Wednesday, February 12, 2014
Saturday, January 25, 2014
MASOKO YETU NA USAFI
Picha hii inaashiria mambo mengi na moja kati ya hayo ni uchafu. Hii ni sehemu rasmi ya kuhifadhia uchafu karibu na soko kuu mjini Mtwara. Sokoni, kama inavyofahamika, ni sehemu muhimu kwa binadamu kujipatia mahitaji yake muhimu. Soko kwa hakika ni eneo la lazima sana kwa maisha ya binadamu. Pamoja na shughuli zingine muhimu kwa mwanadamu; kula (chakula) ni moja kati ya shughuli za muhimu mno kwa binadamu. Katika hali ya kawaida binadamu ana hitaji kupata chakula kila uchao.
Chakula cha binadamu, hususani mijini, hupatikana sokoni. Kwa Mtwara hupatikana karibu kabisa na jaa hili kubwa la taka.Chakula huingia mwilini mwa binadamu na kuleta manufaa makubwa. Ili chakula kilete manufaa ni lazima kiwe katika hali ya usafi, vinginevyo kitaleta madhara makubwa kwa kiumbe huyu mwenye uwezo mkubwa wa fikra na mawazo mapya. Kwanini binadamu huyu, hususani wa Mtwara asitafute mawazo mapya ya namna kuhifadhi taka mbali na mahali pa kupata mahitaji yake ya kila siku?
Je, ni Mtwara tu ndo jaa la taka li karibu vile na soko? Nini kifanyike? Wataalamu wa mazingira, miji safi, mipango miji n.k watupatie mwongozo...
Monday, January 20, 2014
TAFSIRI PICHANI...
Picha hii ni kwa hisani ya GARY CAMERON- Newscon-RTR
Picha hii juu inawakilisha ukarimu wa Kiafrika, na hapa hasa, Kitanzania. Tukio hili lilikuwa ujio wa rais wa Marekani huko Afrika Mashariki na hususani nchini Tanzania.
Picha hii inaweza kuwa na malengo kadhaa. Mosi na lililo kubwa kabisa ni ukaribisho kwa rais Barack Obama na familia yake nchini Tanzania. Pili ni ustadi wa matumizi ya tamaduni, hapa kanga na kuwakilisha ujumbe na mchango wa kiteknolojia mahalia kwa dunia. Tatu Afya za Watanzania; ukitazama sawa sawa; utaona kuwa waliovalia kanga hizi ni kina mama wenye afaya njema. Picha hii inaweza kupotosha juu ya afya za watanzania. Kwa uhalisia Watanzania wengi, hususani kule vijijini, hawana afya inayowakilishwa na kina mama hawa wachache wa Dar es Salaam. Nne ni tabia ya uchafu na ama uchafuzi wa mazingira; utaona kina mama waliopendeza vilivyo ili hali hapo chini wametupa hovyo vyupa vya maji; bila shaka kwa kisingizio kuwa vyupa hivyo vitaokotwa na wahitaji kwa kuwa zahitajika sana siku hizi.
Msomaji unaweza kutoa tafsiri nyingine nyingi...
Thursday, January 2, 2014
JUA LA MWANZO KABISA TAZANIA 01/01/2014
Jua la Mwanzo wa mwaka 01/01/2014 |
Mkoa wa Mtwara unapatikana Kusini-Mashariki mwa Tanzania. Pamoja na Kilimanjaro ni mkoa mdogo kabisa kwa eneo. Mkoa huu unapatikana kusini-mashariki kabisa mwa Tanzania, kwahiyo jua nchini Tanzania, huanza kuonekana mkoani Mtwara. Hivyo picha hii japokuwa haina mwonekano mzuri sana, inaonyesha jua la mwanzo kabisa nchini Tanzania siku ya 01/01/2014
MTWARA MITAANI MWISHO WA MWAKA KAZI MTINDO MMOJA
Tuesday, December 31, 2013
SIKU YA MWISHO YA MWAKA - UJUMBE KWA VIJANA
Hatimaye
ni hakika sasa kila binadamu hai duniani na pia wafu wameongeza mwaka mmoja
toka kuzaliwa. Binadamu wote ila tu waliozaliwa tarehe 29 Feburuari. Ni hao tu
ndo wenye miadi na siku yao ya kuzaliwa kila baada ya miaka minne. Robo nne
zinapotengeneza kitu kimoja kizima. (Mwaka mfupi una siku mia tatu sitini na
tano na robo {365¼} na mwaka mrefu siku mia tatu sitini na sita {366})
Ukweli
huu wa maisha unawakilisha mambo yote duniani kila jambo limepata fursa ya
kukamilika; miezi yote imepata mzunguko wake, nyakati zote zimefikiwa, majuma
yote yamekamilika, saa zote, dakika zote, sekunde zote na kila jambo lenye
kutegemea mzunguko wa mwaka leo linakamilika.
Kupitia
mzunguko na kukamilika kwa mwaka ni jambo la kujiuliza pia sisi wenyewe. Binadamu
pia ana mabadiliko yake; yale ya kibaiolojia, seli mpya kuzaliwa na kuukuu
kupotea, kutumia / kutumika sawa sawa kwa ubongo: kujenga fikra mpya n.k. Kumbe
siku hii ya mwisho ni siku ya tathmini kwa yaliojiri maisha mwetu. Mimi Martin,
Amina, nimefanya jambo lipi la maana kwa
maisha yangu na binadamu wenzangu? Nimepanda miti? Nimegundua jambo jipya
muhimu kwa binadamu? Nimeandika kitabu cha maarifa na manufaa kwa wanadamu
wenzangu? Nimefanya jambo lenye kulinda uhai wa binadamu? Nimefanya nini kwa
nchi yangu, kwa dunia yetu? Naam ni lazima kujiuliza maswali haya, kila mmoja
ajiulize kwa namna yake mwenyewe. Kila mmoja wetu afanye kile mwafalsa wa
Ugiriki ya kale Socrates anavyopendekeza “maisha yasiyo na tathmini hayana tija”
{tafsiri yangu isiyo rasmi}. Tathmini hizi zinatuhusu binadamu wote, viongozi wan
chi duniani wahusika kwa kiasi kikubwa.
Wanasiasa
wana jukumu kubwa la kuongoza nchi zao. Wanasiasa wazuri wanaongoza vyema
wanasiasa wabovu wanaongoza hovyo. Watu hawa wana wajibu mkubwa zaidi kwa
wananchi wenzao. Wana wajibu wa kuongoza nchi zao na kuhakikisha wananchi walio
wengi wananufaika na mali asilia nchini mwao. Rais wa Marekani, mmoja kati ya
mifano mizuri mwaka huu, amepigania kuboresha maisha ya Wamarekani wengi wa
kawaida kwa kuboresha huduma zao za afya; moja kati ya mahitaji na haki muhimu
ya binadamu. Kufanikisha jambo hilo kulihitaji ujasiri mkuu. Kwenye mlolongo
huo wa siasa kuna mengi yamefanyika kote duniani; masuala anuwai mazuri kwa
mabaya. Nchi nyingi hususani barani Afrika zimekumbwa na shida za kisiasa.
Nchini
Mali kulitokea uasi ambao ulivuruga maisha na ustaarabu wa siku nyingi wa moja
kati nchi zenye historia yenye kubeba bara lenye nchi nyingi zaidi duniani.
Afrika ya Kati maisha bado hayajarejea hali ya kawaida kufuatia uroho wa
mamlaka na dhambi ya ubaguzi inayoendelea kuwatafuna wanasiasa wa nchi hiyo
yenye kubeba sawia jina lake na mahali ilipo. Misri, nchi yenye utajiri wa historia
na kumbukumbu mahususi za maendeleo ya kale haikubaki salama na bado
kunaendelea kuwa na chokochoko baina ya makundi hasimu. Jamhuri ya kidemokrasiaya Kongo iliendelea kuwa kwenye hali ya sitofahamu hususani mashariki mwa nchi
hiyo tajiri kwa maliasili na ukubwa wa eneo barani. Ni dhahiri kuwa kila nchi
ilikumbana na masuala anuwai ya kupendeza na yasiyo ya kuvutia, changamoto na
fursa za kimaendeleo. Nchi kadhaa zimeendelea kusheherekea jubilei za miaka
hamsini na zaidi. Tanzania na watanzania kwa mara ya kwanza walipata fursa ya
kuchangia mchakato wa kuandaa sheria mama za nchi yao ama nzuri zaidi
makabrasha ambayo ni mali ya wananchi, mkataba baina ya wananchi wa viongozi. Mkataba
huo maarufu zaidi katiba ni muongozo wa
namna viongozi: watu ambao hutoka miongoni mwa wananchi na hukabidhiwa mamlaka
ya/ na wananchi, ili waufahamu na waelewe ni namna ipi inawapasa kuwatumikia
wananchi. Zoezi la kuandaa mkataba huo kwa mara ya kwanza nchini Tanzania,
lilishirikisha/ linashirikisha wananchi wote ama moja kwa moja ama kwa njia ya
uwakilishi, ni jambo jema. Wafaransa, waanzilishi wa Jamhuri, kupitia mapinduzi
yao maarufu, wana msemo: “hucheka vyema zaidi anayecheka mwishoni” Tunawaombea
watanzania wapate mkataba/ katiba yenye uzalendo hasa wa watu hao. Mwishoni AfrikaKusini, bara Afrika na dunia iliondokewa na Nelson Mandela.
Nelson
Mandela: mtu ambaye alipata umaarufu mkubwa kupitia mambo kadha wa kadha:
kifungo chake kwa kuipinga serikali ya ubaguzi rangi nchini mwake, kung’atuka
madarakani kisha muhula mmoja wa uongozi, kufanya maridhiano badala ya kulipa
kisasi nchini mwake, kupata nishani ya Nobel, kutambuliwa mno na vyombo habari
vya magharibi n.k. Kifo, heshima ya kitaifa na kisha mazishi ya kitaifa ya Nelson Mandela al maarufu
Madiba ilikuwa ni tukio kubwa la kidunia. Viongozi mashuhuri walifika kwenye
kumuaga ndugu huyo ambaye ni sehemu ya wanaAfrika waliotoa mchango mkubwa wa
kizalendo kwa bara hili: Mwalimu JK.Nyerere, Dr.Kwame Nkrumah, Dr. KenethKaunda, na wengine lukuki. Kwa Madiba pengine maneno ya Sauli ama Paulo kwa Warumi
5: 3-5 yanaweza kufaa sana hapa. Kwa sasa tuishie hapa. Lakini kwa ujumbe kwa
vijana.
Mwaka
unapokwisha si kitu cha ajabu sana kwa maana ya kuja kwa jambo jipya kabisa ni
mzunguko ule ule wa Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na
Jumapili. Kwa kuwa mzunguko ni ule ule nawaalika vijana kutafakari juu ya
malengo ya maisha yenu/ yetu. Nini hasa unataka kufanya duniani: kukusanya mali
za dunia yote, “itakufaidia nini kupata mali zote na kisha kupoteza nafsi yako”
Maneno ya Mmisionari mmoja. Maneno na tafakari hii ni muhimu kwa vijana kwani
mwaka huu tumesikia lukuki (hatuna takwimu hapa) wakikamatwa na dawa za kulevya…Kukusanya mali na tena kuvumbua njia nyingi iwezekanavyo za kukusanya mali lakini kwa njia halali ni muhimu vyema lakini tusisahau pia kuwa mwili ni mmoja lakini wenye mahitaji ya kiroho pia...
Wasalaaam,
Wasalaaam,
Thursday, December 26, 2013
SIKU YA KUFUNGUA MAKASHA YA ZAWADI
IMEPAKULIWA HAPA : https://www.youtube.com/watch?v=L99hWdZGelI
Siku moja baada ya Noeli imekuwa, kimapokeo, ni siku ya kufungua makasha ya zawadi. Soma hii taarifa inaonyesha kuwa kazi ya kupokea makasha ya zawadi ni ya wafanyakazi nyumbani, Makasha ya zawadi hupokelewa kabla ya siku husika na leo kazi inakuwa moja tu ya kuyafungua makasha hayo kutaka kujua kuna nini humo ndani. Utamaduni wa kupeana zawadi siku za matukio maalumu ni jambo na utamaduni mzuri.
Jambo hili ni sehemu ya tamaduni za jamii nyingi duniani, na kama si sehemu ya tamaduni zetu basi ni jambo la kuiga na ni vyema tukafanya hivyo kwa wale tusio na utamaduni huo. Kufanya hivyo kunaendeleza na kujenga udugu, umoja, upendo n.k katika jamii.
Kupitia utamaduni wa kupeana zawadi tujifunzie hapo hapo pia kutoa misaada kwa wahitaji bila kujali mahusiano yetu ya kindugu. Kwa asili binadamu wote tu ndugu wamoja. Asili, chimbuko letu wote; kidini, kibaiolojia/kisanyansi ni moja. Hivyo tunawajibika kusaidiana. Kwa wale wenye makasha mengi ya zawadi tuwakumbuke wahitaji wasio na msaada wa karibu; yatima, wajane, wagonjwa na wengine wote wenye kuhitaji katika jamii.
Thursday, October 31, 2013
Maonesho ya WajasiriaMali Mtwara
Maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiria mali kutoka pande mbalimbali za nchi na nchi jirani yamenza mjini Mtwara. Maonesho hayo yaliyoandaliwa na SIDO na wadau wenzi, yanalenga kuonesha bidhaa anuwai zitengenezwazo na wabunifu na pia kutafuta masoko toka kwa wadau. Mkoa wa Mtwara, ambao umesikika masikioni mwa wadau wengi hivi karibu kufuatia kugunduliwa kwa gesi asilia, unaanza kuwa moja ya masoko makubwa tarajiwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maonesho haya ambayo yamefunguliwa rasmi na ndugu mwenye dhamana ya viwanda vya Tanzania, ni fursa nzuri ya kuweza kuonesha bidhaa na mwanzo mzuri ya viwanda vyetu wenyewe kuanzia hatua za mwanzo kabisa. Kupitia wadau hawa wa bidhaa hizo ndogo, Taifa linaweza siku za usoni, kama tutaweka mkazo wa kutosha, kuwa na viwanda vyake lenyewe. Ili tuweze kufikia ndoto na lengo hilo ni muhimu kutengeneza mazingira ya kuwawezesha wajarisiliamali wetu kutengeneza bidhaa zao kwa gharama nafuu. Gharama za uzalishaji ikiwa ni pamoja na mali ghafi zikiwa na bei ya chini, itawezesha wadau wengi kujiajiri na bidhaa zao zitakuwa na bei ya chini.
Nasema hivyo kwa kuwa baadhi ya bidhaa nilizoziona zinauzwa kwa bei kumbwa mno ukilinganisha na ubora wake. Bidhaa nyingi ni za asili kabisa na hivyo kuwa imara ukilinganisha na zitangenezwazo na makanjanja mjini, japokuwa ubora wake unahitaji kuongezwa zaidi ili zivutie wanunuzi wengi zaidi. Nilipohoji juu ya bei mmoja wabunifu wa bidhaa alisema: "nalazimika kuuza kwa bei ya juu kwa sababu nalipia kodi na ushuru mbalimbali na pia kwa kuwa hakuna watazamaji wengi nauza bei ya juu ili kupitia mauzo haya nijikimu hapa mjini". Baadhi ya wadau hawa wa bidhaa asilia waliomba waandalizi wa maonesho haya wafikilie kuwalipia baadhi ya gharama ili kumudu vyema zaidi maonesho hayo. (Mwandishi hakupata fursa kuongea na timu ya maandalizi juu ya suala hili)
Wakazi wa mjini Mtwara, hawajahamasika vya kutosha kutembelea maonesho hayo, jambo ambalo lingewezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao na kumudu kujikimu kupitia mauzo hayo. Hata hivyo ni fursa kwa wenyeji wa mkoa huo kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na maisha na utawala wa mazingira ya binadamu.
Kwa wajasiria mali, napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazozifanya, ila nawashauri pia waweke vitambulisho vya nchi zao wanakotoka ili kutambulisha bidhaa zao na pia kuzitambulisha nchi zao kibiashara zaidi. Hili linajumuisha kundika kwenye bidhaa jina la nchi bidhaa ilikozalishwa, kundika anuani ama utambulisho uliojitosheleza ili mdau husika apatikane kwa wepesi kokote duniani. Ni muhimu kufanya hivyo kwani dunia imekuwa ndogo mno kupitia mapinduzi ya mawasiliano ulimwenguni.
Thursday, September 12, 2013
Thursday, July 25, 2013
SIKU YA MASHUJAA NA UZALENDO TANZANIA
Sehemu ya wanajeshi wa Tanzania wakitoa heshima kwa Amiri Jeshi mkuu wa majeshi. Picha kwa hisani ya BBC |
Tarehe ya leo imeteuliwa kuwa siku ya mashujaa Tanzania. Ni tarehe waliyopokelewa wanajeshi wetu- mashujaa waliokuwa vitani nchini Uganda. Wanajeshi wetu walikwenda kazini kumnyoosha nduli Iddi Amini. Rais huyo wa zamani wa Uganda aliyejigamba kuwa na nguvu za kuchukua sehemu ya Ardhi ya Tanzania na kuifanya kuwa sehemu ya nchi yake. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999), kwa kutumia vigezo vya "vita halali" just war ya St. Augustine of Hippo 354-430 alitangaza vita kwa kuzingatia sababu inayokubalika, kujilinda dhidi ya adui, na kupigana vita kwa uangalifu na kupunguza maumivu kwa wasio na hatia. Vijana wa jeshi la Tanzania na nchi yote kwa ujumla tulishinda.
Tunapokumbuka mashujaa wetu, watu wengi hufikiria tu wanajeshi na wapiganaji wengine waliolipigania Taifa letu. Hapa utakumbuka watawala kama Mkwawa, Kimweri, Mirambo, Mputa, na wengine wengi. Ni vyema sana kuwakumbuka ndugu waliokuwa tayari kulilinda Taifa letu. Muhimu katika kumbukumbu hii ni suala zima la uzalendo. Watu wote tunaowatambua kama mashujaa, kwa namna fulani walikuwa na uzalendo mioyoni mwao. Hawa ni sawa na watu tunao watambu kama watakatifu, watakatifu huitwa wadhambi waliotubu. Nawafananisha mashujaa katika nchi na watu wenye "utakatifu" unapowapima kwa vigezo vya uzalendo. Kumbe tunapowaheshimu mashujaa wetu ni lazima tujitazame na kujipima uzalendo wetu.
Mzalendo tunamtarajia kuwa mtu mwenye kuipenda kwa moyo wake wote nchi yetu ya Tanzania. Katika hili kila mmoja na hasa wenye ofisi za Umma ama zozote zenye kutoa huduma kwa umma wa wanadamu, wanaalikwa kujipima, wanajali kwa kiasi gani maslahi ya wananchi walio wengi dhidi ya maslahi binafsi. Kiongozi anapopata fursa ya uongozi anatakiwa kufanya hivyo kwa niaba ya wananchi walio wengi; na ili aongoze vyema kuna mkataba unaomwelekeza kama anavyosema mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau(1712-1778) kwenye kazi yake ya The Social Contract (1762), kiongozi anafanya yale anayoelekezwa na wananchi na si anayotaka yeye; viongozi wangapi hivi leo hapa nchini wanazingatia anachosema mwanafalsa huyu. Wengi hawafuati makubaliano baina yao na wananchi, na kwa hivi wanalazimika kuacha mamlaka kwa wananchi wengine ili waongoze kama anavyosema mwafalsafa mwingereza John Locke (1632-1704). Locke anasema kiongozi mzuri anatakiwa awe na kumbukumbu ya makubaliano yake na wananchi moyoni mwake, vinginevyo aachie mamlaka.
Hivyo basi tunaweza kuwaenzi vizuri zaidi mashujaa wetu kwa kujitazama katika kioo na kuona kiwango cha uzalendo wetu kwa Tanzania yetu. Asanteni Mashujaa wetu na Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!
Thursday, July 18, 2013
SIKU YA MZEE MADIBA
Nadhani hii ndo siku pekee ambayo binadamu mmoja amepewa heshima ya kuwa na siku yake ya kimataifa duniani. Ndugu Nelson Mandela kapewa heshima hiyo hasa kwaajili ya kumaliza kwa amani, kupitia tume ya haki na maridhiano, mvutano ambao ungejitokeza baina ya weusi wengi, na jamii nyingine za watu wasio weupe wa asili ya Ulaya kwa upande mmoja, na wazungu wa asili ya Ulaya kwa upande mwingine.
Suluhu hiyo iliyohitimisha miaka mingi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kwa utulivu wa namna yake, ndo hasa sababu ya mzee Mandela kupewa heshima yote hiyo.
Saturday, June 29, 2013
Saturday, June 1, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
National Arts Council BASATA
30/05/2013
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) kila Jumatatu kuanzia saa 4 Asubuhi limekuwa likiendesha ‘Jukwaa la Sanaa’ kwenye ukumbi wake ulioko makao makuu ya Baraza Ilala Sharif Shamba.Katika jukwaa hilo linalohusisha wadau wote wa sanaa, hoja nzito na motomoto kuhusu tasnia ya Sanaa na Utamaduni zimekuwa zikijadiliwa na kujibiwa.
Katika kuelekea urasimishaji wa Sekta ya Filamu na Muziki ambao ulianza rasmi tarehe 1/01/2013, ifikapo tarehe 01/07/2013 hakuna kazi yoyote ya Filamu na Muziki itakayoingia sokoni bila kuwa na stamp ya TRA. Baraza la Sanaa katika Jukwaa la Tarehe 03/06/2013 litazikutanisha taasisi zote nne zinazohusika na urasmishaji ili kutoa elimu kwa Wasanii, wadau na wakuzaji sanaa kuanzia saa 4 :30 Asubuhi. Wadau wa sekta ya sanaa mnakaribishwa kuleta michango na hoja zenu ili kuleta mustakabali utakaojenga sekta ya sanaa. Taasisi zinazohusika na Urasimishaji wa sekta ya sanaa ni :
1. Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza
2. Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (COSOTA)
3. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
4. Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
WOTE MNAKARIBISHWA
Godfrey Lebejo Mngereza
KAIMU KATIBU MTENDAJI, BASATA
Barua zote ziandikwe kwa Katibu Mtendaji
All correspondence to be addressed to The Executive Secretary
BASATA Arts Centre, Ilala Sharif Shamba, P.O. Box. 4779, Dar es Salaam, Tanzania.
Telephone: 2863748/2860485, Fax: 0255 - (022) - 286 0486 E-mail: info@basata.or.tz Website: basata.or.tz
Salaam za Rambirambi
Baraza la Sanaa la Taifa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii wa tasnia ya Muziki nchini Albert Mangwea a.k.a Ngwair.
“ Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Ngwair ambaye mchango wake unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wao bado unahitajika katika tasnia hii.” Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini, aidha linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.
Tunaomba mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, tutambue kuwa haya ni mapenzi ya Mungu.
Imetolewa na
Ghonche materego
Katibu Mtendaji
Baraza la Sanaa la taifa.
Monday, May 13, 2013
KAZI NI MOJA TU SASA
Wanazuoni wa mwaka wa tatu chuoni STEMMUCO kwa juma la pili sasa wamekuwa wakitetea tafiti zao walizofanya kwa mieza kadhaa. Tafiti hizo, ambazo ni sehemu ya wajibu wao ili kupata sifa ya kupata shahada yao ya kwanza, (degree ya kwanza) zilikuwa na mada tofauti tofauti kama jinsi walivyo watu na miguso yao.
Baadhi ya kazi zilihusu mchango wa Chuo Kikuu cha STEMMUCO kwa maisha ya watu wa Mtwara kwa ujumla wake, zingine na nyingi hasa zilihusu masuala kadhaa ya elimu. Kwanini shule za Mtwara ubora wake wa elimu ni hafifu, kwanini shule za serikali ubora wake mbele ya zile za binafsi ni dhaifu n.k. Zingine zilihusu shughuli za kiuchumi mkoani Mtwara; uzalishaji chumvi na athari zake, mchango wa bandari Mtwara kwa wananchi. Kazi za wanazuoni wengine zilitazama masuala ya kijamii; kuongezeka kwa watoto wa mitaani, Unyago, jando na faida, hasara na changamoto zake. Mazingira pia hayakuachwa nyuma; tafiti kadhaa zimegusia suala hilo. Uhalifu ni moja ya mada zilizojadiliwa hali kadhalika.
Zoezi hili lilifanywa kwa lugha ya kiigereza; vijana wengi walijipanga na kutafuta misamiati stahiki kuelezea kazi zao; wapo waliofanya vyema sana, waliojitahidi sana na wanaohitaji kuongeza bidii zaidi. Kwa ujumla wanazuoni hawa ni hazina kubwa kwa taifa na wito kwao ni kuendelea na moyo wa kitafiti ili kuvumbua vyanzo vya matatizo na kuyafanyia kazi.
Subscribe to:
Posts (Atom)