Wednesday, December 9, 2015

UHURU NA KAZI: KAZI YA TANU - KAZI YA MAGUFULI - KAZI YA WATANZANIA

Taken from Ndomi's Page
                                          Inapatikana hapa https://www.youtube.com/watch?v=b0Roj3MFrE4
Uhuru na kazi - Kazi ya Tanu. Maneno haya ama yanayofanana na haya yalikuwa ni moja ya salaam ambazo wananchi wa Tanganyika waliitumia kusabahiana mara baada ya uhuru. Bila shaka salaam hii ilitumika kutokana na umuhimu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya haraka.

Ni utamaduni mzuri kukumbushana masuala ya msingi ili kuweza kufanikisha jambo ama mambo muhimu katika jamii. Kauli mbiu ya ndugu John Pombe Magufuli (JPM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kampeni zake za uchaguzi mkuu  mwaka huu alitumia kauli mbiu ya HAPA KAZI TU! Kwa jinsi mambo yanavyoonekana kauli mbiu hiyo inaendelea kutumika wakati huu wa utendaji kazi zake za urais.

Kiongozi ni mtu ambaye huonyesha njia kwa kutenda. Na tena kiongozi mzuri huwa mbunifu na mweledi ili hali akitenda kwa mujibu wa sheria mama ya nchi yake. Hivi karibuni ndugu JPM alitoa agizo la maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika kwa namna ya tofauti kabisa na miaka mingine iliyotangulia. Kwa kawaida nchini Tanzania maadhimisho haya hufanyika kwa gwaride la ukakamavu toka majeshi ya ulinzi na usalama, halaiki, ngoma mbalimbali na matumbuizo anuwai. Lakini agizo la JPM mwaka huu limekuwa kwamba maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wa Tanganyika mwaka huu yafanyike kwa kufanya usafi maeneo mbalimbali zitolewapo huduma za kijamii.

Tumeshuhudia mwitikio mkubwa toka kwa wananchi waliojitokeza kufanya usafi katika maeneo mbalimbali. Ni jambo zuri wananchi kuitikia agizo hili ambalo pia limelenga kusaidia kupambana na ugonjwa wa kipindupindu. Moja ya sifa za kiogozi mzuri tuliona kwa ufupi ni kuonyesha njia kwa mfano; pichani hapo juu JPM anaonekana akishiriki kwa dhati kabisa katika kufanya usafi. Usafi huu ni muendelezo wa kauli mbiu ya HAPA KAZI TU!

HAPA KAZI TU! ni kauli mbiu nzuri inayofaa kutumika vyema na kwa undani zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Wakati kauli mbiu hii inahamasisha watu kutenda kazi, kuna watu wengine wengi hawana kazi na hivi kauli mbiu hii inakosa mantiki kwao. Hata hivyo kauli mbiu hii kama tulivyosema inatuhusu mno watanzania kwa kuwa nchi yetu bado ina uchumi duni. Hivi karibuni wadau wa HAKI ELIMU wametoa ripoti inayoelezea jinsi sekta ya elimu ilivyotenda ndani ya miaka kumi ya uongozi wa awamu ya nne.

Ripoti ya HakiElimu inasema awamu ya nne ilifanikiwa kwenye kuongeza idadi ya vitendea kazi katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya shule za msingi na pia za sekondari, vyumba vya madarasa, mtundu ya vyoo, maabara na kadhalika. Hata hivyo ubora wa elimu katika miaka hiyo kumi imekuwa duni. Kuna wanafunzi wamemaliza masomo pasi ya kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Hivyo ripoti hiyo inaisihi serikali ya awamu ya tano kuwekeza zaidi katika ubora wa elimu. Katika taarifa ya ripoti hiyo watoa mada walisema serikali ya awamu ya kwanza ilifanikiwa kwenye ubora wa elimu kwa kuwa waliweka falsafa ya kutolea elimu. Falsafa iliyotumika kipindi hicho ilikuwa ni elimu ya ujamaa na kujitegemea. Kupitia elimu hiyo wanafunzi walipata mafunzo anuwai wakati wakiwa shuleni. Mwanafunzi alipohitimu masomo yake aliondoka shuleni akiwa pia na ujuzi fulani ambao ungemwezesha kujiajiri ama kufanya kazi ndogo ndogo nyumbani kwao kulingana na fani aliyojifunza na hata aliposhindwa kuendelea na masomo tayari alikuwa na fani ya kuanzia maisha.
Makamu wa Rais aikishiriki zoezi la usafi katika eneo analoishi
Serikali ya awamu ya tano inayo nafasi pia ya kuboresha elimu kwa kauli mbiu ya hapa kazi tu. Kwa mantiki hii elimu yetu inafaa ibebe kauli mbiu hii ya kazi ambapo anaweza kufuata mbinu zilizotumika awamu ya kwanza. Hivi leo elimu yetu iwajengee wanafunzi wetu moyo wa kufanya kazi, iwapatie maarifa yanayohitajika na ambayo anaweza kuyatumia maarifa hayo ama kujiajiri, kuajiri wengine ama ayatumie atakapoajiriwa. Zaidi elimu yetu iwajengee vijana wetu uthubutu wa kutenda mambo, iwajengee uwezo wa kujiamini, iwasaidie kuibua na kuvifanyia kazi vipaji vyao ili wawe na uwezo wa kushindana katika soko la ajira. Ukitazama vizuri nchini mwetu utagundua kuwa kuna watu wengi toka nchi jirani katika nafasi zenye kulipa vizuri katika sekta binafsi kadhaa, sababu ya wageni kupata fursa hizo ni uwezo wa kujieleza kwa ufasaha katika lugha za kigeni hususani kiingereza. 
Waziri Mkuu akishiriki zoezi la usafi wa mazingira
Hivyo, wakati mjadala wa lugha ya kufundishia ukiendelea, wataalamu wa mitaala watazame mbinu za kuwezesha ufundishaji lugha mbali mbali kwa ufanisi. Ushahidi unaonyesha kuwa mwanafunzi anaweza kusoma vizuri na kumudu vyema kabisa lugha zaidi ya mbili. Ni dhahiri kuwa inatengemea pia kipaji cha mtu mmoja hadi mwingine lakini uwezo huo upo kwa binadamu na upo kwa mtanzania pia. Hivyo basi hapa kazi tu, Uhuru na kazi, kazi ya Magufuli, Kazii ya Mtanzania itakuwa na maana zaidi pale itakapowekwa katika falsafa ya kuongoza elimu yetu.

Mandalu Martin


No comments:

Post a Comment