Ndugu John Pombe Magufuli |
Majuma machache tu toka
kupata mkataba toka kwa wananchi wa Tanzania kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi
cha miaka mitano, na ikiwa ni muda mfupi tu kisha kuapishwa kwake kuwatumikia
wananchi, ndugu John Pombe Joseph Magufuli amefanya mambo kadhaa tofauti na
ilivyokuwa imezoeleka huko nyuma.
Alichofanya ndugu JPJ
Magufuli hakikinzani na katiba ya Jamhuri ya Muungano, na zaidi si kinyume na
asili ya ubinadamu na kanuni za kimaumbile kwani hata Heraclitus mwanafalsafa
wa kale wa Ugiriki anasema hakuna jambo la kudumu ila mabadiliko. Kwahiyo
alichofanya kinaendena na kanuni za kifalsafa, ubinadamu na kanuni za
kimaumbile; kila binadamu ni tofauti na wa kipekee mno na hivyo kila binadamu
ana uwezo wa kufanya mambo ya kipekee na tofauti na wengine wote, hiyo ndiyo hulka
sahihi ya binadamu anapokuwa na nafasi ya kujitawala.
Pamoja na mambo mengine
aliyoyafanya ndugu rais, hapa hatulengi kuyaorodhesha, kusitisha safari ambazo
hazina ulazima wala faida kubwa kwa taifa kwa viongozi wa serikali, kufanya
mabadiliko ya matumizi ya pesa iliyokuwa imetengwa kwa sherehe za kuwapongeza
wabunge na kwa kuzinduliwa rasmi kwa bunge la Tanzania. Mambo yote haya
yanalenga kuongeza nidhamu ya matumizi ya pesa; hii ni stadi muhimu ambayo kila
mmoja wetu inafaa ajifunze. Aidha kusitisha shamrashamra zilizozoeleka za 09/12
na badala yake kusheherekea siku hiyo ya uhuru wa Tanganyika kwa kushiriki
kufanya usafi maeneo mbali mbali tunayoishi na kufanyia kazi ni jambo jema
hasa. Ni dhahiri kuwa kipindu pindu hakitakwisha kwa usafi huo wa siku moja
lakini agizo hilo limelenga mbali zaidi. Agizo hilo la ndugu rais linalenga
mabadiliko ya tabia: jambo muhimu kwa mafanikio maishani.
Kasi ya utendaji kazi
aliyoanza nayo rais Magufuli inapendeza na bila shaka tutarajie mabadiliko
zaidi. Hata hivyo analazimika kuwa makini zaidi atakapokuwa “akifanya usajiri
wa baraza lake la mawaziri” kwa lugha ya kisoka zaidi timu yake inafaa kuwa na
wachezaji wenye viwango vya juu na wenye sifa mithili ya wachezaji wa kulipwa
kama ilivyo kwa Samatta na Ulimwengu kwa TP Mazembe, Maguli kwa Stand Utd,
Bocco kwa Azam, Martial, Roney kwa Man Utd, Ronaldo kwa Real Madrid, Messi,
Neymar na Suarez kwa Barcelona na kadhalika na kadhalika.
Wakati wapenda
maendeleo wengi wanaendelea kufurahia hatua za uchapakazi ndugu rais na hivyo
kutoa pongezi kemkem kwake, nasi pia twaungana nao kumtia shime zaidi ndugu
John Magufuli aendelee kufanya vyema na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu amlinde
na kumuongoza zaidi. Hata hivyo tufahamu kuwa ndugu rais anatimiza wajibu wake
kama kiongozi mkuu wa nchi mithili ya baba anayewajibika vyema kwa familia
yake. Baba anayelipa ada kuwasomesha watoto wake katika shule ya viwango vya
juu, anapotoa mahitaji stahiki kwa familia yake na kadhalika hapewi sifa na
wala hapaswi kujisifu kwa vile anatimiza wajibu wake impasavyo. Pengine mazoea
ya kuona baba wa jirani akikosa kuwajibika impasavyo kwa familia yake ndicho
kinachosababisha kuona kuwa baba mtimiza wajibu anafanya mambo yasiyokuwa ya
kawaida. Hivyo tufahamu na tumpatie ushirikiano ndugu rais aendelee kutimiza
wajibu wake vizuri zaidi na zaidi.
Jaji Mstaafu Warioba |
Wito wetu katika Makala
hii/haya kwa rais Magufuli ni juu ya ama kujenga ama kuimarisha taasisi zetu.
Taasisi zetu za uongozi inafaa ziwe imara na zenye mamlaka yaliyojitosheleza,
zikiwa imara basi kiongozi yeyote akipata mkataba kuongoza nchi atalazimika
kufanya kazi vizuri ama kwa utashi wake ama kwa kulazimishwa na taasisi hizo.
Bila kuwa na taasisi imara utendaji kazi na uongozi utategemea hisani na hulka
ya kiongozi aingiaye madarakani. Kiongozi mchapakazi na mzalendo “akiukwaa”
mkataba kuongoza nchi mambo yatakwenda vyema na wanachi tutaona kama
tunafanyiwa hisani ila hali akiingia kiongozi mwenye uzalendo hafifu na mwenyekujipenda
yeye mwenyewe zaidi basi katika nchi tutashuhudia madudu. Hivyo basi ili
tuepuke kucheza bahati nasibu ya uongozi ni vyema basi tukawa na taasisi imara.
Taasisi hizo imara tunaweza kuzipata kwenye mabadiliko ya katiba yenye
kushirikisha na kukubaliwa na wananchi walio wengi.
Bahati njema mabadiliko
ya katiba yanayokubaliwa na wananchi tunayo kwenye chapisho la ‘katiba ya
Warioba.’ Hivyo basi ndugu rais tunakuomba uturejeshee “katiba ya Warioba”
ambayo itatufaa sana kwa dira ya taifa letu kwa miaka mingi ijayo.