UTOAJI wa Tuzo maarufuna muhimu za Nobeli kwa watu mashuhuri na wenye mafanikio ya kipekee katika
maendeleo na amani ya dunia umeanza kutiliwa shaka na baadhi ya wasomi barani
Afrika, na hususan wanazuoni katika baadhi ya vyuo vikuu Kusini mwa Jangwa la
Sahara, Raia Mwema, imebaini.
Mijadala ya chini chini
imeanza kurindima miongoni mwa wanazuoni, wakihoji kulikoni Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa kiungo katika ukomboni barani Afrika na hata
kushiriki kuratibu harakati za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,
asipewe tuzo ya amani.
Wakati tayari tuzo hizo
zimekwishatolewa kwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mwaka 2011, kwa
kupigania haki za wanawake ili washiriki kujenga amani, aliyekuwa Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, mwaka 2001, Askofu Desmond Tutu na Nelson
Mandela, hoja zimeanza kuibuka kwa nini si Mwalimu Nyerere?
Wasomi hao sasa wanakosoa
tuzo hizo na kudai kwamba Mwalimu ananyimwa kwa sababu aliyapinga mataifa ya
magharibi alipokuwa akiongoza harakati za kudai uhuru kusini mwa nchi za Afrika
na akishiriki kuunganisha nchi hizo, sambamba na kutetea haki za binadamu,
akiwa kiongozi aliyeishi kwa mfano mbele ya raia wake.
Wengi wanaamini Mwalimu
ni kiongozi wa mfano katika kuthamini usawa wa binadamu jambo ambalo ndilo
msingi wa amani ya dunia na kwa hiyo, alistahili kutunukiwa Tuzo ya Amani ya
Nobeli.
Tuzo hizo zilizoanzishwa
na raia Norway, hutolewa na kutambulika kimataifa ili kuwapa heshima watu
mashuhuri waliosaidia dunia katika nyanja mbalimbali za uchumi, amani, fasihi
na masuala ya sayansi kama fizikia, kemia, hisabati na mengineyo.
Wahadhiri wakosoa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), chuo ambacho Mwalimu alikianzisha na mara kwa mara
kufika hapo kwa ajili ya mijadala na wanafunzi kuhusu uhuru na maendeleo ya
Afrika na dunia kwa ujumla, Bashiru Alli, anaamini Mwalimu anastahili tuzo hiyo
lakini ananyimwa kutokana na kuyaudhi mataifa ya magharibi wakati aliongoza
harakati za kudai haki za binadamu na uhuru wa mataifa ya Afrika.
“Kuhusu maoni yangu juu
ya namna baadhi media (vyombo vya habari), wanazuoni na watu mashuhuri wa nchi
za magharibi wanavyopuuza mchango wa Mwalimu katika medani za mfumo wa siasa
uchumi duniani na siasa za mahusiano ya kimataifa. Maoni yangu ni kwamba
Mwalimu alikuwa mpinzani mkubwa wa mifumo yote kandamizi hususan mfumo dume,
ukaburu na ubeberu.
“Upinzani wa Mwalimu
dhidi ya mifumo hii ulimjengea heshima miongoni mwa wanyonge duniani kote, vile
vile alikuwa na maadui wengi ingawa maadui wake hawakufanikiwa kuutoa uhai wake
kama ilivyotokea kwa Patrice Lumumba wa Congo.
“Hata kama Mwalimu hakuwa
mmoja wa washindi wa Nishani ya Amani ya Nobel kama vile Neslon Mandela, lakini
mchango wake katika mapambano ya ukombozi hasa barani Afrika hauwezi kupuuzwa.
Hata kama mchango huo wa Mwalimu hautangazwi sana na vyombo vingi vya habari
vya magharibi au wasomi wengi wa nchi za Magharibi lakini maandishi yake,
hotuba zake na msimamo wake dhidi ya dhuluma, unyonyaji na ukandamizji ni
urithi usiokifani wa dunia. Sio rahisi urithi huu wa dunia hauwezi kupotea hivi
hivi,” anasema Mhadhiri Bashiru Alli.
Mhadhiri mwingine wa Chuo
Kikuu cha Stefano Moshi Memorial, Dk. Gaspar Mpehongwa, anasema vyombo habari
vya nchi za magharibi havikuwahi kumpa nafasi Mwalimu Nyerere kwa sababu
alikuwa “mwiba” kwa mataifa ya magharibi kutokana na hatua yake ya kukosoa kila
mara, sera zao za kibepari na ukoloni mambo leo dhidi ya nchi masikini za dunia
ya tatu.
Alisema kuwa sera za
Mwalimu za Ujamaa na Kujitegemea ziliendana na zile za mataifa ya na nchi za
kikomunisti za China na Urusi, hivyo mataifa ya Ulaya Magharibi yenye kufuata
sera za kibepari na uchumi huria yalimtenga.
“Mwalimu alikuwa black
listed na mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani kutokana na kuegemea zaidi
katika siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na hata vyombo vyao vya habari havikuwahi
kumsema vizuri,” alieleza Mhadhiri huyo.
Alisema Mwalimu Nyerere
alipinga sera hizo hasa Shirika la Fedha la Dunia(IMF) na Benki ya Dunia (WB)
taasisi ambazo zililenga kukandamiza nchi masikini hasa za dunia ya tatu,
Tanzania miongoni.
“Kwa bahati nzuri pamoja
na changamoto hiyo ya nchi za Ulaya Magharibi Mwalimu aliendelea kutambuliwa
kama moja wa mashujaa wa Afrika ambao walipigania maslahi ya nchi zao mbele ya
Jumuiya ya Kimataifa”
“Afrika iliheshimika sana
wakati huo kutokana na kuwa na viongozi wenye mtazamo chanya katika masuala ya
kiuchumi, kijamii na kisiasa tofauti na viongozi wa sasa ambao huitikia na
kucheza kila wimbo kutoka taasisi za Bretton Woods (mfumo wa kibiashara na
kifedha wa mataifa makubwa),”aliongeza.
“Kwa mfano leo hata
ukitaka uongozi wa umma vigezo vinavyotumika ni fedha badala ya uwezo wa mtu na
tabia hii imesababisha kuwa na aina ya viongozi katika sekta za umma
wanaojilimbikizia mali na madaraka,” alisema Mpehongwa.
“Na factor (kigezo) ya
uongozi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi angalia mfano nchi ndogo kama
Uswisi imeendelea kutokana na uongozi thabiti lakini Tanzania yenye rasilimali
nyingi kuliko Uswisi imeendelea kubaki kuwa moja ya nchi maskini na serikali
yake inajiendesha kwa kutegemea hisani ya nchi za Ulaya,” alisema.
Kwa upande wake,
Mwananahabari mkongwe na mwandishi wa vitabu nchini, ambaye baadhi ya vitabu
alivyoandika ni pamoja na “Harakati za Nchi zilizo Mstari wa Mbele na Unyanyo
wa Julius Nyerere,” Mkwabi Ng’wanakilala, anasema inawezekana kwa mfano, Nelson
Mandela na Mwalimu Julius Nyerere walikuwa katika mizani tofauti ya kimtazamo
na kwamba ndiyo sababu inayowafanya wapate heshima tofauti hasa kwa watu wa
Magharibi.
Kwa upande wa Nelson
Mandela, anasema, hali yake ilikuwa ngumu kwa sababu hakuwa anafukuza wakoloni
isipokuwa alikuwa anapigania maslahi sawa ya Waafrika Kusini weusi dhidi ya
makaburu, wakati kwa upande wa Nyerere kazi ilikuwa ni kuwafukuza wazungu
waondoke Tanganyika.
“Mandela alionekana kama
mtu ambaye hatakuwa na madhara makubwa kwa uwekezaji na maslahi ya wazungu na
makaburu Afrika Kusini, walijua wanaweza kumpa anachotaka bila kupoteza
chochote, na ndiyo hali inavyoonekana mpaka leo, Waafrika weusi bado wana hali
ngumu kiuchumi kama ilivyokuwa wakati ubaguzi,” anaeleza.
Anafafanua kuwa pamoja na
kwamba Mandela ni mpigania uhuru na ukombozi wa Afrika na amekaa jela miaka 27
kwa ajili ya kupigania ukombozi wa mtu mweusi, lakini ni kama nchi za Magharibi
zilimtumia kimkakati kwa mantiki kwamba anaweza akawafanya wakaishi kwa amani
kwa kuwa atakubalika na wote, weusi na makaburu.
“Hata ukiangalia release
(kuachiwa toka jela) yake ni kama ilikuwa staged (ilipangwa kimkakati) ili
kuweza kukidhi matakwa yao kutokana na shinikizo lilikuwapo wakati huo, na
walipomwachia amekuwa Rais na haki za weusi kupiga kura na mambo mengine
wamepata lakini kwa kweli bado kiuchumi hali haijabadilika sana ni kama ile ile
tu” anasema.
Anasema kuwa huyu ni
lazima asifiwe kwa kuwa ni mtu ambaye hana madhara makubwa sana kwao, kuendelea
kumsifia ni kujihakikishia kuendelea kujiimarisha katika hali waliyo nayo
tofauti na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wa Mwalimu
Nyerere anasema alikuwa anataka uhuru kamili katika nyanja zote, na alikuwa
anawaambia ukweli bila kujali watamtafsiri vipi, na kwamba ilifikia kipindi
wakaumuona kama mkomunisti lakini kimsingi hakuwa mkumnisti yeye alibaki kuwa
mjamaa hata kama alikuwa na marafiki China na Cuba.
“Mwalimu kama ilivyokuwa
kwa Nkrumah walitaka kuvunja vunja kabisa mizizi ya unyonyaji, wamchukia kwa
sababu ya impact (matokeo) ya misimamo yake, he was very disturbing (alikuwa
msumbufu sana) kwao, haikuwa rahisi kumfanyaia ujanja ujanja” alisema.
Kwa upande wake Makamu
Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Charles Kitima, anasema kuwa
Mwalimu Nyerere hawezi kuwa maarufu na kusifiwa na watu ambao aliongoza juhudi
za kuwakatia mirija ya kunyonya rasilimali za Afrika.
Anasema Mwalimu Nyerere
aliongoza juhudi za nchi zilizo mstari wa mbele kwa kuwaunganisha Waafrika
kupinga aina zote za unyonyaji wa wakoloni na koloni mamboleo kitu ambacho
hakikufurahiwa na wakubwa wengi wa Magharibi.
“Asingeweza kuwa maarufu
kwa watu ambao aliwanyang’anya ulaji, kumbuka ni juhudi zake ndiyo
ziliwaunganisha Waafrika nay eye akawa Mwenyekiti wan chi zilizo mstari wa
mbele kuwapinga hawa,kwao mtu wa namna hi hawezi kuwa shujaa hata siku moja”
alisema.
Anasema kwa Afrika kwa
kiasi kikubwa inajitahidi kumkumbuka na kumuenzi ambapo sasa baadhi ya nchi
kama Rwanda wana maadhimisho rasmi ya kumuenzi Mwalimu na Umoja wa Afrika
umeanzisha Scholarship kwa heshima ya Mwalimu.
Mwalimu Nyerere African
Union Sholarship Scheme imeanzishwa kwa ushirkiano na India kuwasomesha Wanafunzi
wa Afrika katika vyuo mahiri Afrika, katika fani ya sayansi na teknolojia kwa
ngazi za shahada, shahada za uzamili na uzamivu.
Chuo Kikuu cha Edinburgh
ambako Mwalimu alichukua shahada yake ya uzamili mwaka 1949, kilianzisha The
Julius Nyerere Master’s Scholarship mwaka 2009, kwa ajili ya wanafunzi wa
Tanzania kusoma katika chuo hicho.
Dk. Kitima anasema kuwa
sababu nyingine ambayo inafanya Mwalimu asipate heshima hiyo ni jinsi serikali
inavyosimamia masuala ya msingi aliyoyaanzisha, kwamba udhaifu huo ndiyo
unafanya hata watu wengine wasione mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Afrika
huru.
Ameshauri ni muhimu
serikali kurejesha somo la historia shuleni ili wanafunzi wajifunze historia ya
nchi yao na kuwatambua mashujaa wao na hapo ndipo wanaweza kusimama kidete na
kuitetea hadhi ya taifa lao.
Naye Mwanasheria Edward
Lekaita alieleza kuwa mataifa ya magharibi pamoja na vyombo vya vya habari
hayakuweza kutambua mchango wa Mwalimu kutokana na tabia yao ya kujali masuala
yenye maslahi na mataifa yao.
“Vyombo vya habari vya
magharibi siku zote ajenda yao kubwa ni kuandika habari zenye maslahi na
mataifa yao hasa habari nyingi za mataifa masikini Afrika na yale ya Bara la
Asia”
“Walikuwa double standard
(ndimi mbili) katika masuala mengi ya msingi kwa mfano walitambua umuhimu wa
Nelson Mandela baada ya kutoka gerezani na kuioongoza Afrika ya Kusini huru
lakini kabla ya hapo walimtabua kama gaidi.”
Alisema Mwalimu na
wenzake kama Nkwame Nkrumah wa Ghana, Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini,
Lepold Senghor wa Senegal walijitahidi kuwaunganisha wananchi ili kuondoa
ukoloni na ubaguzi katika nchi zao.
“Ni aibu mambo
yanayofanyika sasa ni kinyume na dhamira iliyowasukama viongozi wetu wa zamani
kupigani uhuru kutoka kwa wakoloni hata wakati mwingine kuhatarisha maisha yao”alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya
wakazi wa Mbeya waliozungumza na mwandishi wetu wanamueleza Nyerere kama
masikini jeuri, kwamba katika harakati zake za kupigania haki na utu kwa
wanadamu wote hakujali mabavu ya mataifa makubwa wala uwezo wao mkubwa kifedha.
“Nyerere alikuwa masikini
jeuri, alikataa kufanya biashara na Makaburu wa Afrika Kusini, hatua
inayotugharimu hadi leo, lakini heshima ya msimamo wake tunavivunia hadi leo,”
anasema mkazi wa jiji hilo, Newton Kyando.
Kyando anatoa mifano
zaidi kuonyesha ujasiri wa Nyerere kupigania haki za wanyonge duniani,
akikumbuka namna Mwalimu alivyokataa kuitambua serikali ya Mlowezi Ian Smith,
alipojitangazia uhuru wa Zimbabwe, wakati huo ikijulikana kama Northern
Rhodesia. Mbali na uamuzi huo, Nyerere akipata kuvunja uhusiano na Israel
akipinga uonevu dhidi ya wananchi wa Palestine.
“Nyerere alivuka mipaka
ya dini, alikuwa mkristo safi, tena mkatoliki, lakini alivunja uhusiano na
Israel kupinga uonevu dhidi ya Wapalestina ambao wengi ni Waislamu, alichokizingatia
yeye ni haki za wanyonge na utu wa mtu,” anasema Kyando kisha anaendelea
akisema, “Pamoja na Chama cha ANC cha Afrika Kusini kilitangulia kuanzishwa,
ilikuwa ni TANU iliyokijenga kufikia pale ilipofikia leo hadi kufanikiwa
kupatikana kwa uhuru wa Afrika Kusini, na unapotaja TANU unamtaja Mwalimu
Nyerere,” anasema Kyando.
Wananchi hao wanakumbuka
pia mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye medani ya kimataifa, ikiwamo kuwa msemaji
wa “South South Commission,” pamoja na ukweli kwamba yalikuwamo mataifa makubwa
na yenye nguvu za kiuchumi kama vile China na Indonesia.
“Alikuwa ni Mwalimu na
Helmut Kohl wa Ujerumani Magharibi wakati huo, waliokuja na wazo la haki sawa
ya kiuchumi kwa wote duniani, hivyo kunzaliwa kwa “International Economic
Order.”
Marekani kinara Tuzo za
Nobeli
Rekodi zinaonyesha kuwa
Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu waliopata tuzo nyingi zaidi za
Nobeli, wakifikia watu 334, ikifuatiwa na Uingereza tuzo 117, Ujerumani tuzo
102.
Katika Afrika, mbali ya
Ellen Sirlef wa Liberia aliyechangia tuzo hiyo na mwenzake, Leymah Gbowee,
wengine waliopewa tuzo hizo ni Wangari Maathai wa Kenya, Wole Soyinka wa
Nigeria (katika fasihi mwaka 1986), Kofi Annan wa Ghana (katika amani-2001),
Nelson Mandela na Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini. Misri pia imetwaa tuzo
nne.