Picha kwa hisani ya blogu ya udadisi |
Kila nchi duniani hutambulika kwa mambo kadha wa kadha; Japan wanatambulika kwa ubobeaji wao kwenye teknolojia, Marekani wanatabulika katika kwa nguvu zao za kiuchumi, kisiasa, nk. Tanzania, pamoja na kutambulika kupitia mlima Kilimanjaro, mbuga nzuri za wanyama kama Serengeti, historia nzuri na kuvutia kupitia visiwa vya Zanzibar hutambulika pia kupitia Kiswahili.
Mlima Kilimanjaro Picha hisani ya wwf |
Nchi nyingi duniani huongea Kiswahili, hata hivyo Tanzania inaendelea kutambulika kuwa kiranja wa lugha hii adhimu. lakini je, lugha hii ina fursa zozote? Na je, watanzania wanazitumia vipi fursa hizo na ni kwa kiasi gani nchi ina nufaikanazo? Na jamii ya wanazuoni wana mchango upi katika ukuzaji wa lugha hii? Hebu tupitie sehemu ya hotuba ya waziri mkuu ndugu Mizengo Peter Pinda kama ilivyoandaliwa na blogu ya udadisi:
IV UENDELEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
22. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge walipokea na kujadili pamoja na mambo mengine Maazimio mbalimbali. Niruhusu nirejee Azimio lililonigusa sana kuhusu Uanzishaji wa Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Awali, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Chama cha Kiswahili Tanzania (CHAKITA) na Wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuwa na Mpango wa Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Hata hivyo, Baraza hilo halikuanzishwa, badala yake ikapendekezwa kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Azimio la Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo ya Lugha ya Kiswahili tumelipitisha katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana mliyoitoa.....