Mlima Kilimanjaro - TANZANIA, paa la Afrika, na Twiga, ambao hupatikana kwa wingi nchini Tanzania. Bila shaka hizi ni alama muhimu zinazoitambulisha TANZANIA na bara Afrika. |
Hivi tunu za Afrika ya leo ni zipi hasa? Tunu za Afrika ya kina Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Kenneth Kaunda, Houphouët-Boigny, Frantz Fanon, Nelson Mandela, n.k zilikuwa za umoja, kuungana, kushirikiana, uzalendo kwa bara letu, na kufanya kazi kwa bidii. Tunu za leo ni kuhakikisha kuwa kiongozi anashinda uchanguzi kwa mbinu zozote zile halali ama haramu, mashindano ya kujilimbikizia mali kwa wingi iwezekanavyo. Kwa majumuisho ni ushindani wa ubinafsi. Viongozi na raia wanajenga ubinafsi kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuzifanya nchi zetu kuwa vyama wanavyoweza kuvitawala kwa mihula mingi wapendayo wenyewe na mashwahiba wao. Nchi zetu nyingi hatujui hasa nini tunataka kukifanya; tuna maandishi, vielelezo na miongozo mingi mizuri lakini isivyofuatwa katu. Jambo tunalopaswa kujiuliza hapa ni je, kwa tunu hizi za kibinafsi bara Afrika linaweza kweli kuwa mshirika wa maendeleo ya dunia?
Afrika, nyumbani kwa watu zaidi ya milioni 900. Bara hili ni mama ya nchi zaidi ya hamsini. Wenyeji wa bara hilo huitwa Waafrika. Waafrika hawa wana asili mbalimbali; waafrika weusi, waafrika wenye asili ya bara asia, waafrika wa asili bara ulaya. Uanuwai huu unalifanya bara kuwa na utajiri wa tamaduni na hivyo kumiliki tunu kedekede. Kufuatia bahari hiyo ya tofauti, utaona kuwa kuna nafasi ya kupata tunu zilizo bora kabisa mithili ya mbegu za kisasa zenye kufanyiwa tafiti katika maabara na mashamba darasa ya wataalam wa kilimo.
Bara Afrika, kisayansi – daktari Leaky, lasemekana kuwa ndio nyumbani kwa binadamu wa mwanzo hapa duniani. Kwa mantiki hiyo bara hili ilifaa liwe limepiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile (kv) kisayansi, kijamii, na kadhalika kuliko ilivyo hivi sasa. Barani Afrika nyanja iliyopiga hatua kubwa zaidi ni ile ya kijamii. Nyanja nyingine zingali nyuma mno. Sayansi na teknolojia, elimu bora kwa ujumla wake vingali nyuma mno.
Uwanda wa masuala ya kijamii umepiga hatua kubwa barani humo. Ni hulka ya wanyama wote, wawe wa mwituni ama binadamu mwenyewe, kuwalea na kuwatunza watoto wao na pia kuishi katika jamii. Utaona kuwa kwenye eneo hili Afrika imepiga hatua kubwa hasa. Jamii nyingi katika Afrika bado huishi pamoja watu, familia kadhaa zinazotengeneza ukoo bado huishi pamoja. Ni jambo la kawaida kwenye familia za Kiafrika kuona ndugu wa mbali kabisa ama msaidizi akiishi na kutendewa vyema kama mtoto wa familia mwenyeji. Ni barani humo ndo kijana wa miaka hata thelathini huendelea kuishi kwa baba na mama akiwa tegemezi kabisa. Tamaduni za sehemu nyingine duniani humtaka kijana wa miaka kumi na nane aanze kujitegemea; ajitenge na aanze kujenga maisha yake mwenyewe. Ndugu wa mbali katu hathubutu kuishi na familia ya mbali naye. Tamaduni zote hizi zina mazuri na mapungufu yake, hata hivyo hii si mada ya leo. Kwa leo tuendelee na suala la sayansi na teknolojia hapa barani.
Kwenye uwanja wa sayansi na teknolojia bara Afrika linashika nafasi mbili muhimu, ya mwanzo na ya mwisho kabisa; hakuna mkaganyiko, nitaelezea:
Kwenye ubunifu, ufikirivu; utengenezaji na matumizi ya bidhaa za kiteknolojia bara hilo li nyuma kuliko mabara yote.
Kwenye matumizi ya bidhaa za kiteknolojia na kwa kuwa jaa la bidhaa duni, dhaifu, mbovu, zenye kukaribia kuisha muda wake na ambazo hutengenezwa ughaibuni, bara letu laongoza. Umeona, hakuna mkanganyiko wowote bali ni ukweli tupu ila tu wenye kuumiza.
Hivyo katika uwanda huu bara Afrika chini ya viongozi na waafrika wote kwa pamoja tunawajibika kujenga uzalendo wa kulipenda bara hili ili kuleta ustawi na maendeleo ya kweli kwa Waafrika na hivyo kutoa mchango kwa maendeleo ya dunia yetu. Kwenye moja ya mada zilizotangulia tuliona kuwa maendeleo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na tunu zilizo mahali husika. Kwa mtiririko huo wa kimawazo basi, tujiulize je, hapa barani Afrika tunu zetu ni zipi hasa?
Aina ya maisha na jinsi mtu anavyoishi, ikiwa ni pamoja na nyanja za kijamii, sayansi na teknolojia, husaidia katika kumuainisha binadamu husika. Waafrika kwa asili yao ni wakarimu, marafiki, wenye uteremeshi, na wenye tabasamu la kweli lililo karibu mno takribani muda wote. Furaha, bashasha juu ya binadamu wengine ni tunu zilizojaa pomoni maishani mwa mwafrika. Kwenye sayansi na teknolojia ili mmoja aweze kupiga hatua kubwa kwenda mbele ni wajibu kuwa na tunu za kujali muda zaidi, kujituma na hata kuwa mtumwa wa muda kwa kupangilia kila jambo linalotakiwa kufanyika, mtu kujali na kupenda kazi aifanyayo na kubwa zaidi uzalendo kwa nchi, na bara lake. Tunu hizi na nyingine zenye kuleta tija kwa kazi ni muhimu hasa kwa kufikia malengo mahususi ya maendeleo. Tunu hizi zipo pia barani Afrika lakini zimefichwa mno mithili ya vinasaba dhaifu visivyo na athari yoyote katika maisha ya binadamu. Kisha maelezo hayo basi ni muhimu mno kuimarisha tunu zinazoweza kuchochea maendeleo ya kweli.
Bara Afrika kongwe kwenye tunu za ukarimu, upendo, undugu, n.k limeishangaza dunia baada ya kutumbukia katika lindi la kuporomoka kwa utu na upendo barani humo. Kwa miaka kadhaa kumekuwa na vita pande nyingi barani humo. Vita nyingi barani humo zimechochewa na sababu nyingi za kibinafsi; uroho wa mali nyingi kupindukia, uchu wa mamlaka, na hata hamu ya utukufu binafsi. Jamii ambazo zilitazamwa kama zenye wema, upendo na utu wa hali ya juu ziliingia kwenye janga la mauaji na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa watu wao. Kumekuwa na vita pande zote; kaskazini, kusini, magharibi na mashariki hali kadhalika. Wakati jamii nyingi duniani kote zinaungana, baadhi ya jamii za kiafrika zinatengana, zinawindana na kudhoofishana badala ya kusaidiana kuleta maendeleo kwa watu wao.Tumeona kuwa watu hutambulika na kuainishwa kupitia tunu zao.
Hivi tunu za Afrika ya leo ni zipi hasa? Tunu za Afrika ya kina Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Kenneth Kaunda, Houphouët-Boigny, Fanon, Nelson Mandela, n.k zilikuwa za umoja, kuungana, kushirikiana, uzalendo kwa bara letu, na kufanya kazi kwa bidii. Tunu za leo ni kuhakikisha kuwa kiongozi anashinda uchanguzi kwa mbinu zozote zile halali ama haramu, mashindano ya kujilimbikizia mali kwa wingi iwezekanavyo. Kwa majumuisho ni ushindani wa ubinafsi. Viongozi na raia wanajenga ubinafsi kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuzifanya nchi zetu kuwa vyama wanavyoweza kuvitawala kwa mihula mingi wapendayo wenyewe na mashwahiba wao. Nchi zetu nyingi hatujui hasa nini tunataka kukifanya; tuna maandishi, vielelezo na miongozo mingi mizuri lakini isivyofuatwa katu. Jambo tunalopaswa kujiuliza hapa ni je, kwa tunu hizi za kibinafsi bara Afrika linaweza kweli kuwa mshirika wa maendeleo ya dunia?