Tabibu akitoa huduma kwa Mtoto mgonjwa wa malaria |
Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la bidhaa nyingi bandia... karibu kila kitu unachonunua ni kama kuna mbadala wake ambao ni bandia. Hali hii imeonekana kuwa ni kitu cha kawaida na hali inayokubalika kimaisha. Hali hii la hasha haijakubalika kisheria, ambapo kuna nyaraka rasmi kwamba kuanzia sasa tuwe na bidhaa bandia, lakini kulingana na jinsi mambo yanavyokwenda basi tunaweza kusema ni hali iliyokubalika. Bidhaa bandia nyingi zinasemekana kutoka nchi za mashariki zinazoendelea kiuchumi.
Inasemekana kuwa katika nchi hizo za mashariki hususani Uchina; unaweza kutengenezewa bidhaa ya aina yoyote kulingana na uwezo wako wa kifedha. Tatizo hili linasababishwa na wafanyabiashara wenye uchu wa kujitajirisha haraka... utajiri si jambo baya ila utajiri kwa njia isiyo sahihi ni makosa. Lazima mambo haya ya bidhaa BANDIA TUYAKEMEE, na katika afya ni hatari zaidi.
Dawa bandia kwa hakika ni kifo kwa bara la Afrika, takwimu za shirika la afya duniani WHO linaonyesha kuwa Malaria ndo ugonjwa unaoongoza vifo vya watu wengi zaidi barani humo, bara linawekwa kwenye orodha za umasikini duniani. Kuzuka kwa wimbi la dawa bandia za ugonjwa huo unaoongoza kwa vifo barani ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa waafrika hususani wale wenye kipato duni; sehemu kubwa ya Waafrika. Jambo la kusikitisha hapa ni kuwa hukumu hii inatolewa na ndugu zetu wa barani humu.
Wanaoingiza nchi dawa bandia za Malaria ni ndugu zetu waafrika, kwa hili tusimame pamoja tuwaambie acheni kuua ndugu zetu- wafanyabiashara wanaoingiza, wanaoagiza dawa bandia hawana utu na ni wauaji - waache kufanya hivyo!
Taarifa hizi zinapatikana pia kwenye wavuti wa Bbc Kiswahili