Thursday, August 6, 2015

Kwanini KIFO?

Life is a great surprise
Kwanini Kifo? Hili ni moja ya maswali ya lazima na ya mwanzo kabisa ambayo binadamu alianza kujiuliza toka zama za kale kabisa huko Ugiriki karne kadhaa kabla kuzaliwa Yesu Kristo. Swali hili lilikuwa lazima na muhimu enzi hizo na linaendelea kuwa hivyo leo pia.

Kabla ya kujibu kwanini kifo ni lazima kwanza kueleza kifo ni nini? Kifo kinaweza kuelezewa kwa mitazamo anuwai. kwa uchache tunaweza kutazama kile ambacho kinasema katika dini, biolojia kwa maana ya sayansi na falsafa. Sehemu ya maelezo ya dini juu ya kifo inapata ushawishi toka falasafa.

Dini mbalimbali zina mitazamo fulani juu ya kifo. Wayahudi, Wakristo, Waislamu, na Wahindu wanaamini katika maisha baada ya kifo. Na wanaamini kwamba mwili una sehemu mbili: mwili na roho. Katika muunganiko huo, binadamu anapofariki dunia, roho na mwili vinatengana. Dini nyingi zinaamini kuwa roho haifi bali inabadili mfumo wa maisha bila kuambatana na mwili.

Katika falsafa, binadamu ni muunganiko wa mwili na roho. Katika muunganiko huu roho ni mashuhuri na muhimu zaidi kuliko mwili. Roho haiathiriki na utengano wa mwili na roho. Pamoja na mitazamo tofauti katika falsafa toka kwa wanafikra mbalimbali juu ya kifo, kwa ujumla na kwa muhtasari katika falsafa, KIFO ni utengano wa mwili na roho. Hata hivyo wanafalsafa mbalimbali wana mitazamo tofauti tofauti si lengo la makala haya kupitia moni ya wanafalsafa hao.

Katika sayansi; kibaiolojia kifo ni mwisho wa shughuli zote za kibaiolojia mwilini. Hii inatokana na moyo kushindwa kuendelea kusukuma damu mwilini na hivyo ubongo kutopata oksijeni.

Sasa kwanini KIFO? Kwanza tukubaliane kuwa katika hali ya kawaida hili ni jambo la majonzi sana. Binadamu hupatwa na majonzi makubwa tunapopoteza wapendwa na ndugu zetu. Hii ni kwa sababu mara wanapofariki, basi katika maisha yetu yaliyobakia hapa duniani, kwa wingi wake kabisa pengine miaka mia moja, kamwe hatuwezi  kukutana nao tena. Wataalamu wa saikolojia hususani juu ya mambo ya kifo, wanasema kila kiumbe kinapofariki basi kilikuwa kimekomaa tayari kwa kifo. Sasa kwanini kuwe na kifo?

Wanafalsafa wanamitazamo mbalimbali yenye kutofautiana juu ya kifo. Epicurus yeye anasema kifo si chochote...Heraclitus yeye anasema kifo ni lazima kwaajili ya uhai wa ulimwengu. Anadai ili ulimwengu uendelee kuwepo basi ni lazima kuzaliwa na kufa kwa viumbe hai kuendelee kuwepo. Socrates hana hakika kwanini kuna kifo hata hivyo anatoa mapendekezo mawili. Mosi, kama ilivyo kwa Epicurus anaona kifo si chochote ila sawa na usingizi wa daima, ambapo mtu alala vizuri bila kusumbuliwa na chochote. Pili anaona kifo kama fursa ya mabadiliko toka katika hali tuliyonayo, ambayo anaona kuwa ni duni, kwenda kwenye hali iliyo bora zaidi. Plato yeye anakitazama kifo kama fursa muhimu ambapo hatimaye roho inapata fursa ya kujikomboa toka katika gereza la mwili. Mtazamo wa Plato ni kwamba binadamu ni mwili na roho na kwamba roho ina hadhi ya juu zaidi na tena haikumbwi na mauti, haifi na wala haiozi kama ilivyo kwa mwili.

Kibaiolojia, kifo kinatokea kwa sababu mifumo mbalimbali mwilini inakuwa haiwezi tena kufanya majukumu yake kutoka na kuchakaa na kuishiwa uwezo wa kuzalisha viini uhai vinavyoufanya mwiili uendelee kufanya majukumu yake. Maelezo haya yanahusu mtu aliyefikia umri mkubwa mno yaani uzee. Lakini kuna sababu nyingine lukuki zinazosababisha mwili kushindwa kufanya kazi zake sawa sawa na hivyo kushindwa kwa moyo kusukuma damu mwilini. Ajali, magonjwa yasababishwayo na mfumo wa maisha tunayoishi, na kadhalika. Kisayansi kifo ni mwisho wa binadamu, japokuwa kuna wanasayansi wanaofanyia uchunguzi kuona kama kuna uwezekano wa maisha baada ya kifo.

Katika dini, kifo ni ukamilifu wa ubinadamu; kuzaliwa na kufa. kuna maisha baada ya kifo. Ni fursa ya kurejea kwa muumbaji na kutoa hesabu ya jinsi tulivyoishi maisha yetu hapa duniani. Hivyo japokuwa ni jambo lenye majonzi mengi kwetu tunaoachwa duniani, ni fursa kwa anayetuacha kwenda mbele ya muumbaji na pengine anaweza kuwa na ushawishi fulani ili tufanikiwe kuishi vyema kwa maombi yake na hasa kama yeye aliishi vizuri maisha yake hapa duniani.

Kumbe dini inatupatia matumai ambayo mimi pia nayaunga mkono kuwa wapendwa wetu tulioishi nao, tuliokula nao, tuliyoshirikiana nao mambo mengi hawaishii katika kifo na kuzikwa tu ardhini; kuna muendelezo wa maisha yao baada ya kifo. Na kwa imani yangu ya Kikristo ni kifo si mwisho wa kila kitu. Yesu Kristo alifufuka na kutupatia wanadamu matumaini mapya; maisha baada ya kifo. 

Sunday, June 14, 2015

CHEOSOMO WA DAR ES SALAAM


Image by google
Somocheo /Cheosomo wa Dar es Salaam kwa Nigeria ni Lagos, kwa namna fulani, Mombasa kwa Kenya, na tena kwa namna moja ama nyingine Johannesburg kwa Afrika Kusini. Na bila shaka orodha inaweza kuendelea kuwa ndefu ama kubwa mithili ya mpira wa thelujini.

Lakini hapa inafaa pia kujiuliza, je, Dar es Salaam ina shika nafasi ipi tunapotazama masuala ya miumdo mbinu yenye kufanikisha maendeleo ya watu na kukuza uchumi? Barabara zipo vipi? Reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini? Nishati ya umeme na kadhalika. Lakini pia kigezo cha amani na utulivu.

Kwa maoni yangu, kwa kutazama kwa makini na kwa takwimu zilizopo, Cheosomo wengi wa Dar es Salaam niliowaorodhesha wanaicha Dar es Salaam kwa mbali sana katika maeoneo mengi. Dar es Salaam, nadhani inatawaongoza cheosomo wake kwenye eneo la amani na kujaliana kuliko kwingine kote; hii ni kutokana na mtazamo jumla wa Tanzania kama nchi.

Hapa Chini ni Kenya
Sehemu ya Miundombinu Jijini Mombasa

Hapa chini ni Nigeria
Sehemu ya miundo mbinu Jijini Lagos 


Hapa chini ni Afrika Kusini

Picha zote kwa hisania ya mtandao wa google. Unaweza kuweka picha bora zaidi ya hizi, Zilizopo hapa zimetumika kufukisha ujumbe tu kwa wasomaji 

Wednesday, February 4, 2015

TUMIA FURSA VYEMA NJE YA NCHI YAKO

Na. Theddy Matemu Sawaki

Fursa zipo kila sehemu - This image for education purpose is taken from another website

Tofauti na elimu ya darasani lakini mambo ya elimu dunia Zingatia yafuatayo.

Ø  Kujali muda.
Ø  Kuheshimu kila mtu.
Ø  Kujituma.
Ø  Kujifunza lugha na tamaduni za wenyeji.
Ø  Kuwa msikilizaji zaidi ya msemaji.
Ø  Kuwa tayari kupokea ushauri toka kwa watu wote hata wa kada za chini.

Nimekuwa nikizunguka kwenye mitaa ya Mji wa Tokyo nikaja kugundua wahindi ni watu wanaojua kucheza na fursa wanazozipata. Sio kwa nchi zinazoendelea tu hata kwa nchi zilizoendelea kama Japani.

Na nikaamini kuwa darasani tu haitoshi kukufanya ukapata maendeleo ya Kimaisha. Kwa kuwa napenda kula nimekuwa nikizunguka katika mitaa ya Tokyo kutafuta chakula ninachokipenda. Nimekutana na migahawa ya Kijapani na kihindi na kitaliano.Migahawa ya kihindi ina sehemu ndogo sana ya kufanyia biashara naamnisha ukubwa wa nyumba maana jiko liko hapo hapo na viti vya kulia wateja viko hapo hapo karibu( ila kwa huku wamejitahidi kwa usafi sio kama wanavyoutufanyia kwetu Tanzania)hapo napo ni kipengele kingine cha kujifunza kumbe kuwa wasafi wanaweza isipokuwa ni namna gani nchi husika inajali wananchi wake.

Katika kufanya utafiti wangu wa kichumi usio rasmi (mimi sio mwana uchumi) nikagundua wahindi wameweza kujenga umaarufu katika biashara ya chakula na wana wateja wengi sana wenyeji wa Japani. Nikamwuliza mmoja wa wenye migahawa wa kihindi umewezaje kufanikiwa katika kupata wateja wengi akaniambia nina miaka 30 hapa Japani na kweli anaongea kiJapani kama amezaliwa nacho.

Kwanza kabisa alipofika hapa alijifunza lugha (naweza sema kwa Japani ili uweze kuishi vizuri ni vyema ujue lugha vinginevyo utapata shida katika huduma za muhimu),pia alijifunza tamaduni na mengine muhimu katika maisha ya waJapani. Hii ilimsaidia kuweza kuwasiliana na wateja wake, kujua nini wanapenda na nini hawapendi kujua jinsi gani angeweza kuwafanya wafurahie huduma zake. Haya yote alifanikiwa pale alipoajiri wafanyakazi wa kijapani wakati akianza biashara yake na kuwafundisha jinsi ya kuandaa vyakula vya kihindi nao wakamfundisha lugha na mengine yote ya muhimu.

Alipoona biashara imeshamiri alipunguza wafanyakazi wake. Baada yakupunguza wafanya kazi biashara ikayumba sana. Akaitisha kikao na wafanya kazi wake waliobaki kutaka kujua tatizo ni nini kama unavyojua wafanyabiashara wengi wa kihindi hupenda kuamrisha zaidi na huamini watu wachache tu.
Mmoja wa wafanyakazi akamwambia bosi ili biashara ikue warudishe wale wafanyakazi uliowapunguza kwasababu wanajua siri ya kazi na wameizoea na ndio walichangia biahara kukua. Hapo ndipo alipojifunza kwamba ili upate mafanikio lazima uamini kwamba kila mtu hata kama ni mdogo kiasi gani anaweza kuwa na mchango katika maisha yako. Muda mfupi baada ya wale wafanyakazi kurudishwa kazini biashara ikainuka mpaka leo na wateja wanajaa mpaka wanasubiria nafasi ya kuketi kwa foleni.

Nimejifunza Maisha sio kukaa darasani tu bali pia na hasa namna gani unaweza kuthubutu na kufanya chochote hata kama ni nje na nchi yako na ukafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, ili mradi kuwe na amani na utulivu katika nchi husika.



Saturday, November 15, 2014

MAISHA NI NINI? - What is Life? - Qu'est-ce que la vie?



Image by google

Hivi karibuni nimesikia kutoka radio Maria Tanzania kuwa wana mpango wa kuanzisha kipindi kipya juu ya maisha. Nimesikia wanauliza maisha ni nini? Swali hilo limenivutia kufanya tafakari. Kisha tafakari hiyo nikaona vyema kuwashirikisha watakaopata fursa ya kutembelea ukurasa huu.

Maisha ni nini? Ni swali linalohitaji kufikiria ili kulijibu na hakika mtu hawezi kutoa jibu la maana kama atafanya hivyo bila tafakari. Swali hili lahitaji maelezo ya utangulizi kabla ya kueleza maana ya maisha. Maisha yanahusu viumbe hai, swali letu linamlega hasa binadamu nami nitamuelezea binadamu bila kwenda kwenye falsafa ya ndani ya binadamu - philosophical anthropology, nitamuelezea binadamu kwa lugha nyepesi kabisa ili kila msomaji aelewe. Hivyo basi kwa kuanza na kiumbe huyu, binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi zaidi kuliko viumbe wengine. 

Kiumbe huyu huanza safari ya maisha baada ya mtu mume na mtu mke kushiriki tendo la ndoa na kutungwa mimba. Kisha kutungwa mimba kiumbe kipya kinaanza kuishi ndani ya mji wa uzazi wa mwanamke. Kuishi kwa kiumbe ndani ya mwanamke kunatupatia fursa ya kurudi kwenye swali letu la msingi la maisha, yaani maisha ni nini hasa?

Maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu toka kutungwa mimba hadi pale moyo (kiungo chenye kazi ya kusukuma damu mwilini sehemu zote za mwili na hivyo kuurutubisha mwili kwani damu ndiyo njia kuu ya usafirishaji mwilini) utakapokoma kufanya kazi yake.

Katika maisha ya kila binadamu kuna shughuli zinazofanana kwa viumbe wote na kuna shughuli zinazotofautiana toka binadamu mmoja hadi mwingine. Kwa kawaidaa shughuli zote za kimaumbile za binadamu hufanana. Shughuli hizo ni pamoja na zile zifanyikazo ndani ya mwili wa binadamu; ndani ya mwili wa binadamu kuna mifumo zaidi ya kumi inayoshirikiana kati yao na pia ikipata ushirikiano na idara kadhaa mwilini. Baadhi ya mifumo iliyo mwilini kwa binadamu ni pamoja na mfumo wa usafirishaji ambapo moyo na mishipa mwilini husafirisha damu na vyakula sehemu zote za mwili. Upumuaji ni mfumo unaotumia idara za pua, mapafu na kadhalika kuwezesha upumuaji wa mwili. Utoaji taka mwilini huhusisha idara kadhaa na hata mifumo mingine kufanya kazi hiyo...

Pamoja na shughuli zinazofanana kwa binadamu wote kuna mahitaji ya lazima ambayo ni muhimu kwa viumbe wote hao bila kuzingatia nafasi zao kijamii, kiuchumi na kadhalika. Chakula, hewa safi, na hifadhi ya namna fulani ni kati ya mahitaji ya lazima kwa binadamu wote.

Ili aweze kuishi vyema na mwili wake ufanye kazi, binadamu analazimika kula; lazima apate chakula katika kipindi fulani ili mwili wake uendelee kupata mahitaji na virutubisho vinavyouwezesha mwili kuendelea kuishi, hali kadhalika kwa hewa safi. Ili mwili uendelee na kazi zake lazima upate hewa safi ili kubadilishana kwa hewa safi (Okisijeni O2)  na hewa chafu (Kaboni diokisaidi CO2) kuendelee kufanyika. Binadamu wote huhitaji hifadhi ya namna fulani; toka kwenye mavazi hadi nyumba ya kujihifadhi, ni ubora tu ndiyo hutofautiana toka mmoja hadi mwingine.

Tunapojiuliza maisha ni nini kuna jambo la lazima kuligusa pia. Nini lengo la maisha? LENGO KUU LA MAISHA NI KUTAFUTA FURAHA. Kwenye dini tunaambiwa lengo kuu la maisha ni kumtumikia Mungu kupitia huduma kwa binadamu wenzetu na mwisho turudi kwa Mungu. Kwahiyo, kwa mara nyingine, kwa binadamu wote lengo kuu la maisha ni kutafuta furaha. Binadamu wote shughuli zetu zote, ama kwa kujua ama kwa kutokufahamu, ni harakati za kutafuta furaha na hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote binadamu anazozifanya katika harakati za kusaka furaha.

Binadamu wote bila kasoro, lengo la maisha yetu ni kusaka furaha. Tuliona mwanzoni kuwa binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi mkubwa kuliko viumbe wengine wote. Utashi na akili nyingi aliyonayo binadamu humpatia fursa ya kuitafuta furaha kwa namna ya kipekee kwa jinsi ya maumbile na muundo wake unaotokana na mpangilio wa 'genes' zake, ushawishi wa mazingira aliyolelewa na pia aina na ubora wa chakula alacho hasa toka utotoni. Ndiyo maana kuna wenye hutafuta furaha kwa kufanya kazi halali kwa bidii, wengine kwa kufanya kazi haramu kwa bidii (kazi haramu huleta furaha ya muda tu kwa kuwa huwadhuru binadamu wengine), wengine kwa namna yao kulingana na vipaji vyao na wengine kwa namna zao kwa namna namna.

Hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu katika harakati za kusaka furaha katika kipindi chote ambapo moyo unafanya kazi ya kusukuma damu mwilini!

Martin Mandalu
Alice, Eastern Cape
15/11/2014