Sunday, November 27, 2011

Huu ndo uzuri wa akili ya binadamu...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete akiongea na Ujumbe wa Chama cha CHADEMA

Ni busara sana kwa kiongozi wa nchi kukubali kukutana na viongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Ni busara hali kadhalika kwa CHADEMA kutoka na wazo la kuomba fursa ya kukutana na kiongozi wa juu wa nchi ili kujadili suala hili la msingi kabisa.

Nini viongozi hao wataafikiana ni suala la kusubiri na kujua. Moja ambalo ni dhahiri kwa hakika itakuwa ni fursa nzuri kabisa ya kuweza kufikia muafaka wa mtiririko sahihi wa utaratibu upi utumike kupata chombo cha kukusanya kuratibu, kujumlisha na kutoa majibu ya mawazo na maoni ya watanzania. Kumbe kuna njia lukuki za kusikilizwa kama sehemu moja inashindikana basi unajaribu njia nyingine. Ni vyema sana kuwa viongozi wa CHADEMA wameamua kufanya hivyo. Muhimu kuliko vyote ni amani ya kweli; amani ya kweli ni utulivu unaoendana na haki, hivyo wananchi tunahitaji utulivu lakini pia na hasa haki na usawa katika masuala yanayohusu maliasili za nchi yetu na maendeleo ya watu wake. Tanzania ni muhimu kuliko chama chochote cha kisiasa, Tanzania itakuwepo tu na si vyama vya siasa.  

Thursday, November 24, 2011

UTANZANIA HALISI

Bendera za vyama kadhaa vya siasa zikipepea nje
ya jengo la Nyumba ya Demokrasia - huko Buguruni Dsm


















Tanzania ni nchi ya kipekee sana hapa duniani. Ndani ya nchi hiyo kuna zaidi ya makabila 120, watanzania hao wana dini nyingi na tofauti tofauti mithili ya nyuki mzingani, itikadi za kisiasa anuwai, kuna vyama vya
kisiasa zaidi ya kumi. Pamoja na mambo yote hayo hulka ya watanzania ni kuishi pamoja bila kujali tofauti zao. Hili ni jambo la msingi na maana zaidi. Utanzania ni muhimu zaidi kuliko dini zetu, itikadi zetu za kisiasa, tofauti zetu za rangi, misimamo yetu ya kitaaluma na kadhalika. Kama jinsi ilivyo kwa Mungu, yeye ni muhimu zaidi kuliko dini ama madhehebu yetu, Mungu hana dini, analojia hiyo tunaweza kuitumia pia kwa Tanzania. Nchi yetu ni muhimu kuliko tofauti zetu zote kama jinsi ilivyo katika vitambaa hivi vyenye rangi tofauti tofauti lakini vyote vinawakilisha watu wa taifa moja la Tanzania. Mungu Bariki Umoja na amani yetu!