Monday, July 18, 2011

Siku ya Nelson Rolihlahla Mandela

Leo Jumatatu, 18 Julai ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya Kidemokrasia (18.07.1918). Kadri ya kumbukumbu zangu huyu ndiye mtu pekee ambaye Umoja wa Mataifa umemtengea siku katika mwaka mahususu kwa heshima yake. Hivi leo anatimiza miaka 93 toka azaliwe; ni mmoja kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameishi kwa muda mrefu.

Nelson Mandela ni mtu anayepewa heshima kubwa duniani kote kwa wanaomfahamu na hata wasiomfahamu. Watu wengi hasa nje ya Afrika hususani katika jamii zinazopenda kusoma vitabu wamfahamu kupitia kitabu chake cha "Long Walk to Freedom". Hiki ni kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake kwa kina kabisa. Sehemu kubwa ya kitabu hicho ameiandika yeye mwenyewe na tena akiwa gerezani. Hili ni moja ya mambo ya kujifunza toka kwa mzee huyu-maktaba kubwa duniani kote. Tujipange tuandike historia zetu sahihi ili kuiachia jamii na dunia kwa ujumla utajiri wa mawazo kama alivyofanya mzee Mandela. Wengine tulimfahamu mzee Madiba toka enzi za utoto; tukiwa shule ya msingi tuliimba nyimbo za kutaka Mandela achiwe huru na serikali ya makaburu. Utawala wa makabulu ulitawala Afrika Kusini kwa mabavu na kwa misingi ya kibaguzi ya rangi za binadamu; ni udhalimu wa aina yake kwa ustawi wa wanadamu.

Kwanini mzee huyu ni maarufu vile?
  
Kwa hakika sifahamu yote juu ya mzee huyu anayependwa mno si tu kwake huko Afrika Kusini bali pia duniani kote kwa ujumla, hilo ladhihirika kwa Umoja wa Mataifa (UM) kumtengea siku maalum kumuenzi.
Mandela, ambaye kipindi fulani Marekani ilimchukulia kama gaidi soma makala hii (http://faithinactiononline.com/2008/07/nelson-mandela-freedom-fighter-or-terrorist/,) alifungwa katika magereza tofauti kwa jumla ya miaka 27; umri wa kijana aliyekomaa. Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa pia Mwanasheria, mwanamichezo na mpigania haki za watu, alifungwa na serikali ya Makaburu kwa walichokiita uhaini. Nelson Mandela moja ya vijana walionzisha madai ya uhuru kwa njia ya mapigano alikuwa na imani kuu juu ya haki sawa kwa watu wote. Aliamini na anaamini kuwa binadamu wote ni sawa katika misingi ya ubinadamu- kwa haki na mahitaji yetu. Ni kwa imani na msukumo huo wa kudai uhuru na haki za watu wote wa Afrika Kusini ndo alikuwa tayari kudai haki hizo hata kama ingemlazimu kuyatoa maisha yake; funzo kubwa hilo.

Kwa hakika imani juu ya haki sawa kwa watu wote ni funzo na changamoto kubwa kwa viongozi wote duniani. Nini imani yako wewe kiongozi juu ya haki sawa kwa wananchi unaowaongoza? Ni dhahiri kuwa unatambua kuwa wananchi wako wote wanahitaji chakula cha kutosha, makazi, huduma muhimu za kijamii; afya, elimu, na kadhalika (nk). Lakini tunacho kishuhudia hii leo ni ubinafsi mkubwa wa viongo na hata wananchi wengine wenye nafasi bila kujali mahitaji ya wengine wenye haja ya vile vitu tu vya msingi. Wasomi wengi katika nchi zetu za zinazoendelea tunahangaika na mahitaji ya ziada ila hali kuna wenzetu wengi tu wasio na mahitaji yao ya lazima. Tukita kutambulika vyema hapa duniani ni lazima tujifunze kwa mzee Mandela kujisahamu kwaajili ya wengine.

Baada ya kuachiwa huru mwaka 1990 alirejea kwenye harakati za kudai haki za Waafrika Kusini walio wengi. Mwaka 1991 alichaguliwa rais wa "African National Congress" ANC http://www.anc.org.za/showpeople.php?p=19. Mandela alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya kidemokrasia mwaka 1994. Alitumikia muhula mmoja tu wa miaka mitano na mwaka 1999 kuacha mamlaka  ya dola kuu kabisa kiuchumi barani Afrika. Utaona kuwa Mzee Madiba alifanya kinyume kabisa na viongozi wengi wa barani mwetu. 

Suala kuu ambalo dunia imejifunza toka kwa mzee huyu wa miaka 93 sasa ni moyo wa msamaha. Kumbe hata kwa binadamu msamaha unawezekana. Msamaha huu umeongozwa na busara kuu bila shaka na neema tele za Mwenyezi Mungu. Rais Nelson Mandela angeweza kabisa kulipa kisasi cha Waafrika Kusini weusi wengi waliopoteza maisha kwenye harakati za kujikomboa, lakini hakufanya hivyo, alisamehe na badala yake aliwaunganisha wananchi wote wa Afrika Kusini mpya, ingawa kuna vidonda vingi na makovu watakayoishi nayo daima, na kuanza kuijenga nchi yao kwa manufaa yao wote. Hii ni changamoto kuu kwa wanadamu wote - nadhani ni sababu hii hasa ndo imeulazimu Umoja wa Mataifa kuanzisha siku mahususi kumuenzi mpigania haki za binadamu Nelson Mandela Madiba. Kwa hakika Madiba ni mjenga dunia!!!


Picha kwa hisani ya Mjengwa blogu!   

No comments:

Post a Comment