WAKATI wananchi wengi wakipongeza hatua ya Rais Dk. John Magufuli kuelekeza pesa zilizochangwa kwa hafla ya kuzindua Bunge kununua vitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wapinzani wake wanaeleza huo ni mwanzo wa kushindwa katika vita dhidi ya ufisadi.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Profesa Mwesiga Baregu amesema hatua ya Rais Magufuli kupokea pesa hizo bila kuhoji malengo na msingi wa Mhimili huo wa kutunga sheria kuchangiwa fedha ni ishara ya wazi kuwa ameingia kwenye mtego wa ufisadi wa kimfumo.
“Bunge ni taasisi nyeti sana kuruhusu kuchagiwa pesa na watu ambao linapaswa kuwasimamia, hizi taasisi za fedha zilizochangia zinaweza kujikuta zinatakiwa kuchunguzwa na Bunge, credibility yake itakuwa wapi. Angeuliza kwanza kwanini wamechangisha pesa hizo, nani anawajibika nazo?
“Kama anasimamia uadilifu hakupaswa kuchukua tu hela ambazo zimechangwa bila kujua dhamira za wachangiaji, huko tunakokwenda tunahitaji miswada ya kusimamia sekta ya fedha, sheria za kodi wanapolipia dhifa ya kwanza ya kufungua Bunge, huu ni mtego, kwani Bunge haliwezi kupewa uwezo wa kuchukua hazina kiasi kidogo hata kama ni shilingi milioni tano kufanya mambo yake, dignity (heshima) yetu iko wapi kama tuna Bunge omba omba na hatujui dhamira za wachangiaji?” alihoji Profesa Baregu.
Aliongeza kwamba huo ndiyo ufisadi wa kimfumo unaoitesa Tanzania, huku akiweka wazi kuwa anazofanya sasa Rais ni mbio za sakafuni kwa kuwa hawezi akadumu na hali hiyo.
“Mkapa (Benjamin, Rais wa awamu ya tatu) alianza na kasi kuliko hata hii, pamoja na juhudi kubwa za Mwalimu Nyerere, kumtangaza kuwa Mr. Clean, kuunda Tume ya Warioba kuhusu rushwa na kuwa na baraza aliloiita la askari wa miavuli, ameishia wapi, katika kipindi chake ndiyo kashfa nyingi za ufisadi zimeibuka. Simuoni kama atakuwa tofauti na watangulizi wake,” alisema.
Ni kama Nyerere
Wakati Profesa Baregu anayatazama mambo kwa jicho hilo mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Dk. Charles Kitima ameliambia Raia Mwema kuwa Rais Magufuli, amejipambanua kuwa ni aina ya kiongozi anayeweza kutekeleza anayoyasema kutokana na rekodi yake ya utendaji.
Amemweleza Rais Magufuli kuwa ni kiongozi wa kipekee ambaye hotuba yake ya kuzindua Bunge imeonyesha ni jinsi gani anaweza kuunganika na wananchi masikini wa ngazi ya chini.
“Hotuba yake imegusa watu wa kawaida kabisa, kama zilivyokuwa hotuba za Mwalimu Nyerere, anasema kwa lugha inayotoka moyoni, pengine ni kwa sababu ameishi maisha ya kawaida, ndiyo maana ameweza kuwavutia wengi,” alisema Dk. Kitima.
Aliongeza kwamba ingawa hotuba za mwanzo za viongozi ni kujaribu kuwaaminisha wananchi kwamba atatekeleza ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni, utekelezaji wa ahadi hizo hutegemea aina ya kiongozi husika.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge pamoja na mambo mengine aliwekea umuhimu suala la kubana matumizi ya serikali ili fedha zinazookolewa zielekezwe kwenye huduma za jamii.
Ili kuonyesha alivyodhamiria kulitekeleza hilo, juzi Jumatatu, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Magufuli ameagiza kufutwa kwa sherehe za uhuru ili watu watumie siku hiyo kufanya kazi ya usafi.
“Hatuwezi kusherehekea miaka 54 ya Uhuru huku tukiendelea kusumbuliwa na ugonjwa wa kipindupindu unaoweza kuzuilika kwa kufanya usafi tu. Hii ni kejeli kwa taifa huru kwa zaidi ya miaka 50.
“Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wameagizwa kununua vifaa vya kufanyia usafi ili siku hiyo tuiadhimishe kwa utaratibu maalumu wa kupambana na kipindupindu,” alisema Balozi Sefue.
Akizunngumzia hotuba hiyo, aliyekuwa mtia nia ya kuwania urais kupitia CCM, Williamu Ngereja alisema hotuba hiyo ya Rais Magufuli ni mwanzo mpya kwa taifa.
“Hotuba ya Rais Magufuli ni mwongozo sahihi kwa taifa letu kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kama wananchi wanataka mabadiliko ya kweli, kama walivyoonyesha kwenye kampeni, kila mtu anapaswa kumuunga mkono,” alisema Ngeleja. -
CHANZO CHA HABARI HII :http://www.raiamwema.co.tz/magufuli-apasua-vichwa-wasomi