Friday, November 20, 2015

WANASIASA KAMA WANANDOA!!!

Image by google
Makundi haya mawili yote hula kiapo cha utii na uaminifu mbele za watu na Mungu lakini bado wanachakachua!!!

WANANDOA:
Image by google

Watu wawili kwa kawaida mtu mme na mtu mke wanapopendana na kukubaliana kuishi pamoja hulazimika kuweka wazi suala hilo mbele ya umma wa wanajamii wanaoishi nao. Kwa kawaida watu hawa hula kiapo, huwekeana ahadi kuwa watakuwa waaminifu baina yao na kawaida huomba msaada wa Mungu awawezeshe kuwa waaminifu katika kiapo chao. Hufanya hivyo na kuahidi kuwa wavumilifu katika jua na mvua, afya na ugonjwa, mali na kutokuwa na mali hadi hapo kifo kitakapowatenganisha.

Hapa hatutaki kuangalia kama watu wetu wanakuwa kweli wameandaliwa na kama wanajua nini maana ya kuishi katika ndoa. Bila shaka suala hili tutalijadili mara nyingine kwa marefu na mapana yake stahiki.

WANASIASA:

Watu waume na wake walioamua kuingia kwenye shuguli za kisiasa hulazimika, kama ilivyo kwa wanandoa, kula kiapo na kuahidi kulinda na kutumikia kwa lengo la kuboresha maisha ya watu wetu. Wanasiasa pia husikika wakisema na tena kwa kutumia vitabu vitakatifu kuwa kwa akili zao timamu watailinda katiba ya Jamhuri ya Muungano na kuwa wanaomba Mungu awasaidie katika utekelezaji huo.
Image by google

Kwa upande wa siasa nafahamu pia kuwa si wanasiasa wote wanaofahamu uzito na umuhimu wa kazi hii ya kitumishi. Kama asemavyo mwanafalsafa nguli John Locke kwamba mwanasiasa mzuri ni yule anayefahamu moyoni mwake kuwa kazi hiyo ni mkataba baina ya mwanasiasa na wananchi.

MADUDU

Pamoja na kula viapo wanandoa huvikiuka viapo vyao na kuvunja ahadi zao za ndoa na kuanzisha nyumba ndogo ambazo ni kinyume na ahadi zao za ndoa. Kama ilivyo kwa wanandoa, wanasiasa wetu wengi pia hukiuka na kuvunja ahadi na viapo vyao kwa kuchakachua rasilimali zetu na kushiriki kwenye ufisadi na wizi mkubwa mkubwa tu. Mfano wa uchakachuzi hapa ni pamoja na kushiriki katika ESCROW, EPA, RICHMOND na wizi mwingi unaowakesesha wananchi haki zao. Hivyo basi wanasiasa na wanandoa wote kwa nafasi zao hufanya madudu na kukiuka viapo vyao.

No comments:

Post a Comment