Picha zote katika makala hii ni kwa hisani ya
google
Oktoba, 5 ni siku ya walimu duniani. Siku hii ambayo kimataifa imeanza kusheherekewa 1994, ina malengo hasa ya kuikumbusha jamii ya wanadamu kuwa walimu ni muhimu kwa maendeleo ya jamii zetu na kwa dunia kwa ujumla. Ni fursa nzuri kuwakumbuka walimu ambao wamechangia sisi wote kuwa hapa tulipo.
Walimu ndio chanzo cha mafanikio katika kila sekta, kila mtaalamu, katika hali ya kawaida, huhitaji mwalimu wa aina yoyote ile ili kujifunza, kuboresha alichonacho ama kujifunza zaidi na kuwa imara zaidi. Kwa hivi hata wale wenye vipawa maalumu bado ni lazima wapate maongozo ya namna flani. Kwahiyo kimantiki, mwalimu inatakiwa awe ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana kiakili, uwezo mkubwa wa kuwafundisha wengine na si kinyume chake. Na zaidi tunahitaji walimu wengi ili kutoa ujuzi kwa watu wengi zaidi. Vigezo hivi muhimu vyatulazimisha watanzania kutafakari kwa kina mahitaji yetu ya walimu na ubora wao.
Kwa Tanzania, tunaungana na jamii ya kimataifa kusheherekea siku hii adhimu kwa jamii ya wanadamu. Ni muhimu kwa kuwa kila mmoja wetu ana mwalimu ama walimu wake ambao kamwe hawezi kuwasahau kwa jinsi walivyomsaidia na kumjenga kitaaluma, kiutu, kijamii na kadhalika.
Kama tulivyoona hapo juu, mwalimu ni mtu mwenye (anayepaswa kuwa na) mafunzo ama ujuzi maalumu kwaajili ya kuwafunza na kuwasaidia wengine. Mtu mwenye kufanya hizo inafaa awe na uwezo mkubwa wa kuelewa na kuwasilisha ujuzi huo kwa watu wengine. Ujuzi na uwezo wa mtu, kwa bahati mbaya sana, mpaka hivi sasa hupimwa kutumia vyeti alivyonazo. Vyeti hivyo huonesha matokeo ya mitihani mbalimbali ambayo mtu huyo alifanya; binafsi siamini njia hii ya namna ya kupima uwezo wa mtu, nakumbuka
HakiElimu waliwahi kusema elimu sio cheti bali uwezo. Kurejea kwenye mada yetu, swali hapa ni je, walimu wetu Tanzania wana sifa zipi na ni namna gani huwapata?
Sina rejea sahihi kuhusiana na uwezo wa
Mwalimu Julius Nyerere, ila simulizi za walimu wangu shuleni zinaonesha(hapa ni uvivu wa kufanya utafiti) kuwa alikuwa mwanafunzi hodari ndio maana akasomea ualimu. Mwalimu wangu darasani aliniambia kuwa huo ulikuwa ni utaratibu wa kikoloni kuwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa darasani wanakwenda kusomeshwa ualimu ili wafundishe wengine. Utaratibu huu ulikuwa na mantiki na maana kubwa sana. Mtu anataka kuwa mwalimu awe ni yule aliyefaulu vyema sana katika masomo yake, kwa kutumia vyeti, tuchukue wanafunzi wenye daraja la kwanza na la pili.
Na kwa taaluma zingine, ambazo pia ni muhimu kama vile utabibu, uhandishi, sheria, wanasaikolojia n.k kuwe na utaratibu utakaofaa; wanafunzi wote wakifundishwa vyema na walimu wenye uwezo mkubwa basi madaraja yoyote kuanzia la kwanza hadi la tatu yanaweza kutoa wataalamu wenye sifa takikana kabisa. Kwa hali ilivyo hivi sasa baadhi ya watu hapa Tanzania waidharau taaluma ya ualimu, kiasi cha kushauri mwanafunzi aliyefanya vibaya mitihani kusomea ualimu. Sasa hii, si sawa, kwa kuwa mwanafunzi ambaye hana uwezo wa kutosha kuelewa inawezekana kabisa akawa na uwezo mdogo wa kuelewesha wengine. Kwa hivi basi kuna haja ya kuangalia kwa makini namna tunavyowapata walimu wetu wa baadaye ili kupata kuwa na uhakika wa kupata wanataalamu wa fani zingine waliofunzwa na walimu wenye ujuzi na uwezo wa kufaa kuwapatia elimu hitajika. Kinyume na hapo tutapata wataalamu wasioiva sawasawa ni muhimu sana.
Ili wanafunzi wanaofanya vyema waweze kwenda kusomea ualimu na kufunza ni muhimu wakapatiwa motisha ili kuwahamasisha. Ni muhimu kufanya hivyo kuwa kila binadamu ana uhuru wa kufanya aonavyo muhimu ili mradi tu hadhuru ama haathiri haki za wengine. Kuwe na utaratibu na sheria ya namna ya kuwafanya wanafunzi waliofanya vyema zaidi kwenda kusomea ualimu. Hiyo inaweza kuwa moja ya malengo ya kimaendeleo ya taifa hasa wakati huu ambapo hapa nchini kuna shule nyingi kama zilivyo kata. Ili kuepuka kuendelea kuwa na takwimu kubwa ya shule bila ubora stahiki basi hilo tuliangalie.
Sifa stahiki za walimu zinatupeleka kwenye sifa stahiki pia kwa shule zetu. Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu, japokuwa, bado kuna mengi yanatakiwa kufanyika. Kuwa na shule kila kata ni hatua nzuri mno ya kimaendeleo, lakini aina gani ya shule ni muhimu zaidi kwa kuwa shule inaweza kuwa ni ukombozi ama utumwa. Mwanafunzi aliyefunzwa vyema yeye na jamii yote ya wanadamu itakuwa imekombolewa ilhali yule asiyefunzwa barabara atakuwa mzigo mkubwa kwa jamii; kwa vile atatazamwa kama aliyekombolewa na elimu. Mtu aliepata elimu katika mazingira duni ya kitaaluma ni mtu aliyeelimika nusunusu, mtu mwenye elimu nusunusu ni hatari kweli katika jamii kwani anaweza kuutumia, ashalkumu si matusi, umbumbumbu wake kuleta madhara akidhani kuwa anatoa msaada kwa jamii. Kwa hiyo wito hapa ni kuboresha walimu na mazingira yao ili wafanye kazi kwa uzuri na hivyo kuwa chachu kwa maendeleo ya taifa lote.