Tuesday, December 31, 2013

SIKU YA MWISHO YA MWAKA - UJUMBE KWA VIJANA

Hatimaye ni hakika sasa kila binadamu hai duniani na pia wafu wameongeza mwaka mmoja toka kuzaliwa. Binadamu wote ila tu waliozaliwa tarehe 29 Feburuari. Ni hao tu ndo wenye miadi na siku yao ya kuzaliwa kila baada ya miaka minne. Robo nne zinapotengeneza kitu kimoja kizima. (Mwaka mfupi una siku mia tatu sitini na tano na robo {365¼} na mwaka mrefu siku mia tatu sitini na sita {366})

Ukweli huu wa maisha unawakilisha mambo yote duniani kila jambo limepata fursa ya kukamilika; miezi yote imepata mzunguko wake, nyakati zote zimefikiwa, majuma yote yamekamilika, saa zote, dakika zote, sekunde zote na kila jambo lenye kutegemea mzunguko wa mwaka leo linakamilika.

Kupitia mzunguko na kukamilika kwa mwaka ni jambo la kujiuliza pia sisi wenyewe. Binadamu pia ana mabadiliko yake; yale ya kibaiolojia, seli mpya kuzaliwa na kuukuu kupotea, kutumia / kutumika sawa sawa kwa ubongo: kujenga fikra mpya n.k. Kumbe siku hii ya mwisho ni siku ya tathmini kwa yaliojiri maisha mwetu. Mimi Martin, Amina,  nimefanya jambo lipi la maana kwa maisha yangu na binadamu wenzangu? Nimepanda miti? Nimegundua jambo jipya muhimu kwa binadamu? Nimeandika kitabu cha maarifa na manufaa kwa wanadamu wenzangu? Nimefanya jambo lenye kulinda uhai wa binadamu? Nimefanya nini kwa nchi yangu, kwa dunia yetu? Naam ni lazima kujiuliza maswali haya, kila mmoja ajiulize kwa namna yake mwenyewe. Kila mmoja wetu afanye kile mwafalsa wa Ugiriki ya kale Socrates anavyopendekeza “maisha yasiyo na tathmini hayana tija” {tafsiri yangu isiyo rasmi}. Tathmini hizi zinatuhusu binadamu wote, viongozi wan chi duniani wahusika kwa kiasi kikubwa.

Wanasiasa wana jukumu kubwa la kuongoza nchi zao. Wanasiasa wazuri wanaongoza vyema wanasiasa wabovu wanaongoza hovyo. Watu hawa wana wajibu mkubwa zaidi kwa wananchi wenzao. Wana wajibu wa kuongoza nchi zao na kuhakikisha wananchi walio wengi wananufaika na mali asilia nchini mwao. Rais wa Marekani, mmoja kati ya mifano mizuri mwaka huu, amepigania kuboresha maisha ya Wamarekani wengi wa kawaida kwa kuboresha huduma zao za afya; moja kati ya mahitaji na haki muhimu ya binadamu. Kufanikisha jambo hilo kulihitaji ujasiri mkuu. Kwenye mlolongo huo wa siasa kuna mengi yamefanyika kote duniani; masuala anuwai mazuri kwa mabaya. Nchi nyingi hususani barani Afrika zimekumbwa na shida za kisiasa.

Nchini Mali kulitokea uasi ambao ulivuruga maisha na ustaarabu wa siku nyingi wa moja kati nchi zenye historia yenye kubeba bara lenye nchi nyingi zaidi duniani. Afrika ya Kati maisha bado hayajarejea hali ya kawaida kufuatia uroho wa mamlaka na dhambi ya ubaguzi inayoendelea kuwatafuna wanasiasa wa nchi hiyo yenye kubeba sawia jina lake na mahali ilipo. Misri, nchi yenye utajiri wa historia na kumbukumbu mahususi za maendeleo ya kale haikubaki salama na bado kunaendelea kuwa na chokochoko baina ya makundi hasimu. Jamhuri ya kidemokrasiaya Kongo iliendelea kuwa kwenye hali ya sitofahamu hususani mashariki mwa nchi hiyo tajiri kwa maliasili na ukubwa wa eneo barani. Ni dhahiri kuwa kila nchi ilikumbana na masuala anuwai ya kupendeza na yasiyo ya kuvutia, changamoto na fursa za kimaendeleo. Nchi kadhaa zimeendelea kusheherekea jubilei za miaka hamsini na zaidi. Tanzania na watanzania kwa mara ya kwanza walipata fursa ya kuchangia mchakato wa kuandaa sheria mama za nchi yao ama nzuri zaidi makabrasha ambayo ni mali ya wananchi, mkataba baina ya wananchi wa viongozi. Mkataba huo maarufu zaidi  katiba ni muongozo wa namna viongozi: watu ambao hutoka miongoni mwa wananchi na hukabidhiwa mamlaka ya/ na wananchi, ili waufahamu na waelewe ni namna ipi inawapasa kuwatumikia wananchi. Zoezi la kuandaa mkataba huo kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, lilishirikisha/ linashirikisha wananchi wote ama moja kwa moja ama kwa njia ya uwakilishi, ni jambo jema. Wafaransa, waanzilishi wa Jamhuri, kupitia mapinduzi yao maarufu, wana msemo: “hucheka vyema zaidi anayecheka mwishoni” Tunawaombea watanzania wapate mkataba/ katiba yenye uzalendo hasa wa watu hao. Mwishoni AfrikaKusini, bara Afrika na dunia iliondokewa na Nelson Mandela.

Nelson Mandela: mtu ambaye alipata umaarufu mkubwa kupitia mambo kadha wa kadha: kifungo chake kwa kuipinga serikali ya ubaguzi rangi nchini mwake, kung’atuka madarakani kisha muhula mmoja wa uongozi, kufanya maridhiano badala ya kulipa kisasi nchini mwake, kupata nishani ya Nobel, kutambuliwa mno na vyombo habari vya magharibi n.k. Kifo, heshima ya kitaifa na kisha mazishi  ya kitaifa ya Nelson Mandela al maarufu Madiba ilikuwa ni tukio kubwa la kidunia. Viongozi mashuhuri walifika kwenye kumuaga ndugu huyo ambaye ni sehemu ya wanaAfrika waliotoa mchango mkubwa wa kizalendo kwa bara hili: Mwalimu JK.Nyerere, Dr.Kwame Nkrumah, Dr. KenethKaunda, na wengine lukuki. Kwa Madiba pengine maneno ya Sauli ama Paulo kwa Warumi 5: 3-5 yanaweza kufaa sana hapa. Kwa sasa tuishie hapa. Lakini kwa ujumbe kwa vijana.


Mwaka unapokwisha si kitu cha ajabu sana kwa maana ya kuja kwa jambo jipya kabisa ni mzunguko ule ule wa Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Kwa kuwa mzunguko ni ule ule nawaalika vijana kutafakari juu ya malengo ya maisha yenu/ yetu. Nini hasa unataka kufanya duniani: kukusanya mali za dunia yote, “itakufaidia nini kupata mali zote na kisha kupoteza nafsi yako” Maneno ya Mmisionari mmoja. Maneno na tafakari hii ni muhimu kwa vijana kwani mwaka huu tumesikia lukuki (hatuna takwimu hapa) wakikamatwa na dawa za kulevya…Kukusanya mali na tena kuvumbua njia nyingi iwezekanavyo za kukusanya mali lakini kwa njia halali ni muhimu vyema lakini tusisahau pia kuwa mwili ni mmoja lakini wenye mahitaji ya kiroho pia...

Wasalaaam,

No comments:

Post a Comment