Sunday, April 22, 2012

JE UMEANDIKA NINI?

Kipanya kikitoa huduma ya usafiri kwa umma. Picha toka blogu

















Hivi karibuni nilikuwa kwenye basi dogo la usafiri wa umma daladala; toka Mtwara kwenda Mikindani. Usafiri maarufu kwa daladala za Mtwara ni vipanya; vibasi vidogo vidogo ambavyo nadhani vingi ni mitumba toka Dar es Salaam. Vipanya vingi mjini hapa vimechoka na vinakwenda kwa mwendo wa kusuasua vinapokuwa barabarani. Hakuna mabasi makubwa mithili ya yale ya Mwenge Posta kwa Dar es Salaam, pamoja na hayo ule udaladala upo pale pale. Daladala ama vipanya hivi vinajaza kama ilivyo ada ya daladala sehemu nyingi Tanzania. Hapo juu nimegusia Mikindani; huu ni mji mkongwe, mji wa zamani ambao kwa bahati mbaya umesahaulika, hauendelezwi tena. Pengine kwa kuwa neema ya gesi mjini hapa imefunguliwa basi mambo huenda yakawa sawia  kwa mji huu wa kihistoria.Sasa nirejee kwenye mada ya makala hii.

Mikindani chakavu, picha na blobu ya wadau wa safari


















Katika kipanya nilichokuwa abiria, utakumbuka kuwa kwenye daladala huwa kuna mada nyingi, kondakta wetu alikuwa muongeaji kupindukia. Kodakta, konda ndivyo wanavyofahamika zaidi, huyu hatofautiani na wengi walio mikoa mingine; ni kijana aliyevalia sare chakavu ya kazi na ambapo kama walivyo wengi wao suruali yake ilikuwa ikining'inia zaiki kuliko kuvaliwa, namna hiyo ya kuvalia huitwa na vijana wa leo "kata k". Koda yule katika utani na abiria mmoja ndani ya daladala letu, ambaye nadhani ni shwahiba wake kwa jinsi walivyokuwa wameshibana kwa simulizi za kutosha bila shaka kwa lengo la kufupisha safari. Basi yule konda alimtupia rafiki yake swali ambalo hasa nd'o linabeba kichwa habari cha mada hii, hivi wewe toka umalize shule ya msingi umeandika chochote kweli?
Hivi wewe umeandika chochote kweli? Kwa hakika hili ni swali dogo sana na lategemea uzito ambao mtu ataamua kulitilia mkazo. Lakini ni jambo kubwa na muhimu sana pia. Mtu anayeandika kwa kawaida ni mtu anayesoma pia. Kwa hivi swali la konda lauliza pia, je, umesoma nini hivi karibuni? Sina hakika kama yeye mwenyewe ameandika ama amesoma chochote hivi karibuni. Tafiti na ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa moyo na tabia ya kujisomea kwa watu wengi imepotea ama inapotea kwa kasi kubwa . Hapo zamani ilikuwa ni lazima kuandika barua ili kujua nini kinaendelea nyumbani kwa wazazi wako walio mbali nawe, siku hizi inatosha kuweka salio katika simu ya mkoni, simu hizo karibu kila mmoja anayo yake; hii ni moja ya sekta ambazo Tanzania imepiga hatua kubwa sana, na kuanza kuongea. Anayejua kuandika ataongea kama asiyejua kuandika halikadhalika. Kukua kwa tekinolojia ya habari nako kwa kiasi kikubwa kinachangia kushuka kwa moyo wa kuandika na kusoma kama hapo awali. Hivi leo hata zile huduma za kibenki ambazo humlazimu mtumiaji kuandika japo sentensi mbili tatu zinafanywa kwa wepesi na urahisi kabisa kupitia simu ya mkononi hata na mtu asiyejua kusoma na kuandika ila tu masuala ya lazima hususani yahusuyo pesa. Maendeleo ya tekinolojia ya habari ni muhimu lakini tuendelee kujifunza kusoma na kuandika.

Hivi wewe umeandika chochote toka uhitimu elimu ya msingi, sekondari, chuo kikuu, toka upate udaktari wa falsafa?Swali hili la konda mhitimu wa darasa la saba lamgusa kila mmoja wetu toka wale wa shule ya msingi hadi madaktari wasiotimu watu ila falsafa. Nchini Tanzania pamoja na juhudi nyingi za wasomi wetu mahitaji ya vitabu vya mafunzo mbalimbali bado ni vichache; tunaendelea kutumia vitabu toka ng'ambo. Hili si jambo jema hata chembe.

Wito kwa kila mmoja wetu tuongeze muda wa kusoma vitabu zaidi na kufanya hivyo tutapata hamu na ujumbe wa kuandika chochote kitu kwa lengo la kuielimisha jamii, ambalo ni jukumu la kila mmoja wetu.

No comments:

Post a Comment