Tuesday, October 14, 2014

Nyerere kupata tuzo ya Nobel ya Amani Mwaka 2100

The Nobel Peace Prize Medal. Registered trademark of the Nobel Foundation. © ® The Nobel Foundation
Medali ya tuzo ya Nobel
Tuzo za Nobel ni maarufu zaidi katika orodha ya tuzo mbalimbali duniani. Tuzo hizo ambazo zilianza kutolewa mwaka 1901, ni matokeo ya wosia alioucha Mswidi Alfred Nobel (1833-1896) mwaka 1895. Alipofariki alikuwa na utajiri mkubwa ambao alipenda uwaendee watu waliotoa mchango katika ujenzi na uboreshaji wa maisha ya binadamu katika dunia yetu. 

Tuzo za Nobel zimegawanywa katika makundi sita; watu wenye kutoa mchango uliotukuka kwenye Fizikia, Kemia, Biolojia(Tiba), Riwaya (Uandishi), Uchumi na wale wenye kujishughulisha na masuala ya amani.Tuzo hizi hupewa mtu ama taasisi/ asasi yeyote iliyo/ aliyefanya kazi bora katika moja ya maeneo tajwa hapo juu lakini pia asiyepingana/isiyopingana walau wazi wazi na fikra za kibepari na asionekane tishio kwa mfumo huo wa maisha.

Tuzo hizi wamepokea watu toka takribani mabara yote duniani. Hapa naangazia, japo kwa ufupi tu, tuzo ya amani ya Nobel. Ukitazama orodha ya wapokea tuzo hiyo ya amani utaona wapo waume kwa wake, wenye kujishughulisha na kazi anuwai, watu wa imani tofauti, wazee kwa vijana. Na kijana mdogo zaidi kuliko wote kuwahi kupokea tuzo hiyo ni bi Malala Yousafzai (1997). Binti Yousafzai ameshinda tuzo hiyo pamoja na mwanaharakati mwingine kwa mchango wao katika kutetea/kupigania haki ya elimu kwa vijana.

Litania ya washindi wa tuzo hii ya amani ni ndefu na yenye majina makubwa. Kwa uchache utamkuta Martin Luther King JrMama Tereza wa Kalkuta, Elie Wiesel n.k. Afrika ina uwakilishi mkubwa ambapo nchi ya Afrika Kusini ikiwa imetoa watuzwa wengi zaidi barani humo. Kwa uchache tu kuna Albert Lithuli(1898-1967); mmoja wa marais wa ANC na Mwafrika wa kwanza kupata tuzo hiyo, Nelson Mandela (1918-2013), Desmond Tutu n.k. Afrika Mashariki yupo kwenye orodha hiyo hayati Wangari Maathai (1940-2011 ) mwanamke wa kwanza barani kupokea tuzo hiyo kwa mchango wake kwenye upandaji miti.

Julius Kambarage Nyerere (1922- 1999) kiongozi wa kwanza mzalendo wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania, ni mmoja ya viongozi walioshiriki kujenga utu wa mtu duniani. Ushahidi wa mchango wake kutetea utu wa mwanadamu hususani binadamu mwafrika upo wa kutosha. Kwenye imani na kanuni za mwanaTANU, kanuni moja inasema binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja (sisemi kwa mpangilio kama ilivyo). Kiongozi huyu, kupitia sera ya chama na nchi yake, alijitoa kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa huru. Mchango wake ulikuwa mkubwa zaidi kwa nchi za kusini mwa bara hili la kitropiki, bara lenye kuandamwa na magonjwa ya kila namna ya asili na hata ya majaribio.

Sera za Tanganyika na baadaye Tanzania ziliruhusu wapigania uhuru wa nchi kadhaa za kusini mwa Afrika kuweka makazi yao na kufungua vituo vyao vya mafunzo nchini Tanzania. Mfano ni wapigania uhuru wa Afrika Kusini kule Morogoro, wapigania uhuru wa Msumbiji kule Mtwara na kadhalika. Zaidi wapigania uhuru na haki za watu kadhaa waliifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwa namna moja ama nyingine ambapo walijipanga na kuweka mikakati ya ukombozi wa nchi zao. Unaweza kuwataja wachache tu hapa Laurent Kabila (1939-2001) wa Kongo-Kinshasa, John Garang (1945-2005) wa Sudan, Yoweri Museveni (1944) wa Uganda

Tanzania kwa miaka mingi imekuwa nyumbani kwa wakimbizi toka nchi mbalimbali zenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.Tanzania na Zambia zinatajwa na mwandishi Crawford Young kwenye kitabu chake cha "The Postcolonial State in Africa: Fifty years of independence. 1960-2010" cha mwaka 2012, kuwa ni mataifa yenye makabila mengi lakini mataifa haya yameendelea kuwa ni nchi zenye amani na demokrasia. Nikiongelea AMANI ya Tanzania, pamoja na kwamba kuna tofauti lukuki kwa wananchi wake katika masuala ya imani, makabila na hivi karibuni itikadi tofauti za kisiasa, ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa mwanzo wa Tanganyika na baadaye Tanzania na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa miongoni mwao. Amani hiyo, pamoja na kuwa zawadi toka kwa Muumba, ilijengewa mazingira ya kustawi na viongozi hao wa mwanzo. Matumizi ya lugha moja - KISWAHILI, kwa taifa kubwa lililokuwa na vitaifa vingi (makabila) kabla na mara baada ya kupata uhuru, ni mbinu na mchango mkubwa uliostawisha na kuendelea kustawisha amani na mshikamano kwa Watanzania na pia kutoa hifadhi kwa binadamu wa mataifa mengine.

Mchango wa Tanzania kumfukuzilia mbali kiongozi wa mabavu wa zamani nchini Uganda Idi Amin Dada ilikuwa mchango mkubwa wa kazi ya amani kwa Tanzania, Uganda, Afrika na duniani kwa ujumla. 

Orodha hii inaweza kuwa ndefu zaidi, tukomee hapa kwa leo lakini tujiulize swali kwanini pamoja na mchango mkubwa amabao Tanzania imetoa katika masuala ya amani kwa ustawi wa binadamu nchi hii haijapewa zawadi hiyo na Nobel ya amani. Si kwamba bila tuzo hiyo maisha hayaendi la hasa, hata bila tuzo hiyo tunaendelea kuishi kwa mshikamano na udugu. Twauliza swali hilo kwa kuwa vigezo vinavyotumika kuwapima watu mbalimbali duniani inatakiwa ziwe kwenye mizani iliyo sawa.

Binadamu, kama ilivyo kwa maji huwa ana tabia ya kufuata mkondo katika maamuzi yake. Tanzania, kupitia Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa zama zake, ilikuwa ikifuata mfumo wa ujamaa na kujitegemea. Mfumo huu si rafiki sana kwa nchi za magharibi na hivyo Norway na hususani wakfu wa Nobel hata kama wanakubaliana na mchango wa Mwalimu Julius Nyerere si rahisi kwao kutaka kujihusisha na nchi ama kiongozi mwenye kujitangaza hadharani kuwa ni mjamaa, mfumo wenye kupingwa kwa nguvu zote na Marekani, Uingereza na jumuiya za kibepari zenye "kuufadhili" wakfu huo.

Mwalimu Julius Nyerere, kwa mtazamo wangu kupitia mchango wake kutetea haki ya wanyonge kwa mfano wake wa kujinyima, anastahili kupata tuzo hiyo ya amani. Tatizo ni kizazi hiki za watoa tuzo hizo na "wafadhili wao" wana upofu kwenye masuala yenye kugusa ujamaa na upofu huo nadhani utakwisha 2099 karne moja baada ya kifo chake. Ila wahenga walinena vyema mno na ni vyema kufuata maelekezo yao: Tenda wema nenda zako...  

Martin Mandalu
Alice, 14/10/2014

No comments:

Post a Comment