Picha hii inaashiria mambo mengi na moja kati ya hayo ni uchafu. Hii ni sehemu rasmi ya kuhifadhia uchafu karibu na soko kuu mjini Mtwara. Sokoni, kama inavyofahamika, ni sehemu muhimu kwa binadamu kujipatia mahitaji yake muhimu. Soko kwa hakika ni eneo la lazima sana kwa maisha ya binadamu. Pamoja na shughuli zingine muhimu kwa mwanadamu; kula (chakula) ni moja kati ya shughuli za muhimu mno kwa binadamu. Katika hali ya kawaida binadamu ana hitaji kupata chakula kila uchao.
Chakula cha binadamu, hususani mijini, hupatikana sokoni. Kwa Mtwara hupatikana karibu kabisa na jaa hili kubwa la taka.Chakula huingia mwilini mwa binadamu na kuleta manufaa makubwa. Ili chakula kilete manufaa ni lazima kiwe katika hali ya usafi, vinginevyo kitaleta madhara makubwa kwa kiumbe huyu mwenye uwezo mkubwa wa fikra na mawazo mapya. Kwanini binadamu huyu, hususani wa Mtwara asitafute mawazo mapya ya namna kuhifadhi taka mbali na mahali pa kupata mahitaji yake ya kila siku?
Je, ni Mtwara tu ndo jaa la taka li karibu vile na soko? Nini kifanyike? Wataalamu wa mazingira, miji safi, mipango miji n.k watupatie mwongozo...