Thursday, October 31, 2013

Maonesho ya WajasiriaMali Mtwara




















Maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiria mali kutoka pande mbalimbali za nchi na  nchi jirani yamenza mjini Mtwara. Maonesho hayo yaliyoandaliwa na SIDO na wadau wenzi, yanalenga kuonesha bidhaa anuwai zitengenezwazo na wabunifu na pia kutafuta masoko toka kwa wadau. Mkoa wa Mtwara, ambao umesikika masikioni mwa wadau wengi hivi karibu kufuatia kugunduliwa kwa gesi asilia, unaanza kuwa moja ya masoko makubwa tarajiwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maonesho haya ambayo yamefunguliwa rasmi na ndugu mwenye dhamana ya viwanda vya Tanzania, ni fursa nzuri ya kuweza kuonesha bidhaa na mwanzo mzuri ya viwanda vyetu wenyewe kuanzia hatua za mwanzo kabisa. Kupitia wadau hawa wa bidhaa hizo ndogo, Taifa linaweza siku za usoni, kama tutaweka mkazo wa kutosha, kuwa na viwanda vyake lenyewe. Ili tuweze kufikia ndoto na lengo hilo ni muhimu kutengeneza mazingira ya kuwawezesha wajarisiliamali wetu kutengeneza bidhaa zao kwa gharama nafuu. Gharama za uzalishaji ikiwa ni pamoja na mali ghafi zikiwa  na bei ya chini, itawezesha wadau wengi kujiajiri na bidhaa zao zitakuwa na bei ya chini.

















Nasema hivyo kwa kuwa baadhi ya bidhaa nilizoziona zinauzwa kwa bei kumbwa mno ukilinganisha na ubora wake. Bidhaa  nyingi ni za asili kabisa na hivyo kuwa imara ukilinganisha na zitangenezwazo na makanjanja mjini, japokuwa ubora wake unahitaji kuongezwa zaidi ili zivutie wanunuzi wengi zaidi. Nilipohoji juu ya bei mmoja wabunifu wa bidhaa alisema: "nalazimika kuuza kwa bei ya juu kwa sababu nalipia kodi na  ushuru mbalimbali na pia kwa kuwa hakuna watazamaji wengi nauza bei ya juu ili kupitia mauzo haya nijikimu hapa mjini". Baadhi ya wadau hawa wa bidhaa asilia waliomba waandalizi wa maonesho haya wafikilie kuwalipia baadhi ya gharama ili kumudu vyema zaidi maonesho hayo. (Mwandishi hakupata fursa kuongea na timu ya maandalizi juu ya suala hili)

















Wakazi wa mjini Mtwara, hawajahamasika vya kutosha kutembelea maonesho hayo, jambo ambalo lingewezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao na kumudu kujikimu kupitia mauzo hayo. Hata hivyo ni fursa kwa wenyeji wa mkoa huo kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na maisha na utawala wa mazingira ya binadamu.

Kwa wajasiria mali, napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazozifanya, ila nawashauri pia waweke vitambulisho vya nchi zao wanakotoka ili kutambulisha bidhaa zao na pia kuzitambulisha nchi zao kibiashara zaidi. Hili linajumuisha kundika kwenye bidhaa jina la nchi bidhaa ilikozalishwa, kundika anuani  ama utambulisho uliojitosheleza ili mdau husika apatikane kwa wepesi kokote duniani. Ni muhimu kufanya hivyo kwani dunia imekuwa ndogo mno kupitia mapinduzi ya mawasiliano ulimwenguni.

Thursday, September 12, 2013

MTAZAMO MAISHANI


Bodi ya Korosho Mjini Mtwara

Bodi ya Tumbaku Mjini Tabora


Mtazamo wa nafsi yako mwenyewe - Picha kwa hisani ya wadau

Thursday, July 25, 2013

SIKU YA MASHUJAA NA UZALENDO TANZANIA


Sehemu ya wanajeshi wa Tanzania wakitoa heshima kwa Amiri Jeshi mkuu wa majeshi.
Picha kwa hisani ya BBC

Tarehe ya leo imeteuliwa kuwa siku ya mashujaa Tanzania. Ni tarehe waliyopokelewa wanajeshi wetu- mashujaa waliokuwa vitani nchini Uganda. Wanajeshi wetu walikwenda kazini kumnyoosha nduli Iddi Amini. Rais huyo wa zamani wa Uganda aliyejigamba kuwa na nguvu za kuchukua sehemu ya Ardhi ya Tanzania na kuifanya kuwa sehemu ya nchi yake. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999), kwa kutumia vigezo vya "vita halali" just war ya St. Augustine of Hippo 354-430  alitangaza vita kwa kuzingatia sababu inayokubalika, kujilinda dhidi ya adui, na kupigana vita kwa uangalifu na kupunguza maumivu kwa wasio na hatia. Vijana wa jeshi la Tanzania na nchi yote kwa ujumla tulishinda.

Tunapokumbuka mashujaa wetu, watu wengi hufikiria tu wanajeshi na wapiganaji wengine waliolipigania Taifa letu. Hapa utakumbuka watawala kama Mkwawa, Kimweri, Mirambo, Mputa, na wengine wengi. Ni vyema sana kuwakumbuka ndugu waliokuwa tayari kulilinda Taifa letu. Muhimu katika kumbukumbu hii ni suala zima la uzalendo. Watu wote tunaowatambua kama mashujaa, kwa namna fulani walikuwa na uzalendo mioyoni mwao. Hawa ni sawa na watu tunao watambu kama watakatifu, watakatifu huitwa wadhambi waliotubu. Nawafananisha mashujaa katika nchi na watu wenye "utakatifu" unapowapima kwa vigezo vya uzalendo. Kumbe tunapowaheshimu mashujaa wetu ni lazima tujitazame na kujipima uzalendo wetu.

Mzalendo tunamtarajia kuwa mtu mwenye kuipenda kwa moyo wake wote nchi yetu ya Tanzania. Katika hili kila mmoja na hasa wenye ofisi za Umma ama zozote zenye kutoa huduma kwa umma wa wanadamu, wanaalikwa kujipima, wanajali kwa kiasi gani maslahi ya wananchi walio wengi dhidi ya maslahi binafsi. Kiongozi anapopata fursa ya uongozi anatakiwa kufanya hivyo kwa niaba ya wananchi walio wengi; na ili aongoze vyema kuna mkataba unaomwelekeza kama anavyosema mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau(1712-1778) kwenye kazi yake ya The Social Contract (1762), kiongozi anafanya yale anayoelekezwa na wananchi na si anayotaka yeye; viongozi wangapi hivi leo hapa nchini wanazingatia anachosema mwanafalsa huyu. Wengi hawafuati makubaliano baina yao na wananchi, na kwa hivi wanalazimika kuacha mamlaka kwa wananchi wengine ili waongoze kama anavyosema mwafalsafa mwingereza John Locke (1632-1704). Locke anasema kiongozi mzuri anatakiwa awe na kumbukumbu ya makubaliano yake na wananchi moyoni mwake, vinginevyo aachie mamlaka.

Hivyo basi tunaweza kuwaenzi vizuri zaidi mashujaa wetu kwa kujitazama katika kioo na kuona kiwango cha uzalendo wetu kwa Tanzania yetu. Asanteni Mashujaa wetu na Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Thursday, July 18, 2013

SIKU YA MZEE MADIBA


Nadhani hii ndo siku pekee ambayo binadamu mmoja amepewa heshima ya kuwa na siku yake ya kimataifa duniani. Ndugu Nelson Mandela kapewa heshima hiyo hasa kwaajili ya kumaliza kwa amani, kupitia tume ya haki na maridhiano, mvutano ambao ungejitokeza baina ya weusi wengi, na jamii nyingine za watu wasio weupe wa asili ya Ulaya kwa upande mmoja, na wazungu wa asili ya Ulaya kwa upande mwingine.

Suluhu hiyo iliyohitimisha miaka mingi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kwa utulivu wa namna yake, ndo hasa sababu ya mzee Mandela kupewa heshima yote hiyo.