Thursday, December 26, 2013

SIKU YA KUFUNGUA MAKASHA YA ZAWADI




                                                                                                                           
IMEPAKULIWA HAPA : https://www.youtube.com/watch?v=L99hWdZGelI

Siku moja baada ya Noeli imekuwa, kimapokeo, ni siku ya kufungua makasha ya zawadi. Soma hii taarifa inaonyesha kuwa kazi ya kupokea makasha ya zawadi ni ya wafanyakazi nyumbani, Makasha ya zawadi hupokelewa kabla ya siku husika na leo kazi inakuwa moja tu ya kuyafungua makasha hayo kutaka kujua kuna nini humo ndani. Utamaduni wa kupeana zawadi siku za matukio maalumu ni jambo na utamaduni mzuri.

Jambo hili ni sehemu ya tamaduni za jamii nyingi duniani, na kama si sehemu ya tamaduni zetu basi ni jambo la kuiga na ni vyema tukafanya hivyo kwa wale tusio na utamaduni huo. Kufanya hivyo kunaendeleza na kujenga udugu, umoja, upendo n.k katika jamii. 


Kupitia utamaduni wa kupeana zawadi tujifunzie hapo hapo pia kutoa misaada kwa wahitaji bila kujali mahusiano yetu ya kindugu. Kwa asili binadamu wote tu ndugu wamoja. Asili, chimbuko letu wote; kidini, kibaiolojia/kisanyansi ni moja. Hivyo tunawajibika kusaidiana. Kwa wale wenye makasha mengi ya zawadi tuwakumbuke wahitaji wasio na msaada wa karibu; yatima, wajane, wagonjwa na wengine wote wenye kuhitaji katika jamii.   

Thursday, October 31, 2013

Maonyesho Mtwara katika Picha


Vikapu vya kiwango cha juu kabisa katika maonyesho ya Mtwara




Sehemu ya Maonyesho ya wajasiriamali




Mawasiliano ya baadhi ya vikundi vya wajasiriamali toka sehemu mbalimbali








Maonesho ya WajasiriaMali Mtwara




















Maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiria mali kutoka pande mbalimbali za nchi na  nchi jirani yamenza mjini Mtwara. Maonesho hayo yaliyoandaliwa na SIDO na wadau wenzi, yanalenga kuonesha bidhaa anuwai zitengenezwazo na wabunifu na pia kutafuta masoko toka kwa wadau. Mkoa wa Mtwara, ambao umesikika masikioni mwa wadau wengi hivi karibu kufuatia kugunduliwa kwa gesi asilia, unaanza kuwa moja ya masoko makubwa tarajiwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maonesho haya ambayo yamefunguliwa rasmi na ndugu mwenye dhamana ya viwanda vya Tanzania, ni fursa nzuri ya kuweza kuonesha bidhaa na mwanzo mzuri ya viwanda vyetu wenyewe kuanzia hatua za mwanzo kabisa. Kupitia wadau hawa wa bidhaa hizo ndogo, Taifa linaweza siku za usoni, kama tutaweka mkazo wa kutosha, kuwa na viwanda vyake lenyewe. Ili tuweze kufikia ndoto na lengo hilo ni muhimu kutengeneza mazingira ya kuwawezesha wajarisiliamali wetu kutengeneza bidhaa zao kwa gharama nafuu. Gharama za uzalishaji ikiwa ni pamoja na mali ghafi zikiwa  na bei ya chini, itawezesha wadau wengi kujiajiri na bidhaa zao zitakuwa na bei ya chini.

















Nasema hivyo kwa kuwa baadhi ya bidhaa nilizoziona zinauzwa kwa bei kumbwa mno ukilinganisha na ubora wake. Bidhaa  nyingi ni za asili kabisa na hivyo kuwa imara ukilinganisha na zitangenezwazo na makanjanja mjini, japokuwa ubora wake unahitaji kuongezwa zaidi ili zivutie wanunuzi wengi zaidi. Nilipohoji juu ya bei mmoja wabunifu wa bidhaa alisema: "nalazimika kuuza kwa bei ya juu kwa sababu nalipia kodi na  ushuru mbalimbali na pia kwa kuwa hakuna watazamaji wengi nauza bei ya juu ili kupitia mauzo haya nijikimu hapa mjini". Baadhi ya wadau hawa wa bidhaa asilia waliomba waandalizi wa maonesho haya wafikilie kuwalipia baadhi ya gharama ili kumudu vyema zaidi maonesho hayo. (Mwandishi hakupata fursa kuongea na timu ya maandalizi juu ya suala hili)

















Wakazi wa mjini Mtwara, hawajahamasika vya kutosha kutembelea maonesho hayo, jambo ambalo lingewezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao na kumudu kujikimu kupitia mauzo hayo. Hata hivyo ni fursa kwa wenyeji wa mkoa huo kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na maisha na utawala wa mazingira ya binadamu.

Kwa wajasiria mali, napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazozifanya, ila nawashauri pia waweke vitambulisho vya nchi zao wanakotoka ili kutambulisha bidhaa zao na pia kuzitambulisha nchi zao kibiashara zaidi. Hili linajumuisha kundika kwenye bidhaa jina la nchi bidhaa ilikozalishwa, kundika anuani  ama utambulisho uliojitosheleza ili mdau husika apatikane kwa wepesi kokote duniani. Ni muhimu kufanya hivyo kwani dunia imekuwa ndogo mno kupitia mapinduzi ya mawasiliano ulimwenguni.

Thursday, September 12, 2013

MTAZAMO MAISHANI


Bodi ya Korosho Mjini Mtwara

Bodi ya Tumbaku Mjini Tabora


Mtazamo wa nafsi yako mwenyewe - Picha kwa hisani ya wadau

Thursday, July 25, 2013

SIKU YA MASHUJAA NA UZALENDO TANZANIA


Sehemu ya wanajeshi wa Tanzania wakitoa heshima kwa Amiri Jeshi mkuu wa majeshi.
Picha kwa hisani ya BBC

Tarehe ya leo imeteuliwa kuwa siku ya mashujaa Tanzania. Ni tarehe waliyopokelewa wanajeshi wetu- mashujaa waliokuwa vitani nchini Uganda. Wanajeshi wetu walikwenda kazini kumnyoosha nduli Iddi Amini. Rais huyo wa zamani wa Uganda aliyejigamba kuwa na nguvu za kuchukua sehemu ya Ardhi ya Tanzania na kuifanya kuwa sehemu ya nchi yake. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999), kwa kutumia vigezo vya "vita halali" just war ya St. Augustine of Hippo 354-430  alitangaza vita kwa kuzingatia sababu inayokubalika, kujilinda dhidi ya adui, na kupigana vita kwa uangalifu na kupunguza maumivu kwa wasio na hatia. Vijana wa jeshi la Tanzania na nchi yote kwa ujumla tulishinda.

Tunapokumbuka mashujaa wetu, watu wengi hufikiria tu wanajeshi na wapiganaji wengine waliolipigania Taifa letu. Hapa utakumbuka watawala kama Mkwawa, Kimweri, Mirambo, Mputa, na wengine wengi. Ni vyema sana kuwakumbuka ndugu waliokuwa tayari kulilinda Taifa letu. Muhimu katika kumbukumbu hii ni suala zima la uzalendo. Watu wote tunaowatambua kama mashujaa, kwa namna fulani walikuwa na uzalendo mioyoni mwao. Hawa ni sawa na watu tunao watambu kama watakatifu, watakatifu huitwa wadhambi waliotubu. Nawafananisha mashujaa katika nchi na watu wenye "utakatifu" unapowapima kwa vigezo vya uzalendo. Kumbe tunapowaheshimu mashujaa wetu ni lazima tujitazame na kujipima uzalendo wetu.

Mzalendo tunamtarajia kuwa mtu mwenye kuipenda kwa moyo wake wote nchi yetu ya Tanzania. Katika hili kila mmoja na hasa wenye ofisi za Umma ama zozote zenye kutoa huduma kwa umma wa wanadamu, wanaalikwa kujipima, wanajali kwa kiasi gani maslahi ya wananchi walio wengi dhidi ya maslahi binafsi. Kiongozi anapopata fursa ya uongozi anatakiwa kufanya hivyo kwa niaba ya wananchi walio wengi; na ili aongoze vyema kuna mkataba unaomwelekeza kama anavyosema mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau(1712-1778) kwenye kazi yake ya The Social Contract (1762), kiongozi anafanya yale anayoelekezwa na wananchi na si anayotaka yeye; viongozi wangapi hivi leo hapa nchini wanazingatia anachosema mwanafalsa huyu. Wengi hawafuati makubaliano baina yao na wananchi, na kwa hivi wanalazimika kuacha mamlaka kwa wananchi wengine ili waongoze kama anavyosema mwafalsafa mwingereza John Locke (1632-1704). Locke anasema kiongozi mzuri anatakiwa awe na kumbukumbu ya makubaliano yake na wananchi moyoni mwake, vinginevyo aachie mamlaka.

Hivyo basi tunaweza kuwaenzi vizuri zaidi mashujaa wetu kwa kujitazama katika kioo na kuona kiwango cha uzalendo wetu kwa Tanzania yetu. Asanteni Mashujaa wetu na Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Thursday, July 18, 2013

SIKU YA MZEE MADIBA


Nadhani hii ndo siku pekee ambayo binadamu mmoja amepewa heshima ya kuwa na siku yake ya kimataifa duniani. Ndugu Nelson Mandela kapewa heshima hiyo hasa kwaajili ya kumaliza kwa amani, kupitia tume ya haki na maridhiano, mvutano ambao ungejitokeza baina ya weusi wengi, na jamii nyingine za watu wasio weupe wa asili ya Ulaya kwa upande mmoja, na wazungu wa asili ya Ulaya kwa upande mwingine.

Suluhu hiyo iliyohitimisha miaka mingi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kwa utulivu wa namna yake, ndo hasa sababu ya mzee Mandela kupewa heshima yote hiyo.

Saturday, June 1, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


National Arts Council BASATA
30/05/2013

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) kila Jumatatu kuanzia saa 4 Asubuhi limekuwa likiendesha ‘Jukwaa la Sanaa’ kwenye ukumbi wake ulioko makao makuu ya Baraza Ilala Sharif Shamba.Katika jukwaa hilo linalohusisha wadau wote wa sanaa, hoja nzito na motomoto kuhusu tasnia ya Sanaa na Utamaduni zimekuwa zikijadiliwa na kujibiwa.

Katika kuelekea urasimishaji wa Sekta ya Filamu na Muziki ambao ulianza rasmi tarehe 1/01/2013, ifikapo tarehe 01/07/2013 hakuna kazi yoyote ya Filamu na Muziki itakayoingia sokoni bila kuwa na stamp ya TRA. Baraza la Sanaa katika Jukwaa la Tarehe 03/06/2013 litazikutanisha taasisi zote nne zinazohusika na urasmishaji ili kutoa elimu kwa Wasanii, wadau na wakuzaji sanaa kuanzia saa 4 :30 Asubuhi. Wadau wa sekta ya sanaa mnakaribishwa kuleta michango na hoja zenu ili kuleta mustakabali utakaojenga sekta ya sanaa. Taasisi zinazohusika na Urasimishaji wa sekta ya sanaa ni :

1. Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza

2. Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (COSOTA)

3. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

4. Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)

WOTE MNAKARIBISHWA
Godfrey Lebejo Mngereza

KAIMU KATIBU MTENDAJI, BASATA


Barua zote ziandikwe kwa Katibu Mtendaji

All correspondence to be addressed to The Executive Secretary

BASATA Arts Centre, Ilala Sharif Shamba, P.O. Box. 4779, Dar es Salaam, Tanzania.

Telephone: 2863748/2860485, Fax: 0255 - (022) - 286 0486 E-mail: info@basata.or.tz Website: basata.or.tz



Salaam za Rambirambi


Baraza la Sanaa la Taifa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii wa tasnia ya Muziki nchini Albert Mangwea a.k.a Ngwair.

“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Ngwair ambaye mchango wake unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wao bado unahitajika katika tasnia hii.” Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.

Tunaomba mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, tutambue kuwa haya ni mapenzi ya Mungu.


Imetolewa na
Ghonche materego
Katibu Mtendaji
Baraza la Sanaa la taifa.

Monday, May 13, 2013

FAINALI ZA MASHINDANO YA KUTETEA UHAI (PRO-LIFE)


Makamu bingwa wa kombe la kutetea Uhai timu ya STEMMUCO

Mabingwa wapya wa kombe la kutetea Uhai -
Timu ya Chuo cha Utumishi wa Umma - Mtwara

Wachezaji wa timu zilizofika fainali wakimsikiliza mgeni rasmi





Weledi?









JUHUDI KAZINI?














KAZI NI MOJA TU SASA



Wanazuoni wa mwaka wa tatu chuoni STEMMUCO kwa juma la pili sasa wamekuwa wakitetea tafiti zao walizofanya kwa mieza kadhaa. Tafiti hizo, ambazo ni sehemu ya wajibu wao ili kupata sifa ya kupata shahada yao ya kwanza, (degree ya kwanza) zilikuwa na mada tofauti tofauti kama jinsi walivyo watu na miguso yao.

Baadhi ya kazi zilihusu mchango wa Chuo Kikuu cha STEMMUCO kwa maisha ya watu wa Mtwara kwa ujumla wake, zingine na nyingi hasa zilihusu masuala kadhaa ya elimu. Kwanini shule za Mtwara ubora wake wa elimu ni hafifu, kwanini shule za serikali ubora wake mbele ya zile za binafsi ni dhaifu n.k. Zingine zilihusu shughuli za kiuchumi mkoani Mtwara; uzalishaji chumvi na athari zake, mchango wa bandari Mtwara kwa wananchi. Kazi za wanazuoni wengine zilitazama masuala ya kijamii; kuongezeka kwa watoto wa mitaani, Unyago, jando na faida, hasara na changamoto zake. Mazingira pia hayakuachwa nyuma; tafiti kadhaa zimegusia suala hilo. Uhalifu ni moja ya mada zilizojadiliwa hali kadhalika.

Zoezi hili lilifanywa kwa lugha ya kiigereza; vijana wengi walijipanga na kutafuta misamiati stahiki kuelezea kazi zao; wapo waliofanya vyema sana, waliojitahidi sana na wanaohitaji kuongeza bidii zaidi. Kwa ujumla wanazuoni hawa ni hazina kubwa kwa taifa na wito kwao ni kuendelea na moyo wa kitafiti ili kuvumbua vyanzo vya matatizo na kuyafanyia kazi.



 



WASOMI WAKITETEA KAZI ZAO ZA TAALUMA

Baadhi ya wanachuo wa STEMMUCO wakijiandaa kutetea kazi zao za kitaaluma

Saturday, April 27, 2013

SIKU YA MUUNGANO STEMMUCO

Viongozi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Mwl. Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume wakitia saini makubaliano
Picha kwa hisani ya blogu ya Michuzi   
Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikumbukwa kianazuoni zaidi. Siku hii ya leo ambayo ni kumbukizi ya Muungano baina ya sehemu mbili tajwa hapo juu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; iliadhimishwa kwa namna yake. Kulikuwa na mada nne ambazo ziliwasilishwa na kujadiliwa na wadau mbalimbali ambapo dhima kuu ilikuwa ile ile ya umoja, haki, amani na mshikamano kwa watanzania ili kufikia malengo ya kuungana.



                                  
                                                 Mwalimu Julius K. Nyerere akichanganya udogo wa Tanganyika na Zanzibar
                                                ishara ya muungano huo. Hii kwa hakika ishara yenye nguvu sana.
                                                            Picha kwa hisani ya blogu ya Michuzi

Muungano pamoja na malengo mengine, kwa vyoyote vile ulikuwa na lengo la kufikia maendeleo ya binadamu; maendeleo ya kweli ya Mtanzania na kutoa mfano halisi wa Umoja ama muungano wa bara Afrika.

Mada zilizotolewa pale STEMMUCO zilikuwa pamoja na Muungano na MKUKUTA, Muungano na Uzalendo, Mali asili na Muungano Afrika Mashariki  

Friday, February 8, 2013

MITIHANI INAENDELEA STEMMUCO


WATAALAMU WA BAADAYE WAKIONYESHA UJUZI WA
MAJUMA 16 KATIKA SAA TATU

WANACHUO STEMMUCO WAKIENDELEA
NA MITIHANI MJINI MTWARA



WALIMU WAJIPIMA UJUZI WAO KABLA YA KWENDA KUFUNZA
WENGINE - MITIHANI


Thursday, February 7, 2013

AFRIKA SIMAMA MWENYEWE


Bonde la Olduvai - Picha kwa hisani ya blogu husika

Waziri mkuu wa kwanza wa Kongo
Picha kwa hisani ya blogu husika

Bara letu tukufu la Afrika, kwa mara nyingine limo tena katika migogoro baina yetu wenyewe. Bara Afrika lenye nchi zaidi ya hamsini lilianza kujipatia uhuru wake zaidi ya miaka hamsini iliyopita. Ghana ilikuwa nchi ya mwanzo kabisa, yenye waafrika weusi wengi zaidi, kujipatia uhuru wake chini ya ndugu Kwame Nkurumah. Na mara ya mwisho nchi ya Afrika kujipatia uhuru wake ilikuwa ni Namibia? tarehe 21 Marchi 1990. Ukiacha Sudani Kusini iliyopata uhuru wake toka kwa ndugu yake Sudani tarehe 9 Julai 2011. Afrika Kusini; iliyopata uhuru wa watu weusi walio wengi mwaka 1994  ilikuwa na hali ya kipekee sana; ilivamiwa na wazungu walioifanya nchi hiyo kuwa nyumbani kwao. Nguvu ya Umma haikuzuilika tena na ilikuwa lazima wananchi walio wengi wapate haki yao. Kwa utangulizi huu, ingawa mfupi mno kwa bara lenye kila aina ya utajiri, binafsi nadhani bara hili, japokuwa ni changa kwa umri wa mataifa ya kisasa lakini kongwe kihistoria kwakuwa ndo nyumbani kwa binadamu wa kwanza; tazama Olduvai Gorge, ilitakiwa tuwe na uwezo wa kujitawala na kujisimama wenyewe. 

Afrika ina utajiri anuwai na wenye kupatikana katika nchi nyingi za barani mwetu. Pamoja na utajiri tulionao tunaendelea kuonekana kama masikini wa kutupwa. Wayuropa na Wamarekani na hata Waasia wanatufanya sisi (ama sisi wenyewe )  kama binadamu wa daraja la pili. Matokeo yake ni kubweteka, kukosa fikra zetu wenyewe, kuwa tegemezi na kusubiria misaada toka kwa hao wajomba wasiozaliwa tumbo moja na mama zetu.

Utegemezi upo kwenye nyanja nyingi sana za maisha yetu; toka kwenye mipango ya maendeleo hadi kwenye masuala ya vyakula vyetu wenyewe. Nchi zetu (kupitia viongozi tulionao) ni kama hazijui tunahitaji kitu gani na tunataka kwenda wapi. Utasikia mpango wa maendeleo tunanakili toka Ulaya na Marekani kama ilivyo ili hali tukibadilisha majina na mahitaji yetu mahususi tu. Jambo hili linadumaza hata fikra za vijana wetu shuleni na vyuoni; kwanini kuwa mbunifu ili hali mawazo yangu hayatumika popote, anajiuliza mwanafunzi. Badala ta kutumia muda mwingi kujenga fikra binafsi sahihi ni afadhali kufuatisha mawazo ya watu wengine. Utegemezi unatufanya tushindwe kujenga mambo yetu wenyewe. Mathalani kwenye elimu fursa za kimasomo zinazotolewa nje ya nchi; bila shaka ni kwa lengo zuri tu la kusaidia kujenga wataalamu toka katika nchi zinazokuwa. Hata hivyo ni vyema kutazama misaada ya aina hiyo kwa jicho la kichunguzi; inawezekana kabisa nyuma yake kuna fursa ama bidhaa zinazohitajika toka nchi zetu hivyo unazilainisha nchi hizi zinazoendelea kwa misaada midogo kama hiyo. Nasema midogo kwa sababu nchi zetu za kiafrika zina wajibu wa kujenga shule na vyuo vikuu vyenye sifa na hadhi kubwa kidunia kwa sababu vinavyohitajika kufanya hivyo vipo hapa barani. Tutazame mifano wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo. Kwenye makala hii nitatumia zaidi jina KONGO 

KONGO - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Kongo ni "JITU" lililolala. Nchi hii ina utajiri asilia wa kila namna. Nchi Kongo kuna misitu asilia, madini ya kila namna, watu wenye nguvu na akili, ardhi/ wenye rutuba, mito, nguvu ya umeme, bahari, tamaduni nyingi nzuri na kadhalika. Pamoja na utajiri mkubwa usiodikika, wananchi wengi nchini Kongo hushindia mlo mmoja tena mara nyingi usio kamili. Wafanyakazi  wengi nchi humo hupitisha miezi bila malipo, bidhaa nyingi zinazopatikana huko hutoka nchi jirani. Kongo ilipopata uhuru wake toka mikononi mwa Ubelgiji (kinchi kidogo kikilitawala jitu kubwa vile) tarehe 30 Juni 1960 chini ya uongozi wa rais wa kwanza Joseph Kasa vubu na waziri mkuu wa kwanza Patrice Lumumba  ambaye alikuwa na mawazo mengi mazuri juu ya bara zima la Afrika, Siku ya uhuru wa nchi yake, kama ilivyokuwa huko Ghana kwa Kwame Nkurumah, aliyesema kuwa Ghana sana u huru milele, Lumumba yeye alisema Kongo itakuwa muhimili wa mambo mengi makubwa Afrika na duniani (si maneno yake moja kwa moja - mengi ni tafsiri na vionjo vyangu zaidi). Leo miaka zaidi ya hamsini kisha uhuru hakuna kiongozi wa jitu hilo kubwa aliyeweza kufikia mawazo ya mwana Afrika huyu halisi. Toka kifo chake nchi hii imekuwa itawaliwa kwa namna isiyokubalika, hususani kipindi cha rais aliyeiongoza nchi hiyo kwa muda mrefu Mobutu Sese Seko. Ndugu huyu aliifanya nchi kuwa mali yake binafsi na kufanya alivyotaka. Msemo wa Kiswahili; "Mungu si Athumani" bwana huyu aliondolewa madarakani na vikosi vya Laurent Kabila mwaka 1997. Laurent Kabila, kama ilivyo kwa historia za wapigania uhuru wengi wa Afrika, alishiriki shughuli za kisiasa toka ujana wake kwenye kikosi cha vijana cha Patrice Lumumba. Ndugu huyu alikuwa na matamanio na nia njema sana ya kuleta uhuru wa kweli kwa watu wa Kongo, lakini alishindwa kwa kuwa alikuwa amefungamana na makundi yaliyokuwa na uchu mkubwa wa mali za nchi hiyo. Hivyo miaka minne baadaye aliuwawa. Toka kuuwawa kwake bado hakujawa na uimara thabiti japokuwa Joseph Kabila, mtoto wa rais kabila, anajitahidi kuongoza nchi hiyo kubwa. Hata hivyo kuna waasi wanaoibuka na madai mbalimbali juu ya Kongo.

Hivi karibuni kumezuka kikundi kingine cha waasi maarufu kwa jina M23. Hili ni moja kati ya makundi mengi ambayo tayari yamekwishaibuka ili kudai wanachoita kuwa haki zao. Yamewahi kuibuka makundi mengine kadhaa wa kadhaa "Banyabulenge" na mengine.  Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, mashirika ya kikanda na mashirika mengine mbalimbali duniani yamejaribu kuleta amani ya kudumu bila mafanikio ya kweli kwa muda mrefu sasa. Binafsi nadhani suluhu kwa machafuko ya Kongo imo mikononi mwetu Waafrika na nadhani tunaweza kujilinda na kujiletea maendeleo ya kweli. Kongo ina utajiri mkubwa mno kiasi kwamba wengi wanaokwenda kupatanisha wanaingia kwenye mtego wa kujichukulia utajiri huo japokuwa kidogo- ni vigumu kupata ushahidi wa kuandikwa katika haya lakini kuna mambo mengi yanaendelea. Umoja wa Afrika kwa makubaliano ya Kongo unaweza kujenga jeshi imara na kulinda amani itakayoleta maendeleo ya kweli kwa nchi hiyo. Naamini kuwa uchumi wa Kongo ukiwa imara uchumi wa bara zima utanufaika na kukua vyema zaidi.  Afrika tuna uwezo na wa kufanya mambo yetu wenyewe shida ni huko kupumbazwa na Wayuropa na Wamarekani - matokeo yake tunajihisi kuwa hatuwezi. Afrika simama mwenyewe imara unaweza!