Wednesday, November 23, 2011

Fikra za watu na tafsiri zao!



Hivi mawingu huko angani hutoa ramani za sehemu mbalimbali
ama hutokea tu yakawa jinzi yalivyo kwa bahati tu? Wataalaam
wa Jiografia tafadhali tunaomba maelekezo ama tafiti kujielimisha zaidi  
Hivi karibuni nimesikia mtu aliyetoa tafsiri ya kuwa barani Afrika kumejaa migogoro inayochelewa kutatuliwa na mingine iliyodumu kwa miongo kadhaa sasa kwa sababu ya umbile la bara hilo. Ndugu huyo amedai kuwa bara la Afrika lina umbile la silaha aina ya bastola. Kwamba umbile hilo linalisababishia bara letu kukosa amani ya kudumu.

Bila shaka huu ni mtazamo wa mtu mmoja. Inafaa kuongelea kitu ambacho mtu amekifanyia tafiti ili kuepukana na taarifa  ambazo hazina ukweli wowote ila tu kuipotosha jamii ya wanadamu. Tujenge utamaduni wa kufanya tafiti za kina na si kwenda kwa sangoma kwa mambo ambayo tunaweza kuyapatia suluhu. Bila kufanya tafiti na kuwaelewesha watoto wetu kwa uhakika mambo tuliyoyatafiti tutajijengea hofu na kuendelea kuwa jamii ya hofu na kuogopana.
  
Wingu hili linaonyesha ramani ya wapi na nini tafsiri yake?

Tuesday, November 22, 2011

Sheria ya Mazingira inaishia wapi...?






Plastiki na chupa za maji zikiwa zimetupwa huku na huko na abiria waliochoka
 kutoka na adha ya usumbufu unaoletwa na ubovu wa eneo lisilo na lami.


Barabara kwa Maendeleo

 

Abiria wa Mtwara - Dar es Salaam wakimbilia mabasi yao
baada ya kukwamulia toka tope lililotamalaki barabarani
Usafiri wa uhakika ni moja ya viashiria vya kimaendeleo. Njia za usafirishaji zikiwa nzuri hurahisisha maisha ya watu na kuharakisha maendeleo ya jamii husika na taifa kwa ujumla. Mtwara ni moja kati ya mikoa ambayo imekiwa kisiwa kutokana na miundo mbinu mibovu kwa muda mrefu. Mtwara inafikika kwa njia mbalimbali; kwa ndege, kwa meli, na kwa barabara. Watu wengi zaidi nchini Tanzania husafiri kwa barabara, japokuwa njia hii ya usafiri imejaa damu. Kujegwa daraja la Mkapa ulikuwa ni ukombozi mkuu kwa ukanda wa kusini. Serikali ya Tanzania imeendelea na juhudi kubwa kuijenga barabara ya Dar es Salaam – Mtwara, zaidi ya kilometa 500 kwa kiwango cha lami.

Matembezi ya hiari yaendelea
Ni kipande kidogo kisicho na lami ndo kinaendelea kuwatesa na kuwanyanyasa wananchi wa ukanda huu maarufu kwa zao la korosho na sasa gesi asilia. Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutaboresha maisha ya wakazi wa mkoa huo ambao ni tegemezi kiasi kikubwa kwa jiji la Dar es Salaam.

Wednesday, November 16, 2011

UDHAIFU CHAMA CHA WASANII TATIZO KWA MAENDELEO YAO

Na Mwanndishi wa BASATA
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Martin Mandalu akifafanua jambo wakati akiwaeleza wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya utafiti alioufanya kwenye Muziki wa kizazi kipya. Kulia ni  Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA, Godfrey Mungereza.







Utafiti uliofanywa kwenye muziki wa kizazi kipya ukilenga kubaini changamoto na mafanikio yake umebainisha kuwa, kukosekana kwa umoja miongoni mwa Wasanii ni moja ya sababu kubwa ya kudumaa kwa maendeleo yao.

Sababu zingine zilizotajwa ni pamoja na Wasanii kutokuzingatia mikataba kwenye kazi zao, utengenezaji wa kazi za sanaa zenye ubora hafifu, usimamizi dhaifu wa kazi zao, kukosekana kwa viongozi thabiti katika tasnia ya muziki na sababu zingine.

Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akionesha kitabu kilichoandaliwa na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin Mandalu kinachohusu Tasnia ya Muziki Mkombozi Kwa Vijana kwenye Jukwa la Sanaa wiki hii. Kulia ni mtunzi huyo, Bw. Mandalu.

Akiwasilisha utafiti wake alioukamilisha Mwaka huu kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii , Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin Mandalu alisema kuwa, bila wasanii kuzifanyia kazi changamoto hizo bado kutakuwa na safari ndefu katika kuyafikia mafanikio ya kweli.

Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakimsikiliza mmoja wa Wasanii aliyekuwa akihoji sababu hasa zinazowafanya Wasanii wasiwe kwenye umoja pamoja na juhudi zinazofanywa  za kuunda umoja wao.

“Asilimia 80 ya Wasanii waliohojiwa kwenye utafiti huu hawakuwa na taarifa ya uwepo wa umoja unaowaunganisha. Hii ni hatari kwa sababu nilipofika katika vyombo rasmi nilipata taarifa za uwepo wa vyama na mashirikisho ya wasanii. Hii ina maana wasanii hawatambui uwepo wa umoja huo” alisema Mandalu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Wasanii wengi waliohojiwa walikiri kuwa, wamekuwa wakipata mapato kidogo ikilinganishwa na kazi wanazofanya lakini hili likielezwa kuwa linasababishwa na kutozingatia mikataba, kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwao na Wasani kutaka kufanya kila kitu yaani utunzi wa nyimbo, usambazaji na hata umeneja.

“Wasanii wengi waliohojiwa walionekana kukosa uongozi na usimamizi thabiti. Walionekana kufanya kila kitu kuanzia utunzi wa nyimbo, kuzifanyia matangazao, kutafuta kazi za maonyesho na umeneja kwa ujumla” alisisitiza Mandalu wakati akifafanua utafiti wake.

Kuhusu utayari wa Wasanii kutoa taarifa au kufika maeneo wanayohitajika, Mhadhiri huyo msaidizi alisema kuwa, ni tatizo kubwa kwani wasanii wengi wamekuwa wazito katika hilo na hata kutokutoa ushirikiano wa kutosha katika masuala yanayowahusu.

“Wengi wa wasanii niliokuwa napanga kukutana nao, walikuwa hawaoneshi ushirikiano. Anaweza kukwambia tukutane saa tano lakini ukifika muda huo anakwambia ana kazi nyingine kwa hiyo haitawezekana” alisema Mhadhiri huyo wakati akieleza changamoto alizokumbana nazo.

Utafiti huo ambao umechapishwa kwenye Kitabu cha Tasnia ya Muziki Mkombozi kwa Vijana umefanywa na Mhadhiri huyo kama sehemu ya kupata shahada yake ya uzamili katika stadi za Maendeleo.

Friday, November 11, 2011

Vimbwanga vya 11.11.11


Bila ubishi hii ni moja ya tarehe za aina yake ambapo kukutana nayo tena katika maisha ya hapa duniani unahitaji kupingana na uzoefu uliopo duniani mpaka hivi sasa. 11.11.11 inatazamwa kwa namna tofauti tofauti na watu tofauti tofauti soma hapa kupata mtazamo wa wanahisabati wanasema nini juu yake.

Vazi la kitaifa na miaka 50 ya Uhuru Tanzania

 Mwanamitindo maarufu nchini Tanzania, Asia Idarous akipita jukwaani na mwanamitindo kuonyesha ubunifu wake katika ufunguzi wa Swahili Fashion week.

Picha kwa hisani ya blogu la michuzi








Umri wa miaka hamsini kwa binadamu si umri haba. Katika umri huo kwa hakika binadamu anaanza kuhesabu mengi aliyoyafanya; lugha yake inaanza kuwa ya wakati uliopita. Utamsikia nilipokuwa fulani, nilipokuwa na kina fulani, nilipokuwa sehemu fulani, nilifanya hivi, nilikuwa hivi... hata hivyo hiyo ni lugha hiyo ni watu tu wa sehemu fulani tu. Kuna wengine ambao husema miaka hamsini ndo kwanza maisha yanaanza na hivyo lugha zao ni zile za wakati ujao, nitafanya hiki, nitakuwa fulani... nita... nita... nita...

 Hata hivyo muhimu zaidi kwa Tanzani hivi sasa ni kuwa baada ya miaka 50 ya Uhuru wa taifa hili ambalo ni nyumbani kwa Serengeti,mlima Kilimanjarokreta ya Ngorongoro, nyumba kwa visiwa vya karafuu Zanzibar bado haina VAZI RASMI la kitaifa. Huu ni wakati kwa wanamitindo na wanasanaa kutumia ujuzi wao kutoa kinachoweza kuwa vazi la taifa na hivyo kuwasaidia watanzania kuwa na vazi lao la kujivunia lenye kubeba na kuheshimu tamaduni zetu. 




Thursday, November 3, 2011

KUMBE KWELI SISI SHAMBA LA BIBI...

Picha kwa hisani ya google
Moja ya makala za HabariLeo katika chapisho lake la leo, imetoa habari inayotufanya nchi yetu kuonekana kama shamba la bibi lisilo na mmiliki...

Bibi ni mama mzazi wa baba ama mama; ni mtu muhimu kwani, huyu pamoja na mumewe ama mwanaume flani ambaye tutamuita babu, ameshiriki moja kwa moja kuwaleta duniani wazazi wetu. Mtu huyu ki-umri amekula chumvi nyingi, na kitamaduni sehemu nyingi barani ni mahiri katika mambo mengi. Ujuzi na busara ya mambo ipo katika uzoefu wa siku nyingi.

Bibi ndiye aliyewalea baba na mama (kila mmoja na mzazi wake - wote waitwa bibi ); hivi basi kwa jinsi wazazi wetu walivyo na nidhamu na utaratibu wa maisha, sehemu flani wamevipata toka kwa bibi. Ni yeye hasa ndio aliyewalea na kupata watoto wenye maadili mema na staha kama tuwajuavyo wazazi wetu. Ni kweli kuwa hupata ujuzi mwingine kwenye mazingira waliokulia, mafunzo sehemu mbalimbali lakini nafasi ya bibi kwa maana ya mzazi na mlezi ni kubwa hasa. Hata hivyo kuna jambo jingine ambalo hushangaza sana toka kwa bibi.

Kina bibi wengi wanaelezewa kama watu wenye kuwadekeza kupindukia watoto wa watoto wao; wajukuu. Kiasi cha kuwadekeza huko, huwashangaza watoto wao yaani baba na mama zetu, ambao mara nyingine hulazimika hutoa simulizi za namna ambavyo bibi alivyokuwa mkali enzi za malezi yake kwao. Kuna sababu kadhaa zinazoeleza kwanini bibi anakuwa mpole na rafiki mno kwa wajukuu zake. Moja ya sababu hizo ni uzee, uchovu na upweke wa utu uzima. Bibi anawahitaji watoto wa watoto wake ambao kwake ni marafiki; ili kuwapata mara nyingi huweza kutumia rasilimali alizonazo kuwaweka kwenye himaya yake. Ni kupitia mwanya huo basi mali za bibi huweza kutumika vibaya; kuharibiwa, kuhujumiwa, kila mmoja akachukua anachotaka na tena kwa nafasi yake. Katika hili bibi hajali mali yake inaharibiwa kiasi gani, muhimu kwake ni kujenga mahusiano na wajukuu wake wakiharibu ama wasiharibu hilo si muhimu kwake muhimu ni kwamba uhusiano wa kirafiki na wajukuu unakuwa bora zaidi na zaidi. Ni kutokana na masuala hayo ndo analojia ya shamba la bibi ikazuka.

Habari Leo hivi leo wametoa taarifa yenye kufanana na analojia ya shamba la bibi. Hapa nchini, katikati ya kitovu cha uchumi wa nchi, Dar es Salaam kumekuwa na shule ikiendeshwa kinyume na sheria kwa miaka kumi na miwili. Hii inaweza kuwa kipande cha pande kubwa la “jabari” la barafu baharini. Si ajabu kuna mengi ambayo hayajagunduliwa na tena yenye madhara makubwa kwa taifa.  Nchi ina mali asili nyingi tena za kila namna; je ni namna gani rasilimali hizo zinaendeshwa katika namna inayowanufaisha wananchi walio wengi na taifa kwa ujumla wake.

Tanzania ina mbuga lukuki za wanyama pori, je shughuli za kiuchumi za wanyama pori zinafanyika kwa jinsi inayotakikana? Je, taifa linapata pato stahiki? Tanzania ina bahari, maziwa, mito na mabonde yenye uwezo wa kunufaisha taifa kwa namna anuwai; je watu waliokabidhiwa madaraka kuendesha vyanzo hivyo vya mapato wanaitendea haki jamii na taifa kwa ujumla? Je, shughuli hizo zinaendeshwa katika namna endelevu? Ili kwamba wajukukuu wa wajukuu wetu wakute mali hizo ama faida zake na wao pia wamudu kuendesha maisha yao kwa furaha? Tunaweza kuorodhesha utajiri na zawadi nyingi zilizopo nchini  hata hivyo si nia yangu kufanya hivyo lengo ni kukumbushana juu ya taifa letu na mustakabali wake.

Kuhitimisha tunasema kuwa kila mmoja wetu awajibike kizalendo ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa letu la Tanzania, na kuboresha maisha ya jamii ya wanadamu wanaoishi sasa na wale watakao kuja baadaye kwa taratibu na sheria zinazokubalika.

Monday, October 31, 2011

KIBANGA AMPIGA MKOLONI

Na. Maisha na Mafanikio
Zamani za ukoloni, palitokea Mzungu mmoja. Mzungu huyo hakuwa mtu mwema. Alikuwa mkali na mkatili sana. Kwa ajili ya ukatili wake watu walimwita mkoloni. Wanancgi wote walimchukia sana popote pale alipokwenda.


Mzungu huyo alikuwa Bwana Shamba. Alikuwa na bakora iliyokuwa imetengenezwa kwa mkwaju. Kila alipokwenda kukagua mashamba, alikuwa na bakora hiyo mkononi. Alipendelea sana kuitwa "Bwana Mkubwa". Mkolono huyo alifurahia sana kupiga watu. Aliwapiga watu waliposhindwa kupalilia mashamba. Aliwapiga pamba yao ilipokuwa chafu. Aliwapa taabu sana.

Friday, October 28, 2011

Mtwara by Night

Mmoja wa mitaa ya mji wa Mtwara ukiwa ndani ya giza licha ya umeme wa uhakika mkoani humo- mipango miji wako wapi?

















Mkoa wa Mtwara ni moja kati ya mikoa michache nchini Tanzania isiyofahamu kadhia ya mgawo wa umeme. Mkoa haujaunganishwa kwenye mfumo mmoja wa taifa, hapa ni kwa faida ya wakazi wa Mtwara. Kwani hakuna maana kuwa chanzo cha umeme na usiupate umeme huo. Kwa Mtwara ni tofauti na maeneo yenye utajiri mkubwa ilihali watu wake hohehahe wa kutupwa.

Mkoani Mtwara kuna umeme utokanao na gesi asilia; gesi hii asilia inapatikana mkoni humu na hii inajidhihirisha kwa wakazi wa mkoani humo kwani hakuna mgao. Nafahamu kuwa hii ni hali ambayo wakazi wa mikoa mingi wangependa kuiishi. Na katika hali ya kawaida, ungetarajia kukutana na mitaa yenye kumulikwa vyema na taa nzuri za barabarani nyakati za usiku, lakini hali si hiyo. Nyakati za usiku mjini Mtwara kuna giza kubwa sawa sawa na mikoa yenye mgao wa nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya binadamu. Wazo kwa wahusika wakuu hususani wapanga maendeleo ya mji, wajipange na kuweka taa za barabarani katika mitaa ya mji huo wa kusini mwa nchi yetu ili kuupendezesha mji huo, kuongeza usalama wa mji na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi mjini humo.