Hatusemi kuwa Tanzania haijapiga hatua za kimaendeleo, la hasha! Maendeleo makubwa yamefikiwa nchini Tanzania toka nchi hii ipate uhuru, hatua hizo za kimaendeleo kwa hakika zaoneka vyema hata kwa asiye na macho ila tu kwamba mwendo kasi bado ni wa taratibu mithili ya ule wa kobe. Na kwa upande wa fikra sehemu nyingi za bara letu bado hatujajikomboa kwenye fikra yakinifu. Watu wetu wengi wanaendelea kuwa tegemezi wa nadharia na fikra za waYuropa na waMarekani na hivi punde tutahamia Beijing. Kufanya hivi kwa lengo la kujifunza si mbaya, lakini hatuna mikakati mahususi ya kufundisha na kuwaonyesha ukweli huo watu wetu ili kwamba waAfrika wengi zaidi tuweze kuwa na ujuzi wa kiteknolojia unaotokana na tamaduni zetu wenyewe. Ili watu wengi zaidi tuweze kukomaa kifikra na kuwa na uwezo wa kuchambua masuala ya msingi maishani na kujenga hoja zenye mashiko na katika misingi inayokubalika, basi ni vyema watu wetu wapate kusoma falsafa, na tena waisome kwa lugha zao wenyewe. Suala hili tunaweza kuliongelea siku nyingine, sasa natuingie mada ya leo. Elimu ya mlaji juu ya bidhaa anuwai zilizopo kwenye maduka na sehemu mbalimbali za kutolea huduma kwa wananchi.
Hapa nchini na nchi nyingi Afrika, tuna bidhaa nyingi zinazotoka nje ya bara letu, zipo pia zinazotengenezwa katika nchi zetu. Kuna bidhaa anuwai katika maduka ya bidhaa; baadhi ya mahitaji hayo yapo toka viwanda, nchi, tamaduni na ustaarabu tofauti na wa nchi mbalimbali. Chukua mfano wa dawa ya meno. Madukani zipo za kila aina; Whitedent, Colgate, Rungu, nini dent na kadhalika.., Sabuni za kipande; Jogoo, Mbuni, Magwanji, Dobi...Sabuni za kuogea; Malaika, Ayu, Geisha, Protex, Familia...Sigara; Nyota, Baridi, SM, Aspen, Portsman n.k. Baadhi ya bidhaa nilizozitaja huwa na maelezo ya matumizi na faida kwa mlaji / mtumiaji. Hata hivyo tuna bidhaa nyingine nyingi ambazo hazitoi maelezo yoyote ya matumizi, faida na hata hasara kwa mtumiaji lakini bidhaa hizo zipo madukani na sehemu nyingine za kujipatia mahitaji. Ni jambo muhimu na lazima kwa bidhaa kuwa na maelezo kwa mtumiaji. Vyombo husika nchini vina jukumu la kufanya hivyo ili kunusuru afya za wananchi na kuwawezesha kufika inapotakiwa.
Nchini kuna mafanikio yaliyofikiwa; watengeneza sigara walitakiwa kuweka alama ama tangazo linaloonyesha madhara ya bidhaa hiyo na kwamba atakayeamua kuitumia afanye hivyo kwa hiari yake mwenyewe na si kwa kukosa elimu. Nadhani halikuwa jambo jepesi, pamoja na kwamba maandishi yale ni madogo, lakini walau jambo hilo limefanyika. Hata hivyo kuna bidhaa nyingine nyingi zinahitaji kuelezewa ili kufanya mambo yaende sawa sawa. Natumia mifano miwili tu hapa. Mmoja ni mfano wa bidhaa inayoingia mwilini mwa binadamu na mwingine ni wa bidhaa tunayoitumia kujenga nyumba zetu; vinywaji baridi na saruji.
Vinywaji baridi al maarufu zaidi SODA; havionyeshi vilivyotumika kutayarisha bidhaa hiyo. Faida wala hasara yake mwilini haijulikani kwa watu wengi. Binafsi naamini kuwa bidhaa hizi zina faida na hasara mwilini kama ilivyo kwa bidhaa nyingi, sasa kama ni hivyo kwanini mimi mtumiaji sipatiwi hiyo elimu? Je nini lengo la kutotoa elimu hiyo kwa mtumiaji? Je, tunaangalia faida za kiuchumi tu kuliko afya ya mlaji? Ni muhimu kwa vyombo husika kuwasimamia waandaa bidhaa hiyo ili watoe hayo maelezo muhimu. Na serikali kwa ujumla wake inalazimika kusimamia hilo, ni vyema kufanya hivyo bila kuogopa tu kupungua kwa kodi toka makampuni husika pindi wananchi watakapofahamu kilichomo ndani ya vinywaji hivyo na kusitisha ama kupunguza matumizi yake. Najua yamekuwa ni mapokeo kwa baadhi ya bidhaa, toka nchi fulani zenye nguvu kiuchumi, kutotaja vilivyomo kuepuka mbinu zao za biashara kuibwa na washindani wao, lakini sisi tunasema afya za watu wetu walio wengi ni muhimu zaidi kuliko faida za wachache wanaonufaika kupitia ujinga wetu juu ya bidhaa zao.
SARUJI: hii ni bidhaa muhimu katika nchi nyingi zinazoendelea; nimeona hata kauli mbiu ya moja ya makampuni hayo kuwa ni kulijenga bara Afrika. Nchini Tanzania, hivi sasa kuna makampuni kadhaa yanayozalisha bidhaa hii muhimu. Kwa hakika hili ni jambo la msingi na la kimaendeleo kabisa kupitia bidhaa hii wananchi wengi zaidi wanaweza kujijengea nyumba zao za kisasa na za kudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko za tope na nyasi. Mjini Mtwara; kwenye maduka mengi ya vifaa vya ujenzi utakutana na saruji / simenti ya Simba, Twiga, Rufiji, Rhino na kadhalika. Bidhaa hizi huwa na bei tofauti tofauti; tofauti hii ya bei bila shaka inasababishwa na mambo kadhaa; huenda ikawa ni gharama za uzalishaji, ubora, ama tu tamaa ya pesa nyingi. Hata hivyo tatizo langu hapa, kama ilivyo kwa SODA ni lile lile la kutopata elimu ya mtumiaji. Sikumbuki kuona mfuko wa simenti aina yoyote, hata mara moja, ukiwa na maelezo juu ya bidhaa na utumike sehemu ipi ya nchi; kwa maana ya aina ya udongo ama ardhi, ama aina fulani ya saruji itumike katika hatua ipi ya ujenzi; msingi, kujenga boma na kadhalika. Nafahamu kuwa baadhi ya makampuni ya ujenzi hufanya upembuzi yakinifu juu ya hilo na kujua pengine aina ipi ya saruji itumike, hata hivyo inanitia mashaka kwa kuwa hakuna kilichoandikwa popote pale. Makampuni, na wananchi wenye uwezo mkubwa zaidi kiuchumi wanaweza kufuata maelekezo na taratibu za kihandisi kwa uaminifu na si wananchi wa kawaida. Mwananchi anayejenga wa kiwango cha kati atatumia saruji ya bei ya juu kwa imani kuwa hiyo nd’o yenye ubora takikana ama atatumia uzoefu wa fundi mahalia, ambaye mara nyingi hana hata hiyo elimu husika.
Wito kwa wadau wa saruji, najua kuwa sisi sote ni wadau, lakini moja kwa wenye makampuni ya kutengeneza saruji; wahakikishe wanaweka maelekezo yatakayoheshimu thamani ya pesa na kumpatia mtumiaji/mlaji kile anachohitaji na kustahili kupata. Kwa vyombo husika vya serikali; wasimamie kuwekwa kwa maelekezo hayo ili wananchi wanufaike vilivyo na kujenga taifa la watu wa kima cha kati kama usemavyo mkakati wa maendeleo wa taifa wa 2025 na si hohehahe. Wananchi mmoja mmoja tusaidiane kudai haki zetu kwa njia ya amani na kwa utaratibu unaokubalika kisheria.
Hitimisho la jumla ni kwamba wazalishaji wote nchini na barani Afrika wazalishe bidhaa zenye ubora, maelekezo ya matumizi kwa walaji / watumiaji ili kujenga afya njema kwa wananchi na kusaidia kusukuma mbele zaidi hatua za kimaendeleo kwa wananchi mmoja mmoja, Tanzania na bara Afrika zima kwa ujumla wake.