Tuesday, August 7, 2012

BASATA LAKERWA NA WASANII KUNG’ANG’ANIA FILAMU NA MUZIKI PEKEE

BASATA LAKERWA NA WASANII KUNG’ANG’ANIA FILAMU NA MUZIKI PEKEE


Na Mwandishi wa BASATA

Sehemu ya wadau waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa
wiki hii wakifuatilia kwa makini programu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kusikitishwa na hali iliyopo sasa ya wasanii kuzipa kisogo Sanaa zingine na kung’ang’ania filamu na muziki pekee hali inayowafanya wengi wao kubaki wakihangaika na kulalama.

Akizungumza wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika makao makuu ya Basata, Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego alisema kuwa, ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakifunga milango yote katika sekta ya Sanaa na kubaki wakihangaika na madirisha mawili tu ya filamu na muziki.

“Ndugu zangu hebu tujiulize tu, Sanaa ni pana sana na ina fursa nyingi katika kutupa ajira na kuzalisha kipato kwa vijana wengi lakini kwa nini wote tunang’ang’ana na filamu na muziki pekee? Fursa nyingine tunamwachia nani? Alihoji Materego.

Monday, August 6, 2012

Wabunge ‘wala’ rushwa marufuku kuingia China

Bunge la Tanzania Mjini Dodoma















Tumeambiwa na tunafahamu siku zote kuwa rushwa ni adui wa haki, na ni ya wananchi, ya binadamu, ama ya viumbe vilivyo hai walau kulingana  na miongozo na makubaliano yetu. Moja ya makubaliano hayo, kwa Tanzania ni kuwa rushwa ni adui wa haki, na kwenye kanuni/ ahadi za mwanaTANU (chama kilichopigania uhuru wa Tanganyika) kulikuwa na ahadi ya kutotoa na kutopokea rushwa kwani hupinga ama huzuia watu wengine kupata haki zao.

Katika nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwa mojawapo, kuna utaratibu wa kuwa na chombo cha kutolea mawazo, kuihoji serikali iliyo madarakani, kutunga sheria n.k. Chombo hicho kinafanya kazi kwa uwakilishi; si rahisi kwa mwananchi mmoja mmoja kuingia katika chombo hiko kutetea, kudai haki yake ama/ na kufanya shughuli zingine za chombo hicho ambazo kwetu kinajulikana kwa jina la BUNGE. Kwa kuwa si rahisi wote kuingia basi tumelazimika kuwa na wawakilishi wachache ili wawe SAUTI zetu na waseme na kutenda kwa niaba yetu. Hivi karibuni tumesikia habari ya kushangaza juu ya hawa wawakilishi wetu. Tumesoma na kusikia vyombo vya habari vikielezea juu ya baadhi ya wawakilishi wetu hawa wakifanya kile tulichofundishwa kuwa ni adui wa haki, sio lengo la makala hii kuongelea suala hilo bali tu kuiwasilisha makala iliyo katika gazeti la MTANZANIA inayoeleza juu ya kicha habari.   

Mwalimu JKNyerere aliwahi kusema IKULU ni patakatifu nadhani BUGENI halikadhalika ni vivyo hivyo. Je, kama kweli kuna wabunge wameenda kinyume na utakatifu inafaa kweli waendelee kuwepo patakatifu?

Na Arodia Peter .

TUHUMA za rushwa zinazoendelea kuwaandama wabunge, zimechukua sura mpya, baada ya Serikali ya China kujiandaa kupiga marufuku wabunge wote wanaotuhumiwa kujihusisha na rushwa kuingia nchini humo.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata kutoka ubalozi wa China hapa nchini, zinasema umepokea taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wakuu wa China, wafuatilie kwa karibu wabunge wote wanaotuhumiwa kwa rushwa, kisha watume taarifa ili wakibainika wasiingie kwenye nchi hiyo.
“Tumeletewa taarifa na viongozi wetu wa ngazi za juu, kuwa tufuatilie kwa kina wabunge wote ambao wanatuhumiwa na wakibainika majina yao yatumwe China, ili wazuiliwe kuingia kule,

…unajua taifa letu ni taifa ambao halina mchezo na mtu anayepokea rushwa ovyo ovyo na ni kosa la jina. kwa kiongozi kama hawa wabunge kujihusisha na siasa,

“Kwa kipindi chote hiki, kama wabunge hawa wangekuwa China leo hii, tungekuwa tunazungumza mambo mengine, wangekuwa wamechukuliwa hatua kali,

“Tunashangaa kuona kwa nini hapa kwenu, bado wanaendelea kuruhusiwa kuingia bungeni… au wanasubiri majibu ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizi,” kilihoji chanzo chetu.

Chanzo hicho, kilisema ubalozi wa China hapa nchini, umetuma maofisa wake mjini Dodoma kwa ajili ya kupata mwenendo wa wabunge wote wanatuhumiwa.

“Hivi sasa hapa Dodoma kuna maofisa wa ubalozi wa China, wanaendesha uchunguzi kuhusu tuhuma hizi, ikibainika ni za kweli baada ya majina ya wabunge ‘wala rushwa’ kutajwa, watachukua picha zao kwa ajili ya kuzituma China, ambako hawataruhusiwa kukanyaga kwa sababu kwao rushwa ni kosa la jinai,” kilisema chanzo chetu.

Naye Mratibu wa maombi yanayoendeshwa na Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania, mjini Dodoma Mchungaji William Mwamalanga alisema kwa kauli moja viongozi wa dini, wamesikitishwa na tuhuma hizo.

Alisema viongozi wa dini ambao wamepiga kambi mkoani Dodoma, kwa ajili ya kuliombea taifa, wamewataka wabunge wote waliotajwa wajiuzulu mara moja.

“Viongozi wa madhehebu mbalimbali tupo hapa Dodoma, kwa ajili ya kuliombea taifa, lakini moja ya jambo kubwa ambalo tumekubaliana kupita katika majimbo yao, kueleza waumini wetu matatizo haya ya rushwa… tunataka wajiuzulu kwa ajili ya kulinda heshima zao,  

Saturday, July 28, 2012

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU KUGOMA


SERIKALI kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Ijumaa, Julai 27, 2012 majira ya saa tisa alasiri, imepokea notisi ya saa arobaini na nane (48) ya kusudio la walimu wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma kuanzia Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 saa moja na nusu asubuhi.

Kabla ya notisi hii kutolewa, Serikali imekuwa ikifanya jitihada nyingi za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi ya kuboresha maslahi ya walimu kwa nia ya kumaliza suala hili kwa maelewano kwa kutumia vyombo na ngazi mbali mbali za kisheria.

Kwa sasa, shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii siku ya Ijumaa tarehe 27 Julai, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili zilifika Mahakamani, na Mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne tarehe 31 Julai, 2012 saa sita mchana, ili kuiwezesha Mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi.

Kwa hiyo, Mgomo huu siyo halali kwa sababu shauri hili bado liko Mahakamani.

Kwa msingi huo hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za Kimahakama ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.

Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa kujihusisha na mgomo huu ni kwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi. Hivyo, walimu wanapaswa kupima madhara ya mgomo huu usiokuwa halali na Serikali inawataka walimu kupuuza mgomo huo na kutokujihusisha nao. Walimu wote wanatakiwa waendelee na kazi kama kawaida.



Peniel M. Lyimo
KAIMU KATIBU MKUU KIONGOZI
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Julai, 2012

Tuesday, July 17, 2012

MKUTANO WA WAKUU AFRIKA WAMALIZIKA


Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa.
Viogozi wa Afrika wakimaliza mkutano wa 19 wa kawaida wa Umoja wa bara hilo makao makuu ya Umoja huo jijini Addis Ababa. Pamoja na kumchangua kiongozi mpya mtendaji bi Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye anakuwa mwanamke wakwanza kuuongoza umoja huo, viongozi hao wamekubaliana pia kuangalia na kuifanyia kazi migogoro mikubwa miwili inayoendelea barani humo. Mgogoro ule wa kaskazini mwa Mali na ule wa Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kiongozi mpya wa Umoja wa Afrika
bi Nkosazana Dlamini Zuma picha kwa hisani ya blogu wadau

Mama Nkosazana Dlamini Zuma akifurahia jambo. Picha na wadau