ana uhuru wa kuvaa atakavyo.

Kwa sasa katika mkoa wa Dodoma kuna vyuo vya elimu ya juu vya Udom, St.Johns, Chuo cha Mipango na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).










Tuesday, January 10, 2012

BASATA YAONYA MAPROMOTA WABABAISHAJI

Na Mwandishi wa BASATA
Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA, Vivian Nsao Shalua
   akizungumza na wadau wa Sanaa katika Jukwa la Sanaa linalofanyika
kila wiki makao makuu ya Baraza hilo. Kulia ni Afisa Habari wa
BASATA Aristide Kwizela.


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaonya wakuzaji sanaa nchini kuacha mara moja ubabaishaji wanapokuwa wanaendesha matukio na matamasha mbalimbali ya Sanaa.

Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa Baraza hilo, Vivian Nsao Shalua wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharifu Shamba.

Shalua alisema kuwa, Mapromota wamekuwa wakiwarubuni wasanii kwa kuwafanyisha kazi zisizo na mikataba huku wao wakinufaika na kuwaacha wasanii wakishindwa kujikwamua kimaisha.

“Utaratibu uliopo sasa kila mdau yeyote anapoandaa tamasha au tukio lolote linalohusisha wasanii lazima aje na mikataba na wasanii hao, aoneshe uwezo wake kifedha katika kuendesha tukio lakini pia awe na kamati inayoeleweka ya uendeshaji” alisisitiza Shalua.

Aidha, aliongeza kuwa, kumekuwa na ukiukwaji kanuni na taratibu za uendeshaji matukio hayo ambapo Baraza limekuwa likiwapa onyo na kuwafungia wahusika lakini akasisitiza kuwa, njia pekee ya kuepuka hali hii ni kwa mapromota kufuata taratibu zilizopo.

Akizungumzia kuhusu suala la mikataba, aliwataka Wasanii kuhakikisha hawashiriki tukio au onyesho bila kuwa na mkataba na waandaaji kwani hali hiyo inawafanya wadhulumiwe na kushindwa kudai haki zao kwa mujibu wa makubaliano.

“Ni lazima sasa wasanii wadai mikataba. Sisi tunawabana wakuzaji sanaa (mapromota) kuambatanisha mikataba yao kabla hatujawapa kibali lakini lazima na wasanii waoneshe wajibu wao kwa kudai mikataba na kutoshiriki maonyesho bila makubaliano ya maandishi” alionya Shalua.

Alisisitiza kuwa, Baraza litakuwa makini katika kufuatilia wadau wanaopewa vibali vya kuendesha matamasha na matukio mbalimbali ya Sanaa na mara taratibu na kanuni zitakapokiukwa halitasita kuchukua hatua za makusudi.

Wednesday, January 4, 2012

Masomo Zaidi...?

Elimu haina mwisho ndivyo usemavyo mmoja wa semi za wahenga wetu.
Kujiendeleza kielimu ni muhimu kabisa kwa wale wenye kupenda kufanya hivyo.

Mtandao wa Advance Africa lengo lao kuu ni kufanya hivyo; hebu sasa wale wenye moyo na nia ya kufanya hivyo wasome zaidi hapa. Bonyeza hapa

Mbinu za kazi tofauti malengo yaleyale - safi sana!