Saturday, November 17, 2012

MAZOEZI YA UFUNZAJI STEMMUCO 2012



Mwalimu wa hesabu akionyesha moja ya matumizi ya hesabu nyumbani

Kama ilivyo ada kwa waalimu wanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni STEMMUCO hupata fursa ya kufunza darasa dogo kila mwaka. Mwaka huu wa taalumu zoezi hilo limeanza Jumamosi ya tarehe 10 Novemba 2012. Vipaji, kujituma na uwezo wa walimu wanafunzi wa chuo hapo vimeendelea kudhihirika. Hapa ni sehemu kidogo ya kilichojiri katika moja ya Jumamosi hizo. 




Mwalimu wa Jiografia na mabadiliko ya hali ya hewa
















Mwalimu wa Kiingereza kazini
Mwalimu wa Historia kazini - Vita ya Majimaji

































  

TAMASHA LA MaKuYa

Tamasha la Ngoma za asili la makabila ya mkoa wa Mtwara Maarufu kama Tamasha la MaKuYa limeanza rasmi, huku vikundi mbalimbali vya sanaa vikionyesha umahiri mkubwa katika kucheza ngoma za asili za makabila yao.

Tamasha hilo ambalo mwaka huu lilianza kwa maandamano kutoka katika viwanja vya mashujaa kwenda Uwanja wa Nangwanda maarufu kama uwanja wa Umoja mjini Mtwara limevuta hisia za wakazi wengi wa mji huo na vitongoji vyake ambapo licha kuwepo kwa jua kali, watu waliendelea kumiminika uwanjani, mithiri ya maji mtoni, kushuhudia wasanii wakisakata ngoma mbalimbali.

Thursday, November 15, 2012

MHADHARA WA NJIA YA UFUNZAJI VYUO VIKUU - SAUT MTWARA (STEMMUCO)

Sehemu ya Chuo Kikuu Aalborg
Chuo Kikuu Kishiriki Cha Stella Maris Mtwara (Cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania) kilikuwa mwenyeji wa wanazuoni toka chuo kikuu cha Aalborg cha nchini Denmark.

Pamoja na kubadilishana mawazo wanazuoni wawili toka chuo hicho kikuu Profesa Jens Muller(PhD) na Profesa Mona Dahms waliotoa mada ambazo zilijadiliwa na wanazuoni wa Stemmuco ndugu Festo Gabriel na Profesa Eginald Mihanjo(PhD). Kisha mada hizo zilijadiliwa na wanachuo na wanataaluma waliohudhuria mhadhara huo.
Sehemu ya Chuo Kikuu Kishiriki Stella Maris Mtwara
Jens Muller, amebobea katika sayansi ya uhandisi, katika mada yake aliongelea suala la teknolojia mahalia na ulazima wa kuikuza teknolojia hiyo ili iwe na mchango kwa teknolojia ya dunia.

Gabriel Festo, akijadili mada hiyo alisisitiza kuwa jamii zetu nyingi za kale zimekuwa na teknolojia yake na wajibu wetu leo ni kuziendeleza na kujichochea jamii hizo kuziibua zaidi teknolojia hizo ili ziinufaishe jamii kubwa zaidi.

Mona Dahms aliongelea juu ya namna ya ufundishaji katika vyuo vikuu; alieza kuwa chuo chake kimekuwa kikifuata mfumo wa utatuzi wa matatizo katika ufundishaji. Alisema, tafiti zinaonyesha kuwa vijana wanaofundishwa kwa utaratibu huo wanaonekana kufanya vyema wanapokuwa kazi.

Eginald Mihanjo, mtaalam wa historia, aliwapongeza wanazuoni wa Aalborg kwa njia yao hiyo ya ufundishaji. Aliongeza kuwa huo ni mfumo mzuri ambao Tanzania iliutumia kupitia falsafa ya elimu ya Julius K.Nyerere aliyefuata na kusisitiza kuwa elimu iwe kwaajili ya kujitegemea. Mfumo huo haupo tena na hii ni hatari kwani vyuo vyetu vinaweza kutoa wahitimu wasio na ujuzi hitajika katika jamii.

Wednesday, November 14, 2012

TANZANIA NA KISWAHILI


Picha kwa hisani ya blogu ya udadisi
Kila nchi duniani hutambulika kwa mambo kadha wa kadha; Japan wanatambulika kwa ubobeaji wao kwenye teknolojia, Marekani wanatabulika katika kwa nguvu zao za kiuchumi, kisiasa, nk. Tanzania, pamoja na kutambulika kupitia mlima Kilimanjaro, mbuga nzuri za wanyama kama Serengeti, historia nzuri na kuvutia kupitia visiwa vya Zanzibar hutambulika pia kupitia Kiswahili.


Mlima Kilimanjaro  Picha hisani ya wwf
Nchi nyingi duniani huongea Kiswahili, hata hivyo Tanzania inaendelea kutambulika kuwa kiranja wa lugha hii adhimu. lakini je, lugha hii ina fursa zozote? Na je, watanzania wanazitumia vipi fursa hizo na ni kwa kiasi gani nchi ina nufaikanazo? Na jamii ya wanazuoni wana mchango upi katika ukuzaji wa lugha hii? Hebu tupitie sehemu ya hotuba ya waziri mkuu ndugu Mizengo Peter Pinda kama ilivyoandaliwa na blogu ya udadisi:  

IV UENDELEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
22. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge walipokea na kujadili pamoja na mambo mengine Maazimio mbalimbali. Niruhusu nirejee Azimio lililonigusa sana kuhusu Uanzishaji wa Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Awali, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Chama cha Kiswahili Tanzania (CHAKITA) na Wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuwa na Mpango wa Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Hata hivyo, Baraza hilo halikuanzishwa, badala yake ikapendekezwa kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Azimio la Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo ya Lugha ya Kiswahili tumelipitisha katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana mliyoitoa.....

Tuesday, November 13, 2012

KONGAMANO LA KIMATAIFA KUZUIA UHALIFU KWA VIJANA


Baadhi ya washiriki wa mhadhara wa kimataifa wa kuzuia uhalifu wa vijana katika jamii
White Sands Dsm 6-8 Nov 2012
Hivi karibuni Tanzania ilipewa uenyeji na taasisi ya haki na uzuiaji wa uhalifu ya Afrika Kusini (CJCP), kuendesha mhadhara (kongamano) wa kuzuia uhalifu kwa vijana. Mhadhara huo ilijumuisha wadau wa kada kadhaa: wanawake, vijana, watoto na yote ambayo yanalenga kuzuia uhalifu katika jamii. Mkutano huu ulifanyika hoteli ya White Sands (tarehe 6 - 8 Novemba 2012), Dar es Salaam.

Ndugu Msangi akitoa mada juu ya sera za jeshi la Polisi Tz















Mhadhara huu ulikuwa na mada anuwai zilizofanyiwa kazi. Malezi mema kwa watoto wangali wadogo kabisa, Njia mbadala za kuzuia uhalifu katika jamii, Polisi jamaa na vijana, Njia mbadala na fursa za kazi kwa vijana na kadhalika.

Ndugu Mandalu akitoa mada juu ya njia mbadala kupunguza
uhalifu miongoni mwa vijana















Wanamhadhara walitoka zaidi ya nchi ishirini na tano za mabara karibu yote ya dunia. Kwa hakika ilikuwa ni fursa nzuri kusikia wadau wa haki na amani wanavyofanya kazi kufanya dunia kuwa sehemu njema na ya kufaa kuishi sisi sote. Wanataaluma hawakuachwa kando pia, waliwasilisha tafiti zao zenye kutoa maelekezo na mwongozo wa namna ya kupunguza uhalifu katika jamii, wakati huo huo vijana, ambao ni wahanga wa fujo na wanawezeshwa kuondokana na adha hiyo. Inafahamika vyema kuwa wadau wakuu wa ujenzi wa dunia ni vijana, kwa kuwa ni kundi la watu wenye uwezo na nguvu kazi kubwa; kwahiyo basi ni muhimu kuwalea vyema wadau hao.   
Ndugu Muchunguzi akiwasilisha mada juu ya malezi