Thursday, January 7, 2016

DHANA YA KUTUMBUA MAJIPU IMETOKA WAPI?

Picha kwa hisani ya mtandao
imepakuliwa hapa:https://www.youtube.com/watch?v=xCjZLhxsOcA
Wakati wengi wetu tukiendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ndugu JPMagufuli kwa kushughulikia vilivyo matatizo yanayoisibu nchi, wachache tu kati yetu tumejiuliza kwanini kaamua kutumia dhana hiyo aliyoichagua kutatua matatizo yanayoikumba nchi Dr JPM ameamua kutumia dhana ya kutumbua majipu kama kiwakilishi cha utatuzi wa matatizo mazito, sugu na yaliyo kero kubwa kwa wananchi wa Tanzania. Wengi wetu tuliisikia kauli na dhana hiyo siku alipoongea na wabunge wa bunge wa la Jamhuri ya Muungano siku ya uzinduzi wa bunge.

Kupata jibu kwanini aliamua kutumia dhana hiyo, kuna njia kuu mbili; ya kwanza ni kumuuliza yeye mwenyewe ndugu JPM na ya pili ni kuutumikisha ubongo kufanya shughuli hiyo. Njia ya kwanza japokuwa ni fupi, nyepesi na inatoa jibu sahihi, si njia tunayoitamani. Hatuitaki njia hiyo kwakuwa haijengi uwezo wa kufikiria kwa namna sahihi. Ila hali njia ya pili ni ndefu, inashughulisha, inaimarisha uwezo wa ubongo, inakomaza uwezo wa ubunifu na kadhalika. Zaidi njia hii ya pili inachosha lakini hasa ndiyo tunapaswa kuifuata kwa kuwa inazalisha faida nyingi zaidi mbali ya jibu ambalo huenda lisiwe sahihi licha ya kutumia muda mrefu kulipata. Hiyo ndiyo hasa kazi ya falsafa; kujenga uwezo kuuliza maswali sahihi na kupitia njia sahihi za tafakari kujenga fikra sahihi ili hali ikiwa ni kutafuta UKWELI.

Tukirejea kwenye swali letu la msingi je kwanini JPM ametumia dhana ya kutumbua majipu? Ama ametoa wapi dhana hii? Katika falsafa na jinsi ninavyoamini pia kila kitu tumekipata maishani, ama tumekiishi sisi wenyewe, ama tumeona kwa wengine, ama tumesikia, ama kuhisi toka kwa wengine, ama kwa ufupisho huyapata mambo haya kupitia milango yetu ya fahamu za hisia (kuona, kusikia, kunusa, kuhisi na kuonja) haya ndiyo mafundisho ya wanafalsafa kadhaa wakiongozwa na Aristotle. Kwa upande wa wale wanaoongozwa na Plato; mwalimu wa Aristotle na mwanafunzi wa Socrates, wao wanaamini kuwa tuliishi sehemu nyingine kabla ya kuja hapa duniani na hivyo tulifahamu mambo yote huko tulikoishi. Hivyo mambo yote tunayofanya hivi sasa ikiwa ni pamoja na elimu ni juhudi tu za kujikumbusha tuliyoyaishi hapo kabla katika ukamilifu wa maisha. Unaweza kutumia mtazamo wowote kati ya hii miwili kupata jibu. Kwa Makala hii/haya twatumia mtazamo wa kiAristotle kupata jibu na hivyo ndugu JPM katumia dhana ya kutumbua majipu toka kwenye Hasina ya kumbukumbuu zake.
google image

Kwahiyo basi dhana ya kutumbua majipu ndugu JPM ama ameiishi yeye mwenyewe, ama kaishuhudia kwa mtu mwingine, ama alipata kusimuliwa juu ya dhana hiyo na mtu mwingine. Pengine kabla ya kuendelea tujiulize kwanza jipu ni nini? Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Dar es Salaam (TUKI), jipu ni uvimbe mkubwa unaotunga usaha. Na usaha ni ute wa rangi y manjano iliyopauka unaotunga aghalbu katika vidonda na majipu. Kamusi hii inaeleza tu maana ya jjipu na usaha. Lakini katika uhalisia wa maisha jipu ni adha inayousumbua mwili na kuufanya ufanye kazi zake kwa taabu. Zaidi uvimbe huu mara nyingi, bila shaka kuna sababu za kitabibu, huvimba maeneo yenye kumkosesha Amani na kumpatia binadamu usumbufu uliokithiri. Unaweza kukuta jipu limempata mtu kwenye makalio, mgongoni, sehemu zake za siri na kadhalika. Fikiria mtu mwenye kazi ya inayomlazimu kuketi muda mwingi, apatwe na jipu kwenye makalio…bila shaka unapata picha ya adha kubwa ndugu huyo atakayoipata.

google
Mtu huyo anahitaji matibabu ya haraka ili aendelee na kazi zake ili kutumia vipawa vyake,  kuitegemeza familia, jamaa zake, na taifa lake, kinyume na hapo familia jipu litamhangaisha na familia yake itaathirika, nchi itakosa mchango wake wa kimaendeleo. Kuepuka yote hayo mgonjwa anakwena hospitali kutumbuliwa jipu hilo. Kutumbua jipu hilo ni moja ya njia za kutibu uvimbe huo, nyingine inaweza kuwa vidonge vya kupunguza uvimbe na hatimaye kuisha. Kati ya njia hizi mbili, madaktari wanaweza kutujuza kama zipo njia nyinge murua zaidi yaa hizi mbili, ile ya kutumbua jipu ni bora zaidi kwa kuwa njia hii huasaidia kuondoa pia kiini cha jipu na hivyo kuzuia jipu hilo kuhamia sehemu nyingine ya mwili.

Hivyo basi utaona kuwa dhana ya Rais Magufuli ya kutumbua majipu imejengwa toka katika uhalisisa wa maisha yanayofahamika kwa watu wengi. Hivyo umithirishaji wa matatizo yanayoikumba jamii ya watanzania na tatizo la majipu mwilini ni dhana inayoeleweka kwa urahishi na hivyo inaweza kuimarisha na kuhamasisha uungwaji mkono na ushiriki wa watanzania wengi zaidi katika jitihada za kutumbua majipu (juhudi za kutatua matatizo yanayowaumiza wananchi na kubana fursa zao za kujiletea maendeleo). Kwa hiyo basi ndugu JPMagufuli huenda akawa anatumia dhana hiyo kwa kuwa anafahamu kero za majipu mwilini na jinsi ambavyo huwa kero kubwa na kubana fursa za mhanga kufanya shughuli zake za kila siku. 


Mandalu

No comments:

Post a Comment