Friday, October 5, 2018

WHO WILL CRY WHEN YOU DIE - NANI ATAKULILIA SIKU UKIFA?


Tafakuri ya uchambuzi wa kitabu kiitwacho: WHO WILL CRY WHEN YOU DIE (Nani atakulilia siku ukifa?),Na Robin Sharma.

Habari mpenzi msomaji makala hizi,ninatumai u mzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku,leo nimekuja na uchambuzi wa kitabu cha mwandishi Robin Sharma(WHO WILL CRY WHEN YOU DIE)  nakukaribisha nawe usome uchambuzi huu naamini kuna mengi utaenda kujifunza.

Kwanza kabisa katika maisha haya tunayoishi lazima tukumbe kuwa ipo siku yana ukomo wake,hakuna ambaye ataishi milele.Sasa je ulishawahi kujiuliza nani atakulilia siku ukifa?,mwandishi Robin Sharma anaeleza mambo 101 katika kitabu hiki lakini embu twende kuona haya machache na siku baada ya siku tutazidi kujifunza mengine.Karibu,

1.Chunguza na ujue wito wako ni upi? yaani uliletwa duniani ili uje kufanya nini? ukikaa na kupata jawabu,anza kuishi kwa lile kusudi uliloitiwa kuja kulifanya duniani ili uache alama yenye kukumbukwa na kila mtu hata siku ukiwa haupo tena duniani.

2.Jifunze kuwa na shukrani kwa watu,jijengee tabia ya kushukuru hata kama ulichopewa ni kidogo ila ukiweza kuthamini kilicho kidogo basi utaweza kuthamini hata kilicho kikubwa pia.

3.Simamia mitazamo yako,ili utimize lile kusudi ulilolipanga kulitekeleza.

4.Jifunze kuwa na nidhamu binafsi(self discipline),hii itakusaidia kuwa na nidhamu katika utendaji wa mambo yako bila ya kuyumbishwa tena utayatimiza kwa wakati muafaka.

5.Weka kumbukumbu ya yale uyafanyayo kila siku,andika katika notibuku yako ili uweke kumbukumbu na upate tathimini ni wapi pa kujirekebisha.

6.Jijengee tabia ya kuwa muaminifu.Unapotoa ahadi na ukashindwa kuitekeleza jua kwamba uaminifu wako unapotea kwa watu na mwisho wa siku utajikuta ukiangukia katika mahusiano mabaya na watu.Kaa chini kisha jitafakari ni mambo mangapi uliyoahidi ndani ya wiki na hujayatekeleza? ukipata jibu tafuta njia ya kujiboresha ili usirudie makosa.

7.Anza siku yako vizuri.Asubuhi ukiamka tenga japo dakika 30 za kujipanga kwa siku yako ujue kuwa itakwendaje na angalia tathimini ya siku yako iliyopita ila leo ufanye mambo kwa uzuri zaidi.

8.Jifunze kusema hapana.Hapa ipo shida kwa wengi,watu wanashindwa kujizuia kufanya mambo hata ambayo hayana faida yoyote kwao,embu jijengee tabia ya kusema hapana sio kila kitu ukiambiwa utende basi unakuwa mwepesi kutenda,ukifanya hivi itakusaidia kuokoa muda wako na kufanya mambo kwa uzuri zaidi.

9.Tenga siku yako ya mapumziko,jiwekee muda wako hata kama si siku nzima ila tenga masaa utakayopumzika na kupumzisha akili,ikiwa ni pamoja na kukaa na familia ama ndugu kisha ujipange kwa mwanzo mpya wa juma linalofuata.

Machache haya yanaweza kukusaidia endapo utachukua hatua ya utendaji,nami nikutakie kila heri katika hatua unayoenda kuchukua ya kufanya maamuzi ya kutenda.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha,mshairi na mchambuzi wa vitabu;
Marko Kinyafu
+255 714 129 520
Kinyafumarcos@gmail.com.

AMKA HAPO ULIPOKAA KUNA MAVUMBI,SIMAMA UJIFUTE NA UANZE KUSONGA MBELE.

Thursday, October 4, 2018

THE POWER OF READING BOOKS - NGUVU YA USOMAJI VITABU



Tafakuri ya  kitabu cha THE POWER OF READING BOOKS(Nguvu ya usomaji vitabu) Na. Shemeji Melayeki.

Mpendwa rafiki natumai haujambo,kwa wasaa mwingine natamani nikushirikishe mambo machache ambayo mwandishi Shemeji Melayaki ameyaelezea katika hiki kifupi kabisa chenye kurasa 14 tu,lakini kikiwa kimesheheni somo kubwa sana,basi nawe karibu twende pamoja.

Watu wakubwa waliowahi kuwapo na waliopo duniani mafanikio yao ukiwafuatilia utawakuta walikuwa ni wasomaji wakubwa wa vitabu,tabia ya usomaji vitabu imekuwa ni ngumu sana kwa watu kuiigia kutokana na uvivu mkubwa watu walionao na hali ya kupenda kuhairisha mambo na hii hujikuta kuona kama suala la usomaji wa vitabu ni la watu fulani au la watu wachache lakini hii si kweli,ila mtu yeyote atakae kufanikiwa sharti asome vitabu ili apate maarifa thabiti katika lile eneo analotaka kujinoa ikiwa ni katika kipaji,biashara,ujuzi,nk.Tabia huathiriwa na tabia hivyo tabia ya kutopenda kusoma vitabu itaathiriwa pale tu utakapo chukua uamuzi leo wa kuanza kusoma vitabu.

Description: 📚Yapo mambo mengi sana mtu hupata faida baada ya kusoma vitabu,machache miongoni mwa hayo ni kama;

-Maarifa humuongezea mtu nguvu ya kujiamini na kufanya mambo makubwa kwasababu anakuwa ana uhakika na lile alifanyalo.

-Maarifa yanamuongezea mtu nguvu ya ushawishi katika kutekeleza mambo makubwa,kwa sababu vipo vitabu vingi vinavyolezea jinsi watu walivyofanikiwa katika maisha yao mfano kitabu cha I CAN,I WILL,I MUST the keys of success kitabu hiki kinaeleza jinsi Dr Regnald Mengi alivyopitia changamoto nyingi hadi kufikia hapa alipo sasa,hivyo nawe kupitia kusoma kitabu utapata nguvu ya ushawishi wa kuona kuwa kumbe mambo makubwa yanawezekana endapo tu ukiamua kweli kuchukua hatua.

-Kitabu huyaunganisha mawazo ya msomaji na mwandishi wa kitabu kwa kupitia njia ya usomaji.

-Viongozi wote ni wasomaji vitabu(all leaders are readers),huwezi kuongoza kama hupendi kusoma vitabu.

-Maarifa ya vitabuni huunoa ujuzi wako na kukufanya uwe bora zaidi katika eneo lako unalofanyia kazi ikiwa ni biashara,kipaji,huduma n.k,Mungu mwenyewe hutumia kitabu kuweka taarifa zake,je si zaidi sana sisi wanadamu? ,Kutoka 32:33
*BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.*

Description: 📖MBINU ZA KUANZA KUWA MSOMAJI VITABU.

~Kwanza kabisa tafuta vitabu vya eneo ambalo unapenda kujifunza hii itakufanya uwe na hamasa ya kupenda kujifunza kila siku.

~Anza kwa kusoma kitabu kidogo kwa kuanza na kurasa chache chache mwisho utajikuta ukipiga hatua siku hadi siku kama vile wenye hekima walivyosema kuwa haba na haba mwisho hujaza kibaba.

~Soma kila siku.Usiache tabia ya kusoma japo kwa kurasa chache mwisho utajikuta hii itakuwa ni tabia yako ya kudumu.

~Fanya tafakuri ya yale uliyojifunza.Kufanya tafakuri ni sawa na mmeng'enyo wa chakula baada ya mtu kumaliza kula,nawe ukimaliza kusoma kitabu yaangalie yale uliyojifunza kwa kupiga picha na jinsi maisha yako halisi yalivyo,kisha chukua hatua ya kutendea kazi.

~Shirikisha wengine yale unayojifunza.Usiwe mchoyo wa kuwapa wenzio yale uyajauyo,kwa jinsi unavyozidi kushirikisha watu kile ukijuacho ndipo unapozidi kuwa bora zaidi(master) katika eneo hilo.

Anza leo kusoma vitabu ukianzia kwa hatua ndogondogo huku ukiweka nia ya kutamani kupiga hatua zaidi.Aonaye kununua kitabu ni gharama kubwa basi asubiri kulipa gharama kubwa zaidi atayoilipa kwa kutosoma vitabu.Mtu asiyesoma vitabu uhisi dunia ni kama sehemu ndogo ambayo unaweza kuizunguka na kuimaliza punde kama vile uzungukavyo kijiji,lakini si kweli,ila uhalisia ni kuwa dunia ina vitu vingi sana ambavyo kila siku tunatakiwa kujifunza na hatutavimaliza hadi siku tunakufa,basi anza leo nawe kuishi kiutoshelevu ili uje kufa ukiwa tupu.

Nikutakie heri wewe uendaye kuchukua hatua katika kutenda na hakika ipo siku utajishuhudia jinsi utakavyo kuwa mtu mpya siku baada ya siku katika eneo la maarifa.


Mimi Mwanafunzi wa shule ya maisha,Mchambuzi na mshairi.
Marko Kinyafu.
Description: 📞📩+255 714 129 520
Dar es salaam, Tanzania.

_Kuyatawala maisha huanza kwa kuitawala siku moja na siku yenyewe ndio leo_


THE POWER OF READING USEFUL BOOKS - KUSOMA VITABU VIFAAVYO HUONGEZA MAARIFA!


Ndugu msomaji wa blogu ya Wajenga Dunia,

Habari za siku nyingi? Bila shaka u mzima wa afya tele. Napenda kukukaribisha kwa mara nyingine katika ukurasa huu ili uendelee kujipatia maarifa yafaayo maishani.

Kuanzia sasa nakufahamisha kuwa tutakuwa tukifanya tafakari ya vitabu mbalimbali vyenye kukupatia maarifa na ujuzi wa mambo anuwai. Karibu sana. Kwa kila tafakari kutakuwa na mawasiliano ya mwandishi wa makala ama tafakari husika ili kama ukitaka kuwasiliana naye basi ufanye hiyo.

Martin Mandalu
+255 767 864 379

Sunday, November 5, 2017

SI MJAMAA, SI BEPARI JE, VIWANDANI TWAENDAJE?


Kila nchi huongozwa na falsafa fulani ili kufikia malengo iliyojiwekea. Tanzania ina dira ya miaka 25 kupitia maono yake ambapo nchi inajielekeza kwenye kundi la nchi zenye uchumi wa kati. Ili kufikia uchumi huo wa kati Tanzania imejiwekea mikakati kadhaa; mmoja kati ya mingi iliyopo ni ule wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi. Mwongozo unasema sekta binafsi ndiyo hasa itachukua nafasi kubwa katika kujenga uchumi wa kati; hayo yanapatikana katika Tanzania Development Vision  (TDV) 2025. Naam ni jambo muhimu kwa serikali kushirikiana na sekta binafsi kwani inafaa kuweka nguvu kubwa zaidi ili wananchi wengi waingie katika kundi hili kuzalisha ajira nyingi zaidi.

Hata hivyo ukisoma katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977, 3.-(1) inasema nchi yetu ni Jamhuri ya Muungano na ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa....,. Katiba katika nchi ndiyo hasa sheria kuu kuliko zote. Sasa basi kwa mantiki hiyo Tanzania ni nchi ya kijamaa! Je, kweli Tanzania kwa matendo yake, kwa jinsi inavyofanya mambo yake, kwa jinsi viongozi wake wanavyoishi na kutenda, ni nchi ya kijamaa kweli?

Swali hili na mengi mengine yanajadiliwa kwa undani ndani ya THE HIDDEN WEALTH OF TANZANIA. Kitabu kimeandikwa kwa lungha ya Kiingereza. Hata hivyo kimeandikwa kwa Kiingereza chepesi ambacho kijana aliyemaliza kidato cha nne atamudu kukielewa vyema kabisa. Kitabu kwa kiasi kikubwa kinawalenga wanavyuo, wakufunzi, wanataaluma na mtu yeyote anayependa kujua vyema mambo anuwai juu ya Tanzania. Kitabu hiki kinalenga hasa kuibua mijadala kutokana na hoja zilizomo ndani yake. 

Kwa sasa kitabu hiki kinapatikana katika maduka mbalimbali yaliyopo mitandaoni na pia katika mtandao wa Amazon. Hapo baadaye tutafanya utaratibu kuleta nakala hizo hapa nyumbani Tanzania.
http://www.amazon.com/dp/1978203284
http://www.amazon.co.uk/dp/1978203284
http://www.amazon.de/dp/1978203284
http://www.amazon.es/dp/1978203284
http://www.amazon.fr/dp/1978203284
http://www.amazon.it/dp/1978203284

Sunday, February 5, 2017

AZIMIO LA ARUSHA LINAPOFIKISHA MIAKA 50 : NINI KILISABABISHA KUZALIWA KWAKE?


Hivi leo Azimio la Arusha (AA) limefikisha miaka 50 ama nusu karne tangu kutangazwa kwake.... Tarehe 05.02.1977 ambayo ni miaka hamsini ama nusu karne iliyopita, lilitolewa tamko ama tangazo la kihistoria katika mji wa Arusha. Azimio hilo linaendelea kujulikana kama Azimio la Arusha hata hivi leo.



Lengo la Azimio la Arusha
Kimsingi lilikuwa ni kuboresha maisha ya Watanganyika wanyonge. Azimio la Arusha lililenga kuboresha nyanja zote za maisha ya wananchi wa kawaida lakini hasa ililenga kuboresha nguvu yao kiuchumi na kisiasa. 

Tanganyika ilijipatia uhuru wake wa kisiasa 09.12.1961 bila kufahamu kuwa uhuru wa kiuchumi uliendelea kuwa mikononi mwa wakoloni. Tanganyika ilirithi uchumi wa kibepari, tena ubapari wa kikoloni. Kwa mantiki hiyo utaona kuwa "sisi" tulikuwa na uhuru kisiasa ilihali "wao" walikuwa na uhuru wa kiuchumi.

Uchumi huo wa kibepari wa kikoloni ambao ulikuwa ukiongozwa kwa sheria za soko, ulikuwa kandamizi kwa wananchi wa kawaida. Wananchi waliofanya kazi kwa matajiri wa kigeni na kupangiwa mishahara kwa matakwa ya matajiri hao kabla ya uhuru waliendelea kufanya kazi kwa namna ile ile kama walivyofanya hata kabla ya uhuru wa kisiasa. Wakulima hali kadhalika walijikuta katika mazingira yale yale wakiuza mazao yao kwa mabwana wale wale na kwa bei zile zile za kabla ya uhuru.

Kutoka na uchumi ule wa kibepari, serikali haikuwa na uwezo wa kuingilia masuala ya uchumi huo na hivyo haikuwa rahisi kuwawezesha wananchi kuonja ama kushiriki katika furaha ya matunda ya uhuru. Hivyo basi kama ilitakiwa wananchi waonje ladha ya matunda ya uhuru wao basi ilikuwa lazima kwa TANU kudai ama kuchukua pia uhuru wa kiuchumi na mabadiliko hayo yalikuwa lazima.

Ili kusikiliza kusikiliza wananchi na kuhakikisha kuwa wanahisi faida za uhuru katika nchi yao, ndipo hapo chama cha Tanganyika African National Union kilipofanya maamuzi ya kihistoria.

Chama cha TANU kilitangaza za na historia mpya kabisa katika taifa changa la Tanganyika. Mnamo tarehe tano Februari mwaka elfu moja mia tisa sitini na saba pale mjini Arusha chama kilitangaza rasmi kuwa kuanzia siku hiyo nchi ya Tanganyika ilikuwa inaanza na inaingia katika siasa za ujamaa na kujitegemea.

Siasa ya ujamaa na kujitegemea ilijengwa juu ya nguzo mbili za (i) Utaifishaji wa njia zote kuu za uzalishaji mali na (ii) Vijiji vya ujamaa na kujitegemea kama nguzo muhimu kufikisha maendeleo kwa wananchi wengi.

Nini kilifanyika ndani ya siasa za ujamaa na kujitegemea? Hii ni mada ya wakati mwingine; kwa leo itoshe tu kuona kilichofanyika.